Jasusi Honda ndani ya mpango wa Congo

Jasusi Honda ndani ya mpango wa Congo

RIWAYA: MPANGO WA CONGO

SEHEMU YA 14



Zilipita dakika kadhaa ndipo alipohisi kuna hali ya tofauti kutoka pale alipokuwa amelala.

Mwili hakuwa na nguvu lakini alisikia joto jingi huku akianza kupaliwa na alipofumbua macho akakutana na wingu la moshi mzito.

Nyumba ilikuwa inaungua!!.

Akajaribu kuinuka ila hakuwa na nguvu,akajaribu tena akashindwa.

Akakata tamaa na tayari alisikia mmomonyoko wa mabati kutokea huko vyumbani.

Kifo kilinusa pua za Solomoni Bukaba.

****

“Yule boya kakuotea leo aisee” alisema bwana mmoja mrefu aliekuwa anaendesha gari kwa kasi kutoka lango lango huku akipishana na magari na baadhi ya raia waliokuwa wameanza kujazana barabarani kushangaa moto mkubwa uliokumba baadhi ya nyumba zilizokuwa zimepakana na nyumba ya Solomoni Bukaba.

“Ndio mana kitengo kina Helper hasa killer akishindwa” alisema binti.

“Wapi sasa” aliuliza yule bwana.

“Club D nishushe pumzi” alijibu binti huku akiegemea kwenye kiti.


“mmh nadhani urudi nyumbani uoge” alishauri bwana dereva.

“ Haina shaka”

Gari ilichochewa moto.

****

..NCHINI CONGO..

Honda alihakikisha maelezo aliopewa na mateka wake yamemkaa sawia na hakutaka kuendelea kuhoji zaidi kwa wakati huo mana hakutaka kupoteza muda zaidi kwa kuwa alijua hapo ndipo ukomo wa ukweli kutoka kwa yule mateka na zaidi ya hapo ni kwa jasho na damu ndo ukweli atapata au kukosa kabisa.

Hakutaka kucheza bahati na sibu na muda.

Lazima amtafute X ambae kwa mujibu wa marehemu Bulembo ni Mtanzania na pia ni Club lakini kwa maelezo ya mateka; ndie aliewatuma wamkamate.

Akabaki na maswali kadhaa hivi.
Je X inahusu watu wangapi ama inahusu mtu mmoja?

Hakuwa na jibu.

Akajizoa zoa kutoka pale alipokuwa kisha akamsogelea mateka wake

“Kwanini mnamuita X?” aliuliza Honda Makubi.

Mateka akatoa cheko la kebehi kisha akajibu;
“Kwa sababu hafahamiki na hajulikani hata kwa sura!!”

“Duh!!” akaguna Honda kisha akaendelea kumsikiliza mateka wake.

“Kwa hiyo uliniona mjinga kukwambia tumetumwa na Mr X? au ulidhani ningemfahamu ninge….” Mateka hakumaliza kauli yake akajikuta anaelea hewani huku akishindwa kujitetea sababu ya kufungwa kamba ngumu kwenye kiti.

Mateka hakuwa na namna akasambaratika chini kama zigo la maharage mabichi.

Honda alijua kuna sababu za kuambiwa bila kukurukakara mwanzo na sababu aliipata na hakuwa tayari kuendelea kudhihakiwa hivyo akamtandika teke kali yule mateka lililomwacha akiwa hana msaada huko alikoangukia.

Honda akamwinua kisha akamshika kosi wa shati lake na kumvutia kwake wakawa wakitazamana kwa karibu.

“Nikirudi utanieleza aba,cha,da zote unazozijua Kimburu wewe” alichimba mkwara Honda kisha akamwachia na kukusanya vilivyo vyake na muhimu akavitia kwenye kwenye mkoba na kuuvaa kisha akatoka na kufunga milango yote vizuri na kuruka ukuta na kutokomea kuwahi pahali.

****

Kiza kilipoanza kuingia, Honda alikuwa nje ya ubalozi wa Tanzania nchini Congo.

