"....Mwisho wa mivutano Muingereza alikataa kuisaidiya serikali ya Zanzibar
ilipopinduliwa tarehe 12 Januari 1964 na sababu kubwa iliyowafanya kukataa ni
imani yao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni suala la ndani ya Zanzibar na
kuwa hakukuwa na mkono au uvamizi kutoka nje ya Zanzibar.
Kwa upande wa Tanganyika Muingereza aliamuwa kuzuwiya fujo na kumrejesha
kitini Mwalimu Nyerere pale jeshi la Tanganyika lilipoasi tarehe 20 Januari 1964 na
Nyerere akakimbilia mafichoni siku tisa tu baada ya mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi wa Serikali ya Tanganyika haraka walikwenda kuomba msaada kutoka
kwa wakubwa wa Kiingereza.
Anaelezeya Brigadier Douglas:
Kambona, akifuatana na [Paul] Bomani, Waziri wa Fedha, akionekana ana
jambo ameficha, na ana khofu zaidi kuliko kabla, walikuja nyumbani kwangu na barua
kutoka kwa Naibu Raisi Kawawa ilosema: Nimeelekezwa na Raisi wa Jamhuri ya
Tanganyika kuiletea ombi la msaada wa kijeshi serikali ya Kiingereza ili
utuwezeshe kuweka sheria na amani ndani ya nchi.
Mara nyingi uasi wa jeshi la Tanganyika umekuwa ukihusishwa na mapinduzi
ya Zanzibar kwa kuwa wanajeshi wa Tanganyika, Kenya na Uganda waliingiwa moyo wa
kuasi kutokana na kufaulu kwa Mapinduzi ya Zanzibar ingawa hakukuwa na uhusiano
wowote baina ya matukio hayo mawili.
Uamuzi huu unatokana na kukosekana
kuyafahamu Mapinduzi ya Zanzibar kwanza, na pili, kukosekana huko
kufahamika kwa mapinduzi ya Zanzibar kumeondowa hoja ya kufanywa
utafiti wa mahusiano baina ya mapinduzi na uasi wa kijeshi wa Tanganyika.
Suala moja muhimu ambalo linavutiya hoja ya uhusiano baina ya mapinduzi
ya Zanzibar na uasi wa kijeshi wa Afrika Mashariki ni suala la kukamatwa kwa
viongozi wa vyama vya wafanyakazi baada ya kutokeya uasi huo Tanganyika.
Tarehe 29 Januari 1964 Balozi wa Kiingereza kwa niaba, alipeleka ujumbe wa
telegram kwa Commonwealth Relations Office, London, uliopitiya Ubalozi wa
Kiingereza Kampala, Nairobi, Aden na Washington:
Matokeo ya kuasi kwa jeshi la Tanganyika ni kundi kubwa la viongozi wa vyama
vya wafanyakazi kukamatwa Jumapili usiku Tanganyika nzima pamoja na
takriban viongozi wote wa chama cha Shirikisho la Wafanyakazi wa Tanganyika
(Tanganyika Federation of Labour).
Wote walipelekwa kwenye vituo vya polisi
kwa kuhojiwa na baadhi yao baadaye waliwachiwa huru.
Rais [Nyerere] kwenye hotuba yake ya redio ya jana usiku aliligusiya suala
hili na aliongeza kwa kusema kuwa Mkuu wa Wilaya mmoja pia amekamatwa.
Nyerere alitamka kwenye hotuba hiyo ya redio kuwa watu hawa, wa vyama
vya wafanyakazi, walikuwa wamekula njama na viongozi wa uasi wa kijeshi
"kusababisha mtafuruku zaidi."
Kulikuwa na uvumi mwingi wiki iliyopita kuwa vyama vya wafanyakazi
vilikuwa vinapanga mgomo wa jumla au angalau
mgomo wa wafanyakazi wa gatini na wa reli.
Pia inaaminiwa kuwa viongozi kadhaa wa vyama vya wafanyakazi
walikuwa wakipitisha wakati wao mwingi
kwenye kambi ya kijeshi ya Colito."
Hayo ni sehemu ndogo tu ya Kitabu cha Gwiji wa Historia
Dr. Harith Ghassany, cha 'Kwa heri ukoloni, Kwaheri Uhuru'