Israel vs Iran - 2

Israel vs Iran - 2

Joined
Oct 5, 2015
Posts
90
Reaction score
482
ISRAEL vs IRAN - 02
Sehemu ya 2
Screenshot_2024_0530_184234.png

Na Dr. Chris Cyrilo
Mapinduzi ya mwaka 1979 yaliyoondoa utawala wa Shah, na kuifanya Iran kuwa chini ya utawala wa kiislamu wa dhehebu la Shia, yalifuta ndoto ya Iran kupata silaha za kinyuklia. Utawala wa kishia, uliokuwa chini ya Ayatolla Khomeini ulijikuta ukipigana vita dhidi ya Saddam Hussein kwa miaka 8, kuanzia Septemba 22, 1980 hadi Agosti 20, 1988. Saddam Hussein alikuwa akitumia silaha kali za kikemikali, gesi za sumu pamoja na mabomu ya Scud kiasi cha kusababisha vifo kwa mamilioni ya watu wasio na hatia. Kiongozi wa Iran, Ayatollah Khomeini alikataa kutumia silaha za kikemikali kwa sababu za imani ya kidini, lakini alisikitishwa kuona dunia imekaa kimya bila kukemea vitendo vya Saddam. Baadaye, Ayatollah aligundua kuwa Saddam alikuwa akipata msaada wa kivita kutoka nchi za Magharibi, hususani Marekani na jambo hilo likabadili msimamo wake kuhusu silaha.

Mwaka 1990 baada ya kifo cha Ayatollah Khomeini Iran iliamua kurejea mpango wake wa kumiliki silaha za kinyuklia lakini sasa ikiwa na marafiki wapya, Urusi, Uchina na rafiki mwingine mkubwa aliyeitwa Abdul Qader Khan, raia wa Pakistan na mwanateknolojia mashuhuri wa silaha za nyuklia katika ukanda wa mashariki ya kati. Abdul Qader Khan ndiye aliyeuza mitambo ya nguvu za kinyuklia kwa nchi Libya, lakini Iran haikutaka kununua mitambo bali michoro na maelekezo ili iweze kujitengenezea mitambo yake yenyewe.

Wakati huu, Israel ilianza kuangalia Iran kwa jicho la uadui kwakuwa Iran tayari ilikwisha kuwa adui wa Marekani ambayo ni rafiki mkubwa wa Israel. Uadui wa Iran na Marekani ulianza baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Shah na kuanza kwa utawala wa kiislamu wa Shia, mapinduzi yalioambatana na kuwatia kizuizini wanadiplomasia 52 wa Marekani waliokuwamo mjini Tehran kwa karibu miaka takriban miwili (1979 - 1981).

Baadhi ya wafanyabiashara wa Israel waliendelea kufanya biashara na Iran lakini kwa siri kubwa ili Marekani isigundue.

Nahum Manbar, ofisa wa shirika la Mossad alikuwa kiungo muhimu wa biashara ya silaha baina ya Israel na Iran. Zaidi ya silaha kutoka Israel, Manbar alifika hadi Poland kununua silaha na kuiuzia Iran iliyokuwa ikijiimarisha upya baada ya kuachwa hoi na vita dhidi ya Saddam Hussein. Manbar alifika hadi china kwa ajili ya kutafuta malighafi za kutengenezea silaha za kemikali na kuiuzia Iran. Mashushushu wa kiingereza wa MI6 waligundua biashara hii kwakuwa baadhi ya mipango ilifanyika mjini London, lakini iliwawia vigumu kuamini kama kweli Israel inafanya biashara ya silaha na utawala wa kishia wa Iran. Viongozi wa MI6 walibaki kuamini kuwa Nahum Manbar alikuwa na lengo la kuzama ndani ya jeshi la Iran ili kuchota tarifa muhimu za kiintelijensia kwa ajili ya Israel, ingawa haikuwa hivyo. Nahum Manbar alikuwa jasusi wa Mossad aliyefanya biashara na Iran kwa faida zake za kibiashara na si kwa faida za intelijensia ya Israel.