Alikuwa amevaa kofia ya pama na suti matata iliomkaa vyema mwilini na kubadilisha mwonekano wake kwa kiasi kikubwa.

Wakati huu alivaa suti kwa sababu kwa waliomzoea kamwe hawakuwahi kumuona akiwa amevaa suti.

Mkononi alishika mkoba mweusi ambao alijua kabisa una uhumimu mkubwa licha ya kuhifadhi vitu asivyovifahamu maana yake.

Tayari wafanyakazi wengi walikuwa wameanza kurudi makwao.
Muda bado ulikuwa unaruhusu kwa watu wenye dharura kuingia na kutoka pale ubalozini kwa wakati huo.

Alijichanganya na watu hatimae alifanikiwa kuingia hadi mapokezi na bahati bado ilikuwa upande wake,mapokezi kulikuwa na watu kadhaa huku sehemu ya kupumzika kukiwa na watu wengine waliokuwa wakingoja huduma.

Akatumia nafasi ile kwa wafanyakazi kuwa bize akapita na kupanda juu kuelekea kwenye ofisi za Mkurugezni wa uhamiaji Papi Mndewa.

Alipofika karibu na mlango wa ofisi za Mkurugezi; Honda akasita kwenda zaidi akarudi nyuma kidogo akaangalia kushoto na kulia, hakuona mtu.

Kumbukumbu ya picha alioiona mezani kwa mhudumu wa mgahawa wa Tunde ikajijenga tena kichwani kwake.

Na hapo akajaribu kutazama tena ni wapi alipopigwa picha na mpigaji alipiga kwa kulenga kona akitokea upande gani!!

Hatimae macho yake yakatua kwenye kona iliotenganisha ofisi ya Balozi na chumba cha mawasiliano.

Konani pale kulikuwa kuna kamera ndogo mbili za usalama.

Macho yake akayahamishia tena kwenye kona iliotumika kutenganisha ofisi ya balozi na Mkurugenzi.

Tofauti na kona ya mwanzo yenye kamera mbili zilizofungwa pamoja, kona hii ilikuwa na kamera moja tu ambayo hata yeye alijua ilikuwepo na kona nyingine pia ilikuwa na kamera moja na ndivyo ilitakiwa iwe kila siku.

Alah!!!

Kamera ya pili ilitoka wapi na kwanini ilikuwa pale na ilikuwa na faida gani!!

Makubwa jama!!

Honda aliweka kituo kichwani kwake kumaanisha amefikia mwisho wa kufikiri wakati huo.

Wakati akitaka kufungua mlango wa mkurugenzi,mlango ukafunguliwa haraka akarudi nyuma.

Macho yao yakagongana.

Alikuwa ni mkurugenzi ambae alikuwa anataka kutoka kwenda kwake.

“Honda!!” aliita kwa kushangaa Mkurugenzi.

Honda akamwonyesha ishara warudi ofisini.

“Aisee nilijua nimeshakupoteza komredi” ndilo aliloweza kusema Mkurugenzi huku akimtizama Honda kama asieamini uwepo wake pale.

“Sio kunipoteza tu, hata uhai ningeupoteza na usingeniona kabisa” alisema Honda huku akikaa juu ya meza na kubaki wakitazamana kwa sekunde kadhaa.

“Nilijua wale jamaa watakuwa si watu wazuri japo kuwaingilia kiharaka vile kungeleta mkanganyiko wa kidiplomasia!!” alisema kwa masikitiko Mkurugenzi Papi Mndewa huku akitupa gazeti mezani pale alipokuwa amekaa Honda.

Honda alilitizama gazeti lile kisha akatabasamu.

“Kwani limeshatoka?” akauliza Honda bila kujishugulisha kulichukua mana ukurasa wa mbele ulikuwa umepambwa picha yake.

Picha ile haikumstua mana alishaiona tangu akiwa Tunde.

“Kwani linatoka lini hili gazeti mbona limesambaa sana!!” akauliza Honda.

