STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 28
SONGA NAYO............
MBAGALA
Asp Zalimo baada ya kupewa taarifa aliwahi mpaka nyumbani kwa akina Nayrah, baada ya kufika eneo hilo alishtuka sana baada ya kuona kulikuwa kuna gari tatu ambazo zilikuwa ni nyeusi sana, alichukua tahadhari huku mkono wake ukiwa upo kwenye kiuno chake ili kama kuna hatari aweze kuishi nayo kwa namna itakavyo kuja, licha ya kupewa maagizo na IGP kwamba akifika hilo eneo kuna watu ambao atawakuta hapo lakini bado hakuwa na imani sana na usalama wa hilo eneo kwa mazingira ambayo yalikuwa hayaeleweki hata kidogo. Baada ya kusogea zaidi karibu na hilo eneo aliweza kuona mbele yake kukiwa na gari ambazo zilikuwa za bei ghali mno alishtuka sana watu hao walikuwa wamekuja kutafuta nini hapo? Hakupata jibu hivyo alisubiri kama IGP akifika hapo aweze kumuuliza kuhusu ujio wa hao watu na wao ni akina nani hapo.
“Wewe ndiye ASP Bakari Zalimo?” aliuliza mwanaume mmoja ambaye bila shaka alikuwa kiongozi wa hao wenzake ambao walikuwa kama sita hivi, ilikuwa ni tofauti na matarajio yake, kuwa afisa wa polisi alihisi labda watu hao wangemheshimu sana ila kwao alikuwa wa kawaida mno na hata aina ya uulizaji wao ulikuwa ni kana kwamba wanaongea na mtu wa kawaida sana kwao, haikumpa shaka kuhusu kuelewa jeuri ya watu wenye pesa au ambao wanakula pamoja na watu wakubwa kwa mitazamo tu ya suti za bei ambazo walikuwa wamezivaa kwenye miili yao hivyo ilimfanya kuitikia kwa kichwa swali la huyo kijana ambaye kwake alionekana kuwa mdogo sana kwake.
“Yes ndiyo mimi” baada ya kulijibu tu hilo swali haikuchukua muda mrefu sana kijana huyo aliichukua simu yake na kuiweka sikioni baada ya kuwa na uhakika kwamba ilikuwa imepokelewa upande wa pili.
“Bosi huyu ASP amefika hapa tayari”
“Ok subiri dakika moja mlango utafunguliwa hapo ila msiwachukue kabla IGP hajafika hapo” upande wa pili ulijibu
“Sawa bosi” aliitikia na kuikata simu hiyo kitu ambacho kilizidi kumpa maswali mengi sana ASP Bakari kwamba huyo bosi wao ambaye alionekana kumpa maelekezo alikuwa ni nani hasa? Aliamua kuwa mvumilivu ili aje kula mbivu na muda huo huo walisikia mlio wa simu ndani ya nyumba hiyo. Wakati kijana huyo anaipiga hiyo simu yake Kwenda kwa Jason ilimkutia akiwa kwenye pikipiki akiwa anawahi ndani ya Sinza baada ya kupewa taarifa hiyo, aliamua kumpigia simu Nayrah ambaye kweli baada ya simu hiyo kuita tu dakika moja mbele alifungua mlango huo akiwa na mama yake tena wakiwa ni wengi wa wasiwasi sana.
Walishtuka kwani nje walikuta kuna watu kadhaa mbele yao akiwa amesimama ASP ambaye kwao walikuwa wanamjua sana tu, walisikia miingurumo ya mbali ya magari hayo ambayo yalikuwa hayatoi sauti sana ila haikutosha kutowapa wasiwasi maana hawakuwa wakijua ni nani aliyekuwa amekuja na walipewa taarifa na Jason kwamba hawatakiwi kabisa kuufungua mlango kabla ya yeye kuwapigia simu ila walitulia baada ya kumuona ASP ndiye ambaye alikuwa ameongozana na watu hao.
