*NI IPI NAFASI YA MAWAZIRI NA MANAIBU WAZIRI BAADA YA BUNGE KUVUNJWA?*
Na Abbas Mwalimu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anatarajia kulivunja Bunge siku ya Ijumaa tarehe 29/05/2020.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopo kwenye tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (
Parliament of Tanzania) inayoelekeza Mabadiliko ya Ratiba ya Mkutano wa Kumi na Tisa wa Bunge (Mkutano wa Bajeti) inaonesha kuwa siku hiyo (tarehe 29/05/2020) itakuwa na shughuli tatu ambazo ni:
(i) Taarifa ya Kamati ya PAC na LAAC
(ii) Hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(iii) Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufunga Bunge.
Uwanja wa Diplomasia umepokea maswali kutoka kwa baadhi ya wadau wa ukurasa huu wakitaka kufahamu nafasi ya Mawaziri na Manaibu Waziri baada ya kuvunjwa kwa Bunge kwa kuwa Katiba inaonesha kuwa Wabunge hukoma ubunge wao baada ya Rais kulivunja Bunge.
Lakini kabla ya kuanza kufahamu nafasi ya mawaziri na manaibu waziri ni vema kwanza tukatambua mazingira au wakati ambao Rais huweza kulivunja Bunge.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 90 ibara ndogo ya pili inaeleza kama ifuatavyo:
90-(2) Rais hatakuwa na uwezo wa kulivunja Bunge wakati wowote, isipokuwa tu-
(a) kama Bunge limemaliza muda wa uhai wake kwa mujibu wa ibara ya 65 ya Katiba hii; au wakati wowote katika miezi kumi na miwili ya mwisho ya uhai wa Bunge, isipokuwa tu kama Spika amepokea taarifa rasmi inayopendekeza kuundwa kwa Kamati Maalum ya Uchunguzi kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba hii; ibara ya 46A ibara ndogo ya kwanza inasomeka kama ifuatavyo:
46A.-(1) Bila ya kujali masharti ya ibara ya 46 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshtaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.
Ifahamike kuwa Ibara ya 46A inahusiana na kumuondoa Rais madarakani kutokana na sababu zilizoainishwa kwenye ibara ndogo za ibara hiyo, hivyo hili halihusiani na kile tunachoelimishana leo.
Ibara ya 65 ibara ndogo ya pili inazungumzia maisha na ukomo wa Bunge kama ifuatavyo:
(2) Kwa madhumuni ya Katiba hii maneno "maisha ya Bunge" maana yake ni ule muda wote unaoanzia tarehe ambapo Bunge jipya limeitishwa kukutana kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu na kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha Uchaguzi Mkuu mwingine wa kawaida kufanyika.
Sababu nyingine zinazoweza kufanya Rais alivunje Bunge kwa mujibu wa Katiba ni hizi zifuatazo:
(b) kama Bunge limekataa kupitisha Bajeti iliyopendekezwa na Serikali;
(c) kama Bunge limekataa kupitisha Muswada wa sheria kwa mujibu wa idara ya 97(4) ya Katiba hii; ibara hii ya 97 ibara ndogo ya nne inasomeka kama ifuatavyo:
97-(4) Iwapo Muswada umerudishwa kwa Bunge na Rais, halafu ukaungwa mkono kwenye Bunge na Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kama ilivyoelezwa katika ibara ndogo ya (3) na kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya kupata kibali chake kwa mara ya pili kabla haujamalizika muda wa miezi sita tangu uliporudishwa, basi Rais atatakiwa kuukubali Muswada huo kabla ya kumalizika muda wa siku ishirini na moja tangu Muswada huo ulipowasilishwa kwake la sivyo basi itabidi alivunje Bunge.