“Nimeletewa na mtu wetu alieko huko linakopikwa na linatoka kesho.” Alijibu Papi.

“Kwani ilikuwaje!!” aliuliza Papi.

“Ni hadithi ndefu kidogo komredi ila kifupi tunazungukwa na watu wenye akili na ujuzi pia lakini ni lazima tupambane, na mchawi wetu wa kwanza anaanzia hapa hapa,unaionaje hiyo picha hapo?” alimalizia kwa swali Honda.

“ulipigwa wakati ukiingia hapa ofisni. Nimefikiria sana kuhusu mtu aliepiga picha hii na..!” Papi hakumalizia kauli yake alikatishwa na Honda.

“Picha haijapigwa na kamera ya mtu ila imepigwa kamera ilioko humu, lakini swali la kujiuliza, imewekwa lini na nani alieiweka?” akauliza Honda na kuacha swali lile likiambaa kichwani mwa Papi Mndewa.

Ukapita ukimya kidogo!

“Hii hatari sasa!!” alisema Papi huku dhahiri akionekana kuzama kwenye tafakuri!!

“Komredi mmefikia wapi na nyie!” alisema Honda.

“kiukweli tumeshindwa kujua kilichosababisha mawasiliano kukatika wakati balozi aliposhambuliwa. Tumejaribu kupitia kamera na miundo yote ya usalama ili kuona ni wapi hujuma ilianzia,lakini kote kulikuwa shwari aisee na nimeagiza baada ya kumsafirisha Balozi basi tuanze uchunguzi upya mana kuna ukakasi pahali” alimaliza kueleza Papi.

Honda akazishusha pumzi kwa mkupuo.

“Hali ni tete, lakini hili sakata litaisha, ikishindikana basi tutaomba makao makuu watuongezee nguvu” alisema Honda.

“Japo naamini hujashindwa lakini ikifikia huko tutakuwa hatuna namna!” alisema Papi.

“mmh wale vijana wa kitengo cha usalama wapo wangapi vile!!” alihoji Honda huku dhahiri akionekana kuwa na hisia za kumbukumbu.

“wapo watatu Komredi!!” alijibu Papi.

“Basi jicho lako lianzie hapo Komredi” Honda alimwambia Mkurugenzi wake!

Papi akatikisa kichwa bila kutoa sauti na hilo lilimaanisha tayari uchunguzi dhidi yao umeanza.

“Ok naomba unifikishe ofisini kwa Balozi kuna kitu nahitaji kutazama.” Alipokwisha kusema hivyo tayari miguu yao ilianza kufanya harakati za kuondoka ndani ya kile chumba.

Dakika moja badae wote walikuwa wanatazama tundu la risasi lilokuwa limejenga nyufa kadhaa kwenye kioo.

“Mdunguaji!!” alijisemea Honda huku taratibu akisogea lilipokuwa dirisha.

“ina maana hili pazia lingekuwa limerudishiwa basi mdunguaji angekosa shabaha” alisema tena taratibu Honda huku akishika tundu la risasi ilipopita.

Moja ya sifa kubwa ya kubwa ya Honda ni kutambua ukubwa wa vipenyo vya risasi na aina za silaha.

Hata hapo alijua.

“Hii ni Lapua Magnum bila Shaka” alisema Honda huku akimgeukia papi.

“Yes!! Kitengo kimethibitisha aina hiyo ya risasi na silaha ilikotoka.” Papi alijibu swali la kijana wake.

“Lakini kwa nilivyoona siku ile kabla sijakamatwa hili pazia lilikuwa limerudishiwa makusudi kabisa na nadhani wewe ungechunguza pia aliefanya usafi siku hiyo Mkuu au!” Honda alitoa mawazo yake kwa mtindo wa kuhoji.

“Hilo pia litafanyiwa kazi na sikuwa nimeliwaza kabisa komredi” alisema Papi huku akigonga tano kuashiria amekubali mawazo ya kijana wake ambae tangu wajuane walifanya kazi kwa ukaribu kiasi wakajikuta ni kama wanalingana wadhifa.

