Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Mzazi yeyote anajua mojawapo ya kanuni kubwa za kumfunza mtoto; ni kumuacha wakati mwingine aanguke. Sasa humuachi aanguke mahali pa hatari au ambapo anaweza kuumia vibaya; bali unamuacha aangukie mahali ambapo ataweza kujipukuta na kusimama tena hata kama baadaya kulia. Hata ukimwambia pole; unajua hajaaumia sana lakini pia unajua atakuwa mwangalifu mara nyingine tena. Kuteleza na kuanguka, na hata kuchubuka ni alama za mafunzo ya maisha. Wengine bado tunatembea na makovu ya utotoni; ama ulianguka kwenye jiwe, ulijikwaa mahali, au ulichezea wembe. Mdogo wangu anajereha la toka akiwa na miaka kama mitano hivi baada ya kujikata kwa wembe akikakata mrija wa jani la mpapai ili kutengeneza filimbi! Hakuugusa wembe tena!
Katika makala yangu HII HAPA nilionesha haja ya vijana "watatu au wanne" kuangaliwa upya na kupewa nafasi nikiamini kuwa watakuwa wamejifunza. Hata mtoto afanye kosa kubwa kiasi gani mara nyingi kama wazazi tunawapa nafasi ya kutengeneza tena. Ni pale mtoto anapofanya kosa lisilosameheka kwa wazazi kiasi cha wazazi kumpa laana; yaani kumkana kabisa. NI wazazi wachache sana wanafikia sehemu ya kumpa mtoto laana; na wakati mwingine hata huyu akirejea na kujuta hujikuta anasamehewa.
January kama ilivyokuwa kwa Nape na Mwigulu walijaribu kuinua mapembe yao kwenye zizi la fahali mmoja. Wakajikuta wameondolewa nafasi zao na kwa aibu kidogo. Kwa baadhi yetu tuliona kuwa ilikuwa ni nafasi ya vijana hawa kujiangalia na kujitafakari uongozi wanaoutaka. Na kweli karibu wote hawa vijana waliweza kutulia. Waliweza kuwa nje ya madaraka makubwa na kurudi nyuma. Japo wengine bado walikuwa wanahisiwa kuwa wanachokonoa chokonoa katika kuonesha kutokusalimu amri kwao.
Sasa, kurudishwa kwa Mwigulu Nchemba na kwa sasa January Makamba kunatufundisha kuwa Rais Samia ameonelea kutokuwatupa vijana hawa nyota wa CCM. Na labda kuwaita "vijana" tena siyo sahihi sana. Hawa wote wanakaribia miaka hamsini sasa kwa hiyo ni "watu wazima" na neno sahihi labda ni "watu wa makamo". Ujana hauwezi tena kuwa kisingizio wala sababu ya hawa kutokuwa na hekima katika uongozi au kufanya mambo yanayotakiwa kufanywa na vijana wa chini ya miaka 40! Naamini sasa wamejifunza kitu. Rais Samia inawezekana amewapa nafasi yao ya mwisho kuweza kujitengeneza na kuwa sauti na nguvu ya kisiasa Tanzania kuelekea uchaguzi wa 2030.
Kwa January hili lina maana moja kubwa; ni lazima amuunge mkono Rais wake kwa asilimia 100. Wizara ya Nishati ni Wizara ambayo January alikuwa anapenda sana kuiongoza. Ana mawazo mengi kuhusu sekta hii hasa kwa vile aliona mambo yote yaliyokuwemo toka enzi za Dowan na madudu yake. Lakini pia nina uhakika anakumbuka kilichomuondoa Ibrahim Msabaha linapokuja suala la mikataba ya Nishati. Uzuri ni kuwa January amepewa nafasi ya kuongoza Wizara ya Nishati ambayo hatimaye ilitenganishwa kutoka Wizara ya Madini (hili lilikuwa ni jaribu kubwa sana kwa Waziri yeyote yule). Kupewa Nishati kunamfanya awe na nafasi ya kuweza kushughulikia sekta ambayo marafiki zake na watu mbalimbali wanaweza kumsaidia sana katika masual aya sera. Mwisho wa siku ni jukumu lake kuhakikisha kuwa sekta hii inasimamia taifa kwani bila nishati ya uhakika, nafuu, na inayowafikia wananchi kwa uharaka Tanzania itakuwa bado ina ndoto. Kazi kubwa ni kuona Bwawa la Umeme la Nyerere linakamilika kwa wakati; kuhakikisha hatua za awali na za kudumu za kusambaza umeme zinafanyika nchi nzima lakini pia kuhakikisha kuwa gharama ya umeme na upatikanaji wa vyanzo mbadala (alternative/renewable energy source) zinapatikana, ni rahisi na vyenye kuchochea uwekezaji wa ndani vinapatikana.
Ninanua kuna watu ambao kwa vile wanawafahamu vijana hawa kwa karibu na hususan January Makamba (rejea mada zilizorejeshwa JamiiForums baada ya uteuzi wake tena). Kuna watu ambao hawakufurahia wala kuona umuhimu wa Makamba kurudi tena kwenye nafasi kubwa kama hii. Binafsi, licha ya kuyajua yote yanayotajwa, madhaifu na Archille's heel yake naamini sasa hivi siyo tu anaweza kutulia lakini akawa na hekima ya kutenganisha siasa na harakati za kisiasa na kuzama katika kutumikia taifa, kuinua sekta aliyodhaminiwa kwayo na zaidi ya yote kutokusababisha serikali kuingia matatani ama kwa mikataba mingine mibovu ya nishati, au katika kudhoofisha juhudi za kujitegemea katika nishati na kufanya upatikanaji wa nishati ya uhakika uwe utakaosababisha Dowans na Richmon 2.0.
Binafsi, nampa nafasi na nitamhukumu kwa utendaji wake katika wizara hii nyeti licha ya kutambua matatizo yake ya huko nyuma. Ninaamini yeye na vijana wengine kwenye serikali hii (kama bado namuweka kundi la vijana) wana nafasi ya kuonesha kwanini Rais Samia amewapa nafasi hiyo tena; siyo kwa sababu ya kuwabeba (tukumbuke January alikuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kabla ya kuondolewa na Magufuli). Tunataka tuamini kuwa Rais Samia anaamini katika uwezo wake wa kiuongozi na siyo kumbeba kama mama (political matronage).
Tumpe Nafasi January Makamba, na tumuunge mkono bila kusita kumkosoa inapostahili kwani nyota yake bado inang'aa haijafifia na ni jukumu lake kuhakikisha kuwa inaendelea kung'ara.
MM Mwanakijiji.
New Nguvumali, Tanga.