Shirika la Mossad na shirika la intelijensia la ndani ya Israel, ShinBet, kwa pamoja waliamua kumfuatilia Manbar. Katika operesheni moja huko mjini Vienna, Austria majasusi wawili wa Mossad wakiwa na pikipiki walikuwa wakifuatilia mienendo ya Manbar, lakini waligongwa na gari na wote wawili kufa papo hapo. Shirika Mossad liliamua kufanya uchunguzi wa tukio hilo ili kujua endapo ajali hiyo ilipangwa na intelijensia ya maadui au la, lakini haikuwahi kufahamika wazi na hakukuwa na sababu yoyote ya kumlaumu Manbar. Hata hivyo vifo vya majasusi wawili wa Mossad vilichochea hamu ya kumuadhibu Manbar kwa kufanya uchuuzi wa bidhaa za kikemikali kwa taifa adui. Mwaka 1997, Manbar alikamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa siri kubwa bila vyombo vya habari kujua, hatimaye alihukumiwa miaka 16 jela.

Jukumu la kudhibiti mpango wa silaha za nyuklia wa Iran lilikuwa gumu kwa Meir Dagan lakini hakutaka kushindwa kamwe ili asipate aibu kutoka kwa waziri mkuu Ariel Sharon. Wote wawili, Sharon na Dagan waliwahi kufanya kazi pamoja kama majenerali wa jeshi la Israel. Ili kutimiza jukumu hilo, ilikuwa lazima kuiimarisha zaidi shirika la Mossad kuliko lilivyokuwa awali. Mossad na Aman (intelijensia ya jeshi la Israel) waliamua kushirikiana pamoja katika kazi hii ngumu baada ya kujiridhisha kuwa mpango wa Iran wa kutengeneza silaha za Nyuklia ulikuwa unakwenda kwa kasi, kwa kusaidiwa na wanasayansi wa ndani hasa wabadhirifu wa vyuo vikuu na wengine kutoka mataifa rafiki.

Iran yenyewe ilitumia mbinu nyingi kuficha mpango huo, mojawapo ni kutumia shughuli za kijamii kama upanuzi wa miundombinu ya umeme na viwanda vya kutengenezea dawa za binadamu na bidhaa za kilimo. Lakini intelijensia ya Israel ilijiridhisha kwamba Iran wanatengeneza silaha za Nyuklia, na kukadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2004 Iran itakuwa inamiliki angalau bomu moja la nyuklia. Waziri mkuu Sharon alimwambia Dagan itakuwa ni hatari na jambo la aibu kwa intelijensia ya Israel, serikali ya Israel na wayahudi wote endapo Iran itamiliki hata bomu moja la Nyuklia. Kwa maneno hayo, Dagan alikuwa ametumwa vitani kwa sharti moja tu la kushinda, na vita hiyo ilikuwa ya kutumia silaha yoyote iliyopo. Dagan aliamua kuanzisha vita na Iran, vita ya kisiasa, kisaikolojia na kiuchumi kwa njia za siri za kiintelijensia.

Hatua ya kwanza ilikuwa ni kuharibu uhusiano wa kidiplomasia wa Iran na marafiki zake, pamoja na kutengeneza vikwazo vya kidiplomasia kutoka kwa jumuiya za kimataifa. Utawala wa Ayatollah ulipokea ujumbe mara kwa mara kutoka mataifa mengine ukiwalazimisha kuachana na mpango wao wa Nyuklia la sivyo hatua kali zitachukuliwa juu yao.

Hatua ya pili ilikuwa kuwashawishi washirika wa kibiashara wa Iran kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi ili kudororesha uchumi wa Iran. Mashirika mengi yalikuwa ya Ulaya, ambayo yaliaminishwa kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni hatari kwa mataifa ya Ulaya. Matumaini ya Israel yalikuwa kwamba Iran itaamua yenyewe kuacha mpango wa Nyuklia kwakuwa vikwazo vya kiuchumi vitadhibiti biashara zake, safari za viongozi na raia, mihamala ya kifedha na manunuzi ya bidhaa kutoka nchi za nje, zikiwemo bidhaa zinazotumika katika mpango huo wa Nyuklia. Kwa imani ya Intelijensia ya Israel, isingekuwa rahisi kwa Iran kuendelea na mpango wake wa nyuklia huku raia wake wakitaabika, ilihali ilikuwa serikali inaongozwa kwa misingi ya dini inayohitaji kuungwa mkono na wananchi wengi.