“Kile chumba pale ghorofani kinaweza kunifikisha kwa muuaji wa Balozi” alisema Honda huku akinyooshea kidole upande wa pili kulikokuwa na ghorofa kubwa na ndefu.

Ukimya ukapita.

Naendela na majukumu komredi ila usiponiona siku tatu pale ndani kwa Bulembo kuna kipanya nimekihifadhi pale kakichukue kinaweza kukufikisha nilipoishia” alisema Honda huku akianza kutoka pale ofisini.

Kitu kimoja ambacho watu hawa hawakujua ni kuwa kulikuwa na mtu mwingine aliewasikia walichokua wanazungumza.

Lakini kwao ni kama kiza hakuna walichojua.

****

Sajini Kebu alikuwa ametulia kimya huku akiwaza namna alivyonusurika kusombwa na maji yaliokuwa yanapita chini ya daraja alilitupiwamo na Honda.

Kimoyomoyo alihusudu uwezo wa akili wa mtanzania yule.

Sajini kebu akageuza macho yake kushoto kwake akakutana na jicho la Kojo ambae waliunganishwa pamoja baada ya vijana wa Kebu kuadhibiwa na Honda; hivyo sasa alikuwa ameungana na kundi la Kizibo na Kojo.

Aliona jinsi uso wa Kojo ulivyopasuka bila mpangilio.

“Umesema hii kazi ya yule bwege sio!!” aliuliza Sajini Kebu.

Swali lile lilionekana kumkera Kojo ila hakujibu akabaki kutazama pembeni.

“Bwana yule ananitesea rafiki yangu aisee” alidakia Kizibo aliekuwa amekaa kwenye kiti cha dereva.

“Hebu nipelekeni nikapumzike kwa mrembo wangu nikitoka huko risasi za kichwa zitammaliza Honda!!” alisema Sajini Kebu huku akiegemea kiti cha abiria alichokuwa amekalia.

Gari ikawashwa na kuondoka kuelekea viunga vya mji wa Gombe pembeni kidogo ya mji wa Kinshasa.

Ni kwa kuwa hawakujua lijalo halijawahi kujulikana kamwe.

Na kama walidhani wanaenda kupumzika walikosea sana

*****

Shusha komenti yako tafadhali, usipite kimya

Nitaanzia hapa baadae.
Samahani kwa kutotoa mrejesho, lakini nikitulia nitakuja kuelezea mtazamo wangu.


Sent from my iPhone using JamiiForums
 
RIWAYA: MPANGO WA CONGO

SEHEMU YA 13

NA BAHATI MWAMBA.

SIMU: 0758573660


Hakujuwa kesho anaijua mungu pekee na hakuna binadamu aliewahi kuifikia kesho isipokuwa mauti pekee ndio hukufikisha katika ukomo wa kesho ila si mwanadamu aliehai mana kila siku ni kesho ijayo.


Hakujua! Hakujua!

******

2. FUMBO.

Askari wa usalama barabarani bwana Kambi kitime alihakikisha anajua ni nani hasa amewasiliana na Remi pale kituoni na ni kitu gani hasa kilichompeleka pale kituoni.

Upande wake wala haikuwa kazi hasa baada ya kuona kijana mmoja ‘IO' akiharakisha kuingia ofisi namba kumi.

Kwa uzoefu wake wa ushushu usio rasmi ambao hautambuliwi na ofisi za usalama,alijua kuna mwito maalumu wa kijana yule hasa baada ya kuhakikisha Remi ametoka ofisi namba kumi inayokaliwa na OCCID Shaban katwila.

Alimkariri ‘IO’ yule kisha akatoka ndani ya ofisi na kuaga kwa baadhi ya rafiki zake.

Alipohakikisha yupo mbali na viunga vya kituo cha polisi; akachukua simu yake kisha akalitafuta jina alilohifadhi kwa herufi kubwa.

‘Elchapo' alipohakikisha ndilo jina alilohitaji, akapiga.

Punde simu ikapokelewa upande wa pili.