“Shikamoo mama” aliongea kwa sauti ya upole kijana ambaye alikuwa amevaa suti moja ya bei ghali mno.
“Marahaba mwanangu mzima wewe na wenzako” Kabla hawajajibu chochote walisikia muungurumo wa gari ndani ya ghari hiyo alishuka IGP tena akiwa mwenyewe bila kuwa na mlinzi yeyote yule
“Mzee unatembeaje mwenyewe na usiku wote huu?” ASP Bakari alimuuliza mkubwa wake wa kazi huku akiwa anatoa heshima kwa mzee huyo ambaye umri wake kidogo ulikuwa umeenda lakini alikuwa anaonekana bado ni kijana kwa sababu ya kulindwa na maisha mazuri ambayo alikuwa nayo.
“Ni kawaida tu kuna muda huwa natamani nitembee mwenyewe usiku kama saivi kwa sababu natumia gari ambalo hakuna mtu anaweza akajua kwamba mtu kama mimi nipo ndani yake” alijibu huku akisogea eneo ambalo walikuwepo mama na mtoto na kunyoosha ndani moja kwa moja baada ya kusalimiana nao.
“Mimi nadhani mnanijua sana kwa sababu ni mara nyingi sana huwa naonekana kwenye vyombo vya habari” aliuliza kwa sura ya tabasamu ili kuwatoa hofu watu hao
“Ndiyo tunakufahamu sana kwa sababu ni miongoni mwa watu wa mhimu sana kwenye kuchangia usalama wa taifa letu” alijibu mama yake na Nayrah huku Nayrah yeye akili yake haikuwa hapo kabisa alijiona kama vile alikuwa yupo kwenye ulimwengu wa mbali sana
“Sasa yule kijana aliyekuja hapa ni moja ya vijana wangu ambao nawajua kwa muda mrefu sana japo yeye hahusiani kabisa na haya mambo ya kipolisi ameniomba nije hapa ili kuhakikisha usalama wenu lakini pia kufanikisha suala la nyie kuhamishwa hapa na Kwenda kuyaanza maisha mapya huko Kigamboni. Mimi tutaachania hapa hapa kwani mtaondoka na hao vijana ambao wamevaa suti hapo nje ndio waliotumwa na huyo mtu ambaye alikuja hapa hao ni vijana wake hivyo kuweni na amani na muda wowote ule mkihitaji kuwasiliana naye basi mwambieni kiongozi wa hao vijana mtampata kwa wepesi sana japo amesema kwamba kuna muda atapotea kabisa kama miezi sita hakuna ambaye ataweza kumpata popote pale na baada ya huo muda ataweza kurudi yeye mwenyewe”
“Unaweza kuniambia anaelekea wapi muda wote huo na atakuwa salama?” Nayrah alidakia na kumfanya mzee huyo atabasamu sana, kwa wasiwasi wa huyo binti alielewa kilichokuwa kinaendelea hapo
“Kumbe huyu mjinga kujifanya amepata familia mpya ni kwa sababu ya huyu mwanamke” alijiongelesha mwenyewe kimya kimya mheshimiwa IGP huku akikaa sawa ili kumjibu mrembo huyo.
“Kiukweli hata mimi amegoma kuniambia kwamba kwanini anapotea huenda labda ana kazi ya mhimu ambayo anatakiwa kuimalizia ila kuhusu usalama wake usiwe na shaka yule yupo salama kwa masaa 24 ya kila siku ambayo inaenda kwa MUNGU, halafu wewe binti kesho unatakiwa ujiandae keshokutwa unaanza kazi Mhimbili maana ndiyo maagizo ambayo emeniachia hivyo kesho nitapiga simu pale uandaliwe kila siku ikiwemo ofisi yako mengine watakuelekeza wao wenyewe” mzee huyo aliongea huku akinyanyuka ili aondoke, alisikitika sana baada ya kuona namna binti huyo alivyofurahi kusikia kwamba anaenda kuanza kazi ndani ya hospitali ya Mhimbili ambayo ndiyo hospitali kubwa zaidi ya taifa ndani ya nchi ya Tanzania na huenda ni ndoto ya kila mtu anaye somea udaktari kuweza kufanya kazi ndani ya hospitali hiyo.