Hatua ya tatu, ilikuwa ni kujifunza kwa undani muundo wa kijamii wa watu wa Iran pamoja na makabila yao. Nusu ya idadi ya watu wa Iran ni waajemi (Persians), na nusu nyingine inaundwa na makabila kadhaa; Waazeri, Wakurdi, Waarabu, Mabaluchi, (Balushi) na Watukimini.

Watu wa makabila madogo walitazamwa kama watu duni na kuonewa kwa namna fulani. Hapo ndipo intelijensia ya Israel ilipopata mwanya wa kuanzisha vita ya kisaikolojia kwa kuwatumia wananchi wasio na furaha na kuwatumia kuisumbua serikali ya Iran.

Kwa siri kubwa, Intelijensia ya Israel iliwanunua baadhi ya viongozi ndani ya serikali ya Iran na maofisa waliofanya kazi kwenye mpango wa nyuklia ambao walishiriki kufanya hujuma kwenye mradi huo na kuua wataalamu waliokuwa wakifanya kazi kwenye mitambo ya ki-nyuklia.

Utafiti uliofanywa na Intelijensia ya Israel ulibaini kuwapo viongozi wa ngazi za juu wa Iran ambao hawawezi kushawishiwa kwa maneno bali kwa vitendo ili wajue kuwa mpango wao sio tu ni hatari kwa Israel bali pia ni hatari kwao. Serikali ya Israel haikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Iran, urafiki wao wa zamani ulibadilika kuwa uadui uliowabadili kuwa mataifa hasimu yanayowasiliana kupitia vyombo vya habari tu.

Kwa sababu hiyo, ilibidi Israel kutumia mataifa mengine ya Ulaya, Asia na Marekani kwa ajili ya kutuma na kupokea ujumbe. Marekani na washirika wake walikuwa wakifanya mazungumzo na Iran kila mara kushawishi nchi hiyo iachane na mpango huo, kisha taarifa kuhusu mazungumzo hayo zilifika Israel. Pamoja na hujuma zote hizo, Iran ilibaki na msimamo wake wa kutaka kumiliki silaha za Nyuklia, na kusababisha mataifa ya Magharibi kuiwekea vikwazo vya kiuchumi mwaka 2012.

Viongozi wa kisiasa wa Israel walishawishi Mossad kuanzisha vita halisi dhidi ya Iran, kwa kulipua maeneo yote ambayo mradi wa nyuklia ulikuwa ukiendelea, lakini maofisa wa Mossad walisita. "Mradi wa nyuklia wa Iran haukuwa hatari kwa Israel pekee bali kwa dunia nzima", ni kauli iliyotolewa na wanasiasa wakubwa wa Israel tangu wakati wa waziri mkuu Arier Sharon kisha Ehud Omert na baadaye Benyamin Netanyahu, lengo likiwa ni kushawishi mataifa mengi ya dunia kuichukia Iran na kuacha kushirikiana nayo. Hata hivyo, mbinu hiyo ilifanikiwa kirahisi kwa wanasiasa na watu wa kawaida, lakini sio kwa vyombo vya kiintelijensia vya mataifa mengine ambavyo vilijua fika kuwa Israel ndio ilikuwa hatarini na sio dunia yote.

Ilikuwa ni kazi ngumu kushawishi jumuia yote ya intelijensia ya dunia kuwa Iran ni nchi hatari kwani mwaka 2007, Rais wa Marekani George W. Bush alipokea taarifa kutoka Intelijensia ya Marekani kuwa Iran iliachana na mpango wake wa nyuklia tangu mwaka 2003 kwa hofu iliyotokana na uvamizi wa Marekani nchini Iraq. Kwa mujibu wa intelijensia ya Marekani, ni kwamba Iran iliogopa isije kuvamiwa na Mataifa ya magharibi kwa sababu Iraq ilivamiwa kwa vigezo vilivyotolewa na Marekani kuwa ni kumiliki silaha za maangamizi.

Kwanini dunia iamini kuwa taarifa za Israel ni sahihi kuliko za Marekani?

Itaendelea...
 

Attachments

  • Screenshot_2024_0529_191425.png
    Screenshot_2024_0529_191425.png
    459.1 KB · Views: 20
Back
Top Bottom