“Sema kitime” iliunguruma sauti iliopokea.

“Kasuku alikuwa hapa kituoni dakika sita zilizoisha” alisema Afande Kambi Kitime.

Upande wa pili kwa mtu alietambulika kama Elchapo ulikaa kimya kwa sekunde kadhaa.

“Unahakika umemuona yule binti?” akauliza Elchapo.

“Aah!!, sasa nitashindwaje kumjua wakati picha ya Kasuku ninayo?” alihoji Afande Kitime huku akionesha dhahiri kuchukia.

“Aisee hii inaweza kutugharimu poti!” alisema Elchapo huku akisikika dhahiri kuwa juu ya uwezo wake wa kupumua.

“Umepata tetesi za alichokifuata?” Elchapo aliuliza kwa utulivu wa kutisha na hiyo ilimaanisha yupo kwenye kiwango cha mbali sana cha tafakuri.

“Aliingia ofisi namba kumi, na ameacha karatasi kadhaa na sijui kilichomo” alieleza Afande Kitime.

Elchapo akapumua kisha akasema; “Naomba unipe uwezo wa mtu aliekabidhiwa hiyo kesi”

“Solomoni Bukaba, ni intelligence ofisa na ni mjuzi si haba” alifafanua Kambi Kitime.


“Ok nadhani ataponzwa na hizo karatasi” alisema taratibu sana Elchapo.

Ukimya ulipita baina yao.

Sekunde kadhaa mbele Elchapo akavunja ukimya ule.

“Ahsante poti, kazi yako imeisha nenda benki saivi mzigo wako umeshasoma” akamaliza Elchapo kisha akakata simu.

Afande mnoko; Kambi kitime alifurahi kwa kazi yake nyepesi inayomuingizia mkwanja wa kutakata.

Malipo ya usaliti hakujua ni kifo na hilo hakujua afande huyu mnoko ambae rushwa ya barabarani kwa madereva aliona haiwezi kukidhi matakwa yake pengine aliona ni pesa ya kusafisha viatu tu kama alivyosema mheshimiwa mmoja nchini.

Hakujua usaliti wa damu hulipwa kwa damu.

*****

Solomini Bukaba ndie ofisa wa kitengo cha upelelezi ya makosa ya jinai na uhaini ndani ya Nchi na ndie aliepewa karatasi nne zilizotoka kwa Remi.

Kwa maelezo ya mwanzo aliopewa ni kuwa kesi hiyo inahusiana na upotevu wa watoto wawili na karatasi alizopewa ni ushahidi kwa mujibu wa Remi.

Solomoni Bukaba alikuwa na kiporo cha mkasa mwingine wa mauaji ya watu sita huko visiwa vya Mwabhurugu simiyu na yeye alipewa jukumu hilo kwa kuwa ilisadikika wauaji wamekimbilia jijini Mwanza.

Solomoni alikuwa anakamilisha ripoti ya uchunguzi wake kabla ya kuripoti kwa mkuu wake wa kazi hivyo kazi aliopewa na OCCID Shaban Katwila ilikuwa ni nyongeza ya mrundikano wa kazi kwake hivyo aliamua kuzisoma karatasi hizo akiwa nyumbani kwake usiku mnene.

Kiza kilipoingia tayari Solomoni alikuwa ameshakamilisha ripoti yake na akaihifadhi vizuri kwenye makablasha kisha akaihifadhi ndani ya droo ya moja ya makabati yaliokuwa ofisini kwake.

Alipomaliza akapiga mwayo mrefu kisha akajinyoosha ili kuondoa uchovu uliokuwa umeanza kumvaa.

Hakutaka kuendelea kukaa ndani ya ofisi zile, akatoka na kuchukua koti lake akavaa na kuliendea gari lake lililokuwa limepaki likiwa pweke baada ya magari mengine yaliokuwa pamoja nalo kuchukuliwa na wamikiki wake.

Aliweka kablasha lililokuwa limehifadhi nakala za karatasi za Remi kwenye kiti cha nyuma kisha akaingia ndani ya gari lake na kulitekenya.