“Kazi kwenu mimi kazi yangu imeishia hapa” IGP aliwaambia vijana hao ambao walimpa heshima huku yeye akiwa anaelekea kwenye gari yake, alivyo mwangalia ASP Bakari alijua wazi kijana wake huyo alikuwa ana maswali mengi sana kuhusu hayo mambo ambayo yalikuwa yanaendelea hivyo alimpa ishara na kumruhusu aingie kwenye gari hiyo ambapo ASP huyo ndiye aliyetakiwa kuendesha.
“Mzee unajua sielewi elewi mambo yanavyo enda, unajua wakati nakuja huku nimesikia kama mlio wa risasi na kukawa kimya nilitamani sana kuwahi eneo ambalo risasi zilisikika lakini nilisita sana kufanya hivyo kwa sababu ulinisisitiza napaswa sana kuwahi huku halafu tena nafika huku naona mambo yanaenda bila kueleweka yanaendaje kwani ni nini kinaendelea mzee” aliuliza huku akiwa anaingiza gari kwenye barabara isiyo rasmi ambayo ilikuwa inatosha gari moja tu pekee kupita.
“Haya ya huku hayakuhusu kabisa kwa sababu ni mambo ya kifamilia, familia inahama tu basi hakuna kingine ila kuhusu risasi kusikika, kuna mauaji yametokea huko najua na kuna vijana wa kituo cha hapo karibu nimewapigia simu waje hili eneo ili wahakikishe hakuna ambaye anagusa hilo eneo kabla mimi sijaja”
“Whaaaat? Unamaanisha nini kusema unajua maana yake unamjua muuaji?”
“Ndiyo alivyo ua yeye mwenyewe alinitumia meseji kwamba kuna miili inatakiwa kusafishwa hapa kabla ya asubuhi kufika”
“Mzee huyo mtu anatakiwa kukamatwa haraka sana kama unamfahamu nafikiri hatakiwi kufika hata asubuhi akiwa bado yupo mtaani hiyo ni dharau kubwa sana yaani mtu anahusika na mauaji halafu anakutumia taarifa kiongozi mkubwa kabisa wa jeshi la polisi nchini?”
“Achana na haya mambo nitayamaliza mwenyewe” kiongozi wake alimjibu akiwa hana hata wasiwasi utadhani waliokuwa wameuawa hawakuwa watu bali yalikuwa ni machungwa tu na wakati huo walikuwa wamefika eneo hilo ambalo kulifanyika mauaji ya kutisha sana.
“Mzee uko sawa kweli? Yaani leo wewe unaniambia mimi tumuache muuaji? Au umelewa?”
“Ok kama unataka kumtafuta nenda ni huyo ambaye alikuja kwako kuzitafuta taarifa za mauaji ya kaka yake”
“Unamaanisha Jason”
“Ndiye huyo huyo” mzee huyo alimwacha ASP huyo kwenye mshangao mzito sana maana alikuwa haamini kabisa kwa aina ya mtu ambaye alimuona mbeke yake wakati amefika kwake, alikuwa ni mtu wa kawaida mno lakini huenda yeye ndiye ambaye alichelewa sana kumjua mtu huyo. IGP alisogea eneo hilo na kuanza kuikagua miili hiyo, alimwangalia mmoja ambaye shoka ilipita kwenye shingo yake ikawa imebaki kidogo tu itoweke kabisa huku akiwa ameyafumbua macho yake alikufa vibaya sana, aliusogelea mwili mwingine wa mtu ambaye alikufa akiwa hajatoka damu hata tone tu lakini sehemu yake ya kifuani pamoja na prova ambayo alikuwa ameivaa ilibonyea kwa ndani kumaanisha kwamba ni ngumi ya moyo ilipita hapo. Hakuhangaika na waliokuwa wameuliwa kwa risasi hao kilikuwa kifo cha kawaida tu bali alisogea kwenye mwili mwingine ambao ulikuwa upo pembeni pekeyake, kifua kilikuwa kimechanwa vibaya sana mpaka mzee huyo alifumba macho na kuingiza mkono wake mfukoni na kuitoa simu yake.
