Hoja pekee ambayo ninakubaliana nao wale wanaopinga sensa ni kuwa sensa ilipaswa kuuliza sifa zote za msingi za kijamii ili kuweza kupata takwimu sahihi za watu waishio Tanzania. Lengo kubwa la sensa ni kutoa picha sahihi ya jamii yetu ilivyo na imeundwa vipi. Hivyo, maswali yanayohusu kabila, dini, rangi na hata tofauzi za chini ya hapo (madhehebu, kuchanganya kabila au rangi, n.k) yalipaswa kuwepo kama sehemu ya dodoso za sensa. Tofauti yangu kubwa hata hivyo kwenye hili ni kuwa maswali ya aina hiyo yalipaswa kuwa ya uchaguzi wa mtu kujibu (OPTIONAL) bila kumlazimisha. Hivyo, Watanzania ambao wamekuwa wakitaka swali la dini liwepo kwenye maswali ya sensa wana hoja inayoishia hapo tu lakini hawana hoja ya kulazimisha watu kujibu.
Kwa mfano, swali la dini kwenye sensa ya Marekani ni 'optional' kama ilivyo kwa maswali mengine kadhaa ya kidemographia. Sheria ya Marekani inakata Idara ya Sensa kuuliza swali la dini huku ikilazimisha mtu kujibu. Hivyo, hata kwetu swali hili lingeweza kabisa kuwekwa na mtu anayetaka kujibu anajibu na asiyetaka hajibu. Kutokana na kanuni hiyo kama nilivyoandika karibu miezi miwili iliyopita mahali pengine kimsingi hakuna hoja ya serikali ya kutetea kukataa kuuliza swali hili. Hii ni kweli hata kwenye maswali ya kabila, rangi au madhehebu. Mtu - kwa mfano - angeweza kuulizwa "je unajitambulisha kama mfuasi wa dini gani?" na akapewa uchaguzi wa "Uislamu", "Ukristu", "Uhindu" na "Za Jadi", "Nyinginezo" na "Hakuna" lakini swali zima likiwa ni la uchaguzi. Mtu akijibu kwa mfano na kusema ni "Mkristu" bado anakuwa na uchaguzi wa kujibu kama ni wa dhehebu gani "Pentekoste", "Kilutheri", "Romani Katoliki" au "SDA" na bado akawa huru kujibu swali hilo zaidi au kuishia tu kwenye kujitambulisha dini yake.
Sasa, hili lingewezekana kabisa na naamini lingeweza kufanywa bila ya kuonesha aina yoyote ya upendeleo au kubania watu. Hata hivyo, serikali yetu ambayo ina tatizo kubwa la hekima iliamua kuondoa kabisa uwezekano wa swali hili kwa sababu moja kubwa tu: Inaogopa matokeo ya majibu ya swali hilo. Tuchukulia mfano ambao unatokana na hoja nzima ya kundi la Waislamu wanaotaka kususia sensa.
Fikiria kuwa matokeo ya sensa ambapo maswali yangekuwa si ya kulazimisha kujibu (mandatory) na ikaja kuonesha kuwa waliojibu sensa nzima Waislamu wanaonekana ni wengi je ina maana kuwa Waislamu ni wengi zaidi Tanzania kuliko Wakristu au ni kuwa tu wengi waliojibu swali hilo ni Waislamu? Je ingekuwa vipi kama ingekuwa kinyume chake? Lakini zaidi ni kuwa kwenye kundi ambalo linaamini kuwa kuna mfumo Kristu ambao unakandamiza Waislamu nchini je kuna uwezekano wowote wa sensa kuonesha matokeo ambayo hayaoneshi Waislamu wakiwa wengi? Jawabu ni kuwa tayari wapo viongozi na wanaharakati wa makundi ya Kiislamu ambao wameshawaaminisha wafuasi wao kuwa Waislamu ni wengi nchini na hivyo matokeo ya sensa ambayo yangeonesha kuwa ni kinyume na hili (kwamba wako wachache) yangepokewa kwa hisia ya kuonewa, kudhulumiwa na madai yale yale ya kutamalaki kwa kile kinachoitwa "mfumo Kristo".
Ni kutokana na hili basi swali la dini limekuwa gumu kuwekwa katika sensa ya sasa ya watu na makazi kwa sababu hakuna namna rahisi ya kuweza kuliweka bila kuwa tayari na matokeo yake. Ni hili basi naamini (sina sababu ya kuamini vinginevyo) serikali iliamua kama ilivyoamua huko nyuma kutokuuliza swali hili la dini au kabila au la tofauti nyingine za kidemographia. Binafsi ninaamini ni uamuzi wa kiwoga, wenye makosa na ambao unaonesha udhaifu wa walio madarakani kutowaamini Watanzania kuwa hakuna matokeo yoyote ya sensa ambayo yangeweza kubadili mahusiano yaliyopo sasa kama propaganda za sasa zote hazikuweza kufanya hivyo.