Lilipostuka tayari alikuwa ameshaingiza gia na kuondoka kwenye viunga vya ofisi za kipolisi.

Mwendo wake haukuwa wa kasi, alikuwa anaendesha taratibu huku akisikiliza muziki safi kutoka kwa wazee wa kale Kilimanjaro Band wananjenje.

Ingelikuwa ni siku ambazo huwa yupo kwenye hekaheka za kukimbizana na wahalifu basi angekuwa makini sana na vioo vyake vya gari kuangalia mienendo ya gari zilizokuwa nyuma yake.

Labda kwa siku hiyo kwake ilikuwa kifo cha nyani miti yote huteleza au basi wimbi la kupoteza lilikuwa linamwandama.

Hakuweza kabisa kuiona gari ndogo nyeusi iliokuwa nyuma yake tangu atoke kituo cha Polisi Neshino.

Safari yake ilikoma mbele ya geti la kijani pembezoni kidogo ya soko la nguo Langolango.

Alishuka ndani ya gari kisha akaenda kufungua geti na kurudi kuingiza gari lake.

Moja kwa moja aliposhuka ndani ya gari lake, akaenda kuingia ndani kwake ambapo palikuwa pweke kwa sababu hakuwa na mke wala mtoto alieweza kuishi nae.

Makablasha yake akayabwaga kwenye sofa kisha akaenda bafuni kuoga.

Huko hakudumu sana akarejea sebuleni akiwa amevaa nguo nyepesi maalumu kwa kulalia.

Alianza kwa kuyaweka sawa baadhi ya makablasha yake ambayo hakuwa na kazi nayo kwa wakati huo.

Mikono yake ikalifikia kablasha lililohifadhi nakala alizopewa na mkuu wake.

Akalifunua na macho yake yakatua kwenye maandishi ya kwanza kabisa ambayo yalimshawishi aendelee kusoma.

Lakini kila alivyozidi kusoma alijikuta mwili wake unasisimuka kwa alichokisoma..

Hatimae akatua karatasi ya kwanza na kuendelea na ya pili hatimae ya tatu na ya nne ndio ilimtoa jasho.

Kwanini!!

Kwa sababu katikati ya maelezo ya ile karatasi kulikuwa kuna majina mawili yaliokuwa yamekolezwa kwa wino.

Mbali na majina yale kulikuwa pia kuna akaunti mbili za kibenki katika mabenki mawili tofauti.

Solomoni Bukaba akaingiwa na ganzi ya mwili hakika.

Kichwani mwake yaliibuka maswali mawili huku swali kubwa likiwa ni vipi ataindika ripoti yake kwa sababu kwa maelezo ya karatasi zile haikuwa rahisi kuandika tena upotevu wa watoto kama mkuu wake alivyotaka iwe.

Lakini pia alihitaji kumpata binti aliezileta karatasi zile ili amuulize maswali kadhaa.

Angelimpata wapi hilo hakujua na wakati huo mshale wa saa ulisoma ni saa tano na nusu za usiku.

Alihitaji kupiga simu kutoa taarifa ile na si kulala nayo mana hakutaka kabisa kuipuuzia.

Akatoka sebuleni na kuelekea chumbani kuchukua simu yake.

Akiwa chumbani huko huko akapiga simu.

Mwanzo alidhani hana salio mana simu iligoma kutoka. Bila papara akajaribu kuangalia salio.

Lilikuwepo!

“mmh” akaguna

Akarudia tena kupiga simu,hali ikawa ile ile.

Simu haikutoka.

“Alah!!” alagafirika.

Akaichomoa kitesi chake kisha akarudisha.

Bado hali ilikuwa ni ile ile simu yake haikutoka.

Pagumu!!!

Akahisi labda ni mtandao unasuumbua, akatazama juu ya meza ndogo iliokuwa chumbani mwake.