Lakini pia Rais anaweza kulivunja Bunge ikiwa Bunge limekataa kupitisha hoja ya msingi ya serikali, kama inavyoeleza:
(d) kama Bunge limekataa kupitisha hoja ambayo ni ya msingi katika sera za Serikali, na Rais anaona kwamba njia ya kuendelea kutoka hapo si kumteua Waziri Mkuu mwingine bali ni kuitisha Uchaguzi Mkuu;
Na mwisho ni pale Rais anapoona hakuna uwezekano wa kuunda serikali mpya kama kifungu (e) kilivyofafanua:
(e) endapo, kutokana na uwiano wa uwakilishi wa Vyama vya Siasa katika Bunge, Rais anaona kwamba hakuna uhalali kwa Serikali iliyopo kuendelea kuwapo, na wala haiwezekani kuunda Serikali mpya.
(3) Muda wa maisha ya Bunge ukimalizika Bunge litahesabiwa kuwa limevunjwa; isipokuwa kwamba muda huo ukisha wakati wowote ambapo Jamhuri ya Muungano iko katika vita Bunge laweza mara kwa mara kuongeza muda huo uliotajwa katika ibara ya 65 ya Katiba hii kwa muda usiozidi miezi kumi na miwili mara kwa mara lakini maisha ya Bunge hayawezi kuongezwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo kwa muda unaozidi miaka mitano.
*BAADA YA BUNGE KUVUNJWA, MAWAZIRI NA MANAIBU WAZIRI HUENDELEA NA MAJUKUMU YAO?*
Kujibu hili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kama ifuatavyo katika ibara ya 57 ibara ndogo ya pili kifungu (b) kwamba:
(b) ikiwa mwenye madaraka hayo (ya Uwaziri au Unaibu Waziri) atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge;
Hivyo basi kwa mujibu wa Katiba Mawaziri na Manaibu Waziri wataendelea kuwa katika viti vyao licha ya kuvunjwa kwa Bunge na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isipokuwa kama kuna sababu nyingine tofauti na sababu ya kuvunjwa kwa Bunge.
Wataendelea kushika nafasi hizi mpaka pale Rais Mteule atakapopatikana kufuatia uchaguzi mkuu, hili limeainishwa katika Ibara hiyo ya 57 ibara ndogo ya pili kufungu (f):
(f) ukiwadia wakati wa Rais mteule kushika madaraka ya Rais basi mara tu kabla Rais mteule hajashika madaraka hayo;
*Swali ni je kwa nini Mawaziri na Manaibu Waziri waendelee kuwepo kwenye viti vyao ikiwa nao ni wabunge kama wabunge wengine?*
Jibu ni kwamba, Mawaziri ambao kimsingi ni sehemu ya Baraza la Mawaziri kwa nafasi zao ni washauri wa Rais katika masuala mbalimbali ya kiungozi.Tukumbue mawaziri husaidiwa na manabu waziri hivyo nao wana umuhimu kuendelea kuwepo ili wawasaidie mawaziri husika.
Ibara ya 54.-(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafafanua kama ifuatavyo:
Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara ya 37(1) ya Katiba hii, Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais juu ya mambo yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, na litamsaidia na kumshauri Rais juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa maagizo maalum au maagizo ya jumla yatakayotolewa na Rais.
Ifahamike pia kuwa Rais halazimiki kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote isipokuwa pale Katiba inapomtaka kufanya hivyo kama ilivyofafanua ibara ya 37 (1) ambayo imegusiwa ndani ya ibara ya 54 ibara ndogo ya tatu.
37.-(1) Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote.
Hivyo basi, mawaziri na manaibu waziri wataendelea kuwa katika viti vyao licha ya Bunge kuvunjwa kwa kuzingatia umuhimu wa Mawaziri kama washauri wa Rais katika Baraza la Mawaziri ambalo huongozwa na Rais akisaidiwa na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Rejea ibara ya 54.-(1) ya Katiba ambayo inasomeka kwamba:
54.-(1) Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote.
Ni matumaini yetu tumeelimika katika hili.
Asanteni sana.