Sasa, uamuzi wa viongozi wa vikundi hivi vya Kiislamu kudai kuwa wanasusia sensa kwa sababu ati serikali imekataa kuwekwa swali la dini kwenye sensa ni uamuzi wa kibinafsi, wa kujipendelea na kujinyanyua dhidi ya Watanzania wengine. Sababu kubwa ni kwamba katika taifa letu jamii inayodhulumiwa zaidi na mfumo wa kifisadi ambao umetamalaki nchini kwa miaka thelathini sasa SIYO WAISLAMU. Naomba kurudia kauli hiyo ili isije ikapita hivi hivi: katika taifa letu jamii inayodhulumiwa zaidi na mfumo wa kifisadi ambao umetamalaki nchini kwa miaka thelathini sasa SIYO WAISLAMU.
Watu pekee ambao nina uhakika wana haki ya kulalamika na hata kususia sensa hii siyo Waislamu wala Wakristu; siyo Wahindu wala Waarabu! Bali ni watu wa jamii za jadi ambao wametupwa pembezoni mwa mafanikio ya taifa letu, wakiwa ni raia wa daraja la nne (nje ya treni) kwenye taifa lao. Watu ambao maisha yao yamekuwa ni ya kusahauliwa na kutendewa kama wageni. Makabila mawili yanakuja kwa haraka - kwanza ni Wahadzabe na wenzao Watindiga, na Wamang'ati. Makabila haya yana haki ya kutaka kujua idadi yao, wana haki ya kutaka kujua wamefikiwa na maendeleo ya karne ya 21 kwa kiasi gani kulinganisha na makabila mengine. Ikumbukwe kuwa Mchagga Muislamu na Mkristu Muislamu kwa kiasi kikubwa wako katika mafanikio zaidi na nafasi zaidi kufanikiwa kuliko Mtindiga au Mhadzabe Muislamu au Mkristu. Hawa ndio watu ambao kweli wako kwenye pembezoni ya kona za mafanikio ya taifa.
Kwa kundi la Waislamu hawa kuamua kususia sensa kana kwamba wanaonewa sana kuliko jamii nyingine yoyote au hata kuonesha kuwa wanaonewa ni absurd. Ninaamini wangeweza kabisa kudai swali hili na kutumia njia za kawaida ili siku moja liweze kuingizwa kwani lina maslahi makubwa zaidi. Lakini kuamua kususia ati kwa vile hawajasikilizwa ni kujiona kupita kiasi. Na hili ni kweli kwa sababu wanachotaka kujua ni suala la "dini" tu lakini siyo kabila, rangi, madhehebu. Kwanini wanagomea sensa kwa sababu ya kutohusisha dini tu? Yawezekana ni kwa sababu wao HAWAJALI hali za jamii nyingine ambazo nazo zingependa kunufaika na takwimu za sensa.
Ndio maana kwenye hoja yangu ya awali miezi ile miwili iliyopita nilisema kuwa swali la demographia mambo ya dini, kabila, rangi na hata dhehebu nilisema kuwa kujua idadi na mambo mengine yanayohusiana na haya ni muhimu kwa kuweza kupanga maendeleo - ambalo ndilo lengo la sensa. Kujua jamii gani na kwa kiasi gani iko nyuma kwa kuangaliwa takwimu zilizokusanywa kwa sensa kunasaidia taifa.
Kwa vile zoezi hili lengo lake ni kujua hasa 'idadi' ya Watanzania na wakazi wa Tanzania vitambulisho vingine vyao vyovyote siyo vya muhimu kuliko hilo la idadi. Binafsi naamini baada ya serikali kuboronga suala la sensa ipo haja ya kufikiria sensa maalum ya demographia ya wananchi wetu. Ninaamini ili kufanikisha sensa hii ya idadi watawala wetu watoe ofa ya kuamua kufanya sensa ya demographia (kabila, dini, na rangi(race)) Hata hivyo sensa hiyo maalum inapaswa kuwa optional kwa Watanzania watakaotaka kushiriki na isiwe ya lazima. Nje ya hapo serikali itoe ahadi kuwa sensa ijayo (miaka kumi toka sasa) itakuwa ni sensa ya demographia vile vile.
Kususia sensa ya idadi na ambayo miaka yote imekuwa ni ya idadi ni kukosa busara, ni kuonesha kutokujali mahitaji ya wengine lakini zaidi ni kutaka kujipendelea na kujitukuza juu ya wengine. Lakini zaidi ni kuwa wale ambao leo wanahamasisha kususia sensa hii baadhi yao ndio hao hao waliosimama kuipigia debe ilirudi madarakani mwaka 2010. Yaani wale wale ambao waliwacheka wengine walipoona magugu wao waliendelea kulia 'panda mbegu panda mbegu!' Sasa leo yanaota wanaruka na kutaka kukana.
Binafsi ninaamini watakuwa na hoja ya kususia sensa kama kwanza watakuwa tayari kususia na kutaka wananchi wakisusie chama kilichounda serikali hiyo. Kwa sababu uamuzi wa kukataa kuweka maswali ya demographia ni wa kisiasa na umetolewa na viongozi wa kisiasa. Ni uamuzi wa CCM. Badala ya kususia sensa waisusie CCM na wataonesha mfano kweli wa kuchukuizwa kama wataanza kurudisha kadi za CCM. Endapo watafanya hivyo wawe tayari kuunga mkono chama ambacho kitakuja na sera ya kuhakikisha sensa ijayo ya taifa itakuwa ni ya kidemographia.
Nje ya hapo, kususia sensa hakuna tena.
MMM