Akaiona simu ya mezani ikiwepo.
Akaiendea na kuzungusha mara kadhaa ila ilitoa mlio kuashiria hakuna simu inayoweza kupigwa ama kupokelewa na simu ile.

“Kum….ae” likamtoka tusi zito lenye uzani wa kilo kadhaa.

Akajishika kiuono huku akishindwa la kuamua.

Akavuta pumzi nyingi na kuzishusha nusu tu.

Akasita kuzimaliza akavuta tena.

Ewaah!!

Alinusa harufu ya kitu kuungua,akaangaza pale chumbani hakuona kinachoungua.

Haraka akapiga hatua ndefu na kutoka ndani ya chumba huku akibamiza mlango kwa nguvu.

Akapigwa na butwaa kwa alichokiona sebuleni.

Kulikuwa kuna mgeni aliezichoma moto karatasi zile nne huku akiwa amejikaribisha kwenye sofa.

Mgeni yule alikuwa ameziba uso wake wote na kubakiza macho tu.

Kifupi alivaa kininja.

Aligwaya.

Solomoni Bukaba alitazama tena mlango wake, ulikuwa umefungwa lakini pia alikumbuka alifunga mlango wa nje kihakika.

Kapitaje na wapi!!

Hakukuwa na wa kumjibu.

“Wewe ni nani na umeingiaje?” aliuliza Solomoni huku akijitahidi kuupoteza mtetemeko uliokuwa umeanza kuomba makazi mwilini mwake.

“Acha kuwa mjinga Solo; yani hujaona karatasi zilizoungua unauliza nimeingiaje au hazijakuuma karatasi hizo?” alimaliza kwa swali mgeni yule.

Maajabu!!

Solomoni alihisi kuota hivi, sauti ya mgeni wake ilikuwa ya mwanamke.

Lakini kulikuwa kuna kitu cha ziada kwa mwanamke yule na kitu hicho kilijaribu kumuingia Solomoni ila hakikuingia sawa sawa mana hofu na akili vilishindana kuziteka hisia za mwili.

Solomoni Bukaba akatupia tena macho yake pale zilipokuwa karatasi alizopewa na OCCID; zilikuwa zinamalizikia kuteketea.

Akagashabika!!

“Ulishazichoma kwanini usiondoke sasa” aliuliza kwa utaratibu Solomoni.

Mgeni akatokwa na cheko la kishambenga.

Hapo napo Solomoni akakazia tafakuri yake ili aone kama ubongo utamletea kumbukumbu ya sauti hiyo.

Ikagoma!!

“Unadhani nitaondoka kirahisi tu!” aliuliza mgeni yule wa ajabu huku akinyanyuka kwenye sofa.

“Kwanini isiwe kirahisi binti” Solomoni nae akauliza huku akimtizama kwa makini mgeni yule.

“Haya macho mbona..” akajisemea Solomoni ila hakumaliza kuyatafakari binti yule akakwepesha macho yake ili asitazamane na Solo.

“Hakuna aliewahi kuzitazama hizo karatasi akabaki hai” alijibu Mgeni.

“Una….” Solomoni hakumalizia kauli yake akajikuta akipokea teke safi la kifuani lililomsambaratisha chini kama gunia la Panya huko Nyasa.

Solomoni akashangaa alivyopigwa kitaalamu.

Kutoka pale alipokuwa kwa chini kulikuwa kuna bastola ambayo ni vigumu kujua huwa inawekwa mahali hapo karibu na sofa aliloangukia.

Akataka kuikwapua…!

Lauhaulah! !!” akashangaa kisu kikita karibu na mkono uliokuwa ukienda kuinyofoa mafichoni bastola yake.

“ Alijuaje naeka hapa mpuuzi huyu!” alijiwazia Solomoni huku akijizoazoa kutoka chini.

“Mwanaume mzima unakimbilia silaha mbele ya mwanamke, shame on you lazy boy!!” alichamba mwanamke yule.

Solomoni akajaa gadhabu.

Kosa hilo!!

Kwa kujitutumua akanesa juu ili amtandike teke mgeni, ila akaambulia patupu na kabla hajatua chini akajikuta akipokea teke la pumbu.