“Ndo haya mambo ambayo sikutaka kabisa aje kuyafanya, sasa vipi wananchi wakiona wenzao wameanza kuuliwa kwa namna kama hii, shiiiit” alitamka mwenyewe akiwa ameukunja sana uso wake, alipiga simu Kwenda namba ya Jason lakini haikuwa ikipatikana kabisa.
“Pokea simu wewe mtoto, pokea simu” alikuwa akiongea yeye mwenyewe huku akiwa anajaribu kuweza kupiga tena simu hiyo lakini kwa wakati huo haikuwa ikipatikana kabisa. ASP Bakari alikuwa akizunguka kuangalia namna miili hiyo ilivyokuwa imefanyiwa kitu kibaya sana.
“Hapana muuaji hawezi kuwa ni yule kijana, haya mauaji ni ya mtu ambaye hana nafsi ya binadamu, hakuna mtu mwenye roho ya kawaida anaweza kuwaua binadamu wenzake namna hii hapana mzee naomba uniambie tu ukweli kuhusu muuaji halisia ni nani” maneno ya ASP huyo yalimfanya mzee huyo kumgeukia kijana wake huyo na kumwangalia kwa hasira sana.
“Wewe huyo mtu ambaye unadai kwamba hawezi kufanya hivi unamjua? Unajua nini kuhusu yeye wewe hapo mtu ambaye hata kupigana na watu kumi na watano huwezi ila mwenzako hao anaweza kuwaua kwa dakika ambazo hata tano hazifiki na unapata jeuri ya kusema sio yeye"
"Unatakiwa uwe na akili kwamba kwanini alikufuata kwako na kukwambia kwamba ukae mbali na haya mambo siyo wewe wala mimi ambaye ana jeuri ya kulikamata hilo jitu, wewe ongea ongea tu hapo kwa sababu alikuja kwako kilokole mtu ambaye hata raisi wa nchi alikuwa akizungumza naye lugha ya upole itakuwa wewe hapo ambaye unakaa huku Mbagala? Angalia sana kauli zako mdomoni usije ukanifanya nikakupiga vibaya sana usiku huu hapa".
" Sasa nisikilize kwa umakini dakika kadhaa zijazo hawa watu ambao wameenda kuichukua hiyo familia watapita hapa muda sio mrefu wale vijana wake hii miili wameshaiona tangu wanapita mara ya kwanza japo wamepita njia tofauti na hii ila nina uhakika kwamba wameiona miili hii kwa sababu nao ndo wale wale hivyo ile familia ndiyo haitakiwi kujua lolote kuhusu hili wala raia yoyote yule wala chombo chochote cha habari, futeni ushahidi wote na hiyo miili ikazikwe haraka sana kesho watu waendelee na maisha yao kama kawaida wasije wakajua kuhusu haya mambo” aliongea kwa hasira na kupanda kwenye gari yake kisha akaondoka na kumuacha ASP huyo ahisi kama alikuwa anaota, alitamani sana kumtafuta mwanaume huyo ambaye alisifiwa sana mbele yake ili amhoji yeye mwenyewe alikuwa na jeuri gani ya kuua watu hovyo namna hiyo halafu wakuu wa jeshi la polisi wanamfichia hayo maovu yake.
Ngoja tumuone huyu ASP anacho kitafuta atakipta, binafsi sehemu ya 28 naweka nukta hapa tukutane katika sehemu inayofuata.
Wasalaam
Bux the storyteller.