WATU wasiojulikana wanadaiwa kuiba transfoma katika Kijiji cha Mafinga, Kata ya Kipengere, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, tukio lililosababisha kukatika kwa huduma ya umeme katika Kitongoji cha Makela.
Tukio hilo linadaiwa kutokea jana, majira ya saa tisa usiku, baada ya umeme kukatika ghafla na kuwaacha wananchi wakidhani kuwa kulikuwa na hitilafu ya kawaida katika mfumo wa usambazaji wa umeme.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafinga, Eses Chaula, amesema baada ya umeme kukatika, wananchi waliwasiliana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakihitaji msaada wa kurejesha huduma hiyo.
Amesema wataalamu wa TANESCO walipofika eneo la tukio na kufanya ukaguzi, walibaini kuwa transfoma ilikuwa imeshushwa kutoka kwenye nguzo na vifaa muhimu vilivyokuwa ndani yake kuondolewa.
Chanzo : Habari leo