Solomoni akabweka kama mbwa koko aliegonganisha mabwana.

Maumivu yakamtambaa kila kona ya mwili wake.

Ili aisendelee kuotewa akajiegemeza kwenye kabati la vyombo lililokuwa lipo pale sebuleni huku mkono wake mmoja ukiwa umezikumbatia kende zake na macho yake yakiwa makini kwa binti mgeni ambae alikuwa amechora mchoro kwa mtindo wa fujtsu.

Patamu!

Dakika mbili zikapita za ukimya huku kila mmoja akijaribu kumsoma mwenzie mawazo yake.

Binti mgeni alionekana kujiamini sana kuliko maelezo.

Solomoni maumivu yakampungua nae akachora huku akimtizama binti kwa makini bila kufanya papara ya kushambulia.

Binti akacheza kidogo na kumpelekea makonde manne ya haraka haraka ambayo yalipanguliwa kihodari na solomoni.

Kisha bila kutarajia binti akajikuta akivutwa kwa kasi na kupigwa kiwiko cha uso kilichompeleka chini bila kupenda alipotaka kunyanyuka akajikuta akitandikwa teke la tumbo lililomrudisha chini kama mzoga wa kiboko majini.

Binti akawahiwa kwa kupigwa kabari matata wakati akijaribu kujiinua kupambana huku nafsini akijuta kumchukulia poa Solomoni.

Kabali ilizidi kumdumaza binti huku akikohoa na kutapatapa kama Mhaya aliepaliwa na Senene.

Solomoni akataka kupeleka mkono ili amvue kofia ya kuficha uso.

Hakutimiza matakwa yake akajikuta akipigwa mtama safi uliompeleka chini kwa mara nyingine huku akiona mpigaji akiwa nyuma yake.

Alimwachia binti na kusambaratika chini kama mzoga.

Akafanya haraka kujinyanyua baada ya kuona binti kapata usaidizi wa mtu ambae hakujua alikotokea.

Kabla hajasimama vizuri akajikuta kisu kikitua sawia tumboni mwake na kabla hajataka kukichomoa akapigwa mateke mawili ya kifuani na hata kabla hajaanguka akajikuta akijaa kwenye kabari matata ya mwanamke.

Akafurukuta lakini maumivu ya kisu na kuvuja damu kukampunguzia uwezo wa kujikomboa.

Taratibu akaanza kuhisi kizunguzungu na kuhisi akiachiwa na mkono wa chuma uliokuwa umemkaba.

Alihisi mabishano yakiendelea baina ya watu wale ila hakusikia kitu zaidi ya miluzi ilioanza kujenga urafiki na masikio yake.

***

Zilipita dakika kadhaa ndipo alipohisi kuna hali ya tofauti kutoka pale alipokuwa amelala.

Mwili hakuwa na nguvu lakini alisikia joto jingi huku akianza kupaliwa na alipofumbua macho akakutana na wingu la moshi mzito.

Nyumba ilikuwa inaungua!!.

Akajaribu kuinuka ila hakuwa na nguvu,akajaribu tena akashindwa.

Akakata tamaa na tayari alisikia mmomonyoko wa mabati kutokea huko vyumbani.

Kifo kilinusa pua za Solomoni Bukaba.

****
Saana tu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kwani huyu jamaa akitoa riwaya anacheleweshaga inayofuata kama hivi? Manaake mi naona kama anafanya makusudi si kwa kutukalisha muda wote huu afu anatoa moja tu.
Mkuu pengine jamaa mambo mengi hivyo akipata chansi ndo tunapata kama hiki cha jogoo
 
Mkuu pengine jamaa mambo mengi hivyo akipata chansi ndo tunapata kama hiki cha jogoo
Aise ni nouma sana, mi naona bora hata jogoo anamuridhisha jike kuliko hii ya kuchungulia tu na kupotea.
Labda kweli mambo mengi, lakini kiukweli anatukata stimu sana.
 
Back
Top Bottom