Kwa wakaazi wa Wilaya ya Rombo na maeneo mengine yote kuuzunguka mlima Kilimanjaro chochote kinachotokea kuhusiana na Mlima huu ni lazima kiwaguse moja kwa moja kutokana na maisha yao kutegemea miteremko yake kwa maelefu ya miaka iliyopita. Ingawa uwezekano wa Volcano ya mlima huu kulipuka wanasayansi wanasema ni mdogo sana lakini bado wanasisitiza kwamba ni jambo linaloweza siku moja kuja kutokea kutokana na sababu kwamba volcano yake imelala tu na si kama imekufa kabisa.
Mlima mrefu kuliko yote Afrika Kilimanjaro(Kibo) ni mlima uliotokea Duniani baada ya mlipuko wa Volcano chini ya ardhi yapata miaka zaidi ya 1,000,000 hivi iliyopita. Ukiwa na vilele duara 3 (cones), Shira, Kibo na Mawenzi, kila kimoja kilijitengeneza kwa wakati wake huku Shira(kilele-mama) kikiwa ndicho kilichoanza kutokea yapata miaka zaidi ya mlioni 2.5 iliyopita kisha kikaja kuzimika kabisa (kufa) na kuzuka Mawenzi na Kibo vilivyoanza wakati mmoja miaka 1,000,000 iliyopita.
Kufikia miaka 450,000 iliyopita kilele cha Mawenzi kilisimama kabisa kurusha volcano na kuwa volcano mfu pia(iliyokufa) huku Kibo kikiendelea kurusha volcano yake mpaka ilipofika miaka 150,000 hadi 200,000 iliyopita ambapo nacho kilisimama lakini kwa muda tu siyo kufa kabisa kama wenzake Mawenzi na Shira. Hii inamaanisha kwamba kuna uwezekano siku yeyote ile Kibo kikaja kuanza tena kulipuka na kurusha volcano na majivu ya moto.
Kwa mujibu wa Wataalamu wa mambo ya miamba(geologists) Mlima Kilimanajaro na milima mingine ya kivolcano iliyopo Africa Mashariki kama mlima Kenya, mlima Meru, Mlima Elgon, Ol Doinyo Lengai, Dalafilla, longonot, mlima Nyiragongo pamoja na Maziwa mbalimbali kama vile ziwa Victoria, Nyasa, Tanganyika, Turkana nk. ingawa si vyote vipo ndani ya bomde la ufa lakini vyote ni matokeo ya shughuli za kivolcano zilizosababishwa na mpasuko wa umbo la nje la ardhi ya dunia (
tectonic plates) ambazo kila moja hujivuta kutoka kwa mwenzake na kusababisha Bonde kubwa la ufa kutokea katikati.
Mpasuko huo umesababisha baadhi ya maeneo kuwa dhaifu hivyo kusababisha eneo la ndani kabisa la Dunia ambalo kimsingi huwa na joto kali sana kupitisha uji-uji wenye mchanganyiko wa madini mbalimbali na miamba nje ya uso wa dunia(volcano). Uji huu ndio husababisha milima kama Kilimanjaro kutokea taratibu baada ya maelfu ya miaka kupita ukitiririka. Bonde la ufa limeanzia huko Ethiopia mpaka Msumbiji likipitia nchi za Somalia, Kenya, Uganda, Burundi, rwanda, Malawi na Zambia.
Katika eneo ulipozuka mlima Kilimanjaro na kwa kuwa bado shughuli za kivolcano bado zinaendelea chini ya ardhi hasa ukanda mzima wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki basi kuibuka kwa hali kama tunayoishuhudia Rombo yawezekana isiwe ni jambo la ajabu sana. Eneo tukio la Rombo lilipotokea si mbali na ulipo Mlima Kilimanjaro.
VIASHIRIA VINGINE.
ZIWA CHALA
Ziwa chala ni moja kati ya “vijitoto” vilivyotokana na volcano iliyounda mlima Kilimanjaro, ni ziwa lililopo Wilayani Rombo na linakadiriwa kutokea muda sawa na kilele cha Kibo miaka takriban 200,000 ilyopita. Utafiti uliofanyika kwenye ziwa hilo kwa kuchunguza matabaka ya mlundikano wa majivu ya volcano (
tephra layers) ndio uliothibitisha muda halisi wa kutokea kwa mlipuko wa mwisho kiasi cha mikaka 150,000 hadi 200,000 tofauti na jinsi ilivyodhaniwa kabla kwamba ni mamilioni ya mika mingi iliyopita. Hivyo unaweza kuona miaka 200 elfu si mingi sana katika umri wa kijiolojia.
Mpaka sasa hivi hata watu wanaopanda mpaka kufika kilele cha Uhuru wanaweza kuhisi harufu ya gesi za salphur kutokea katika Crater ya mlima Kilimanjaro pale juu kabisa, ishara kwamba bado kuna shughuli za kivolkano bado zinaendelea chini ya mlima huu lakini kwa kiwango cha chini (
under low pressure) kiasi majivu na uji wa miamba haviwezi kuruka umbali mrefu
Binafsi mimi (
Haya ni maoni yangu lakini) nimefikiria moto wa Rombo labda inawezekana ikawa ni moja kati ya viotea vya mlima Kilimanjaro (
monogenetic parasitic eruption associated with Mt Kilimanjaro) mfano wa ziwa chala na vilele vingine mfano kama ilivyotokea mawenzi na Kibo baada ya Shira, ingawa hivi vya sasa vyaweza kuwa na athari ndogo sana na vinavyoisha muda mfupi tu vikiwa na majivu ya udongo wa moto badala ya volcano na uji mzito wa miamba ya chuma shauri ya presha ndogo iliyopo ardhini kwa sasa.
Katika maeneo mengine Afrika Mashariki katika ukanda wa Bonde la Ufa kumewahi kuripotiwa moto wa ardhini ingawa sifikirii kama unafanana kabisa na huu wa Rombo. Huko Kenya mpaka wamefikia hatua ya kufua umeme kwa kutumia moto kama huu (
Geothermal energy). Katika maeneo mengine duniani mfano katika msitu wa Amazon nimewahi kusoma kuna eneo fulani pana mto wa maji moto yanayochemka, nadhani pengine inaweza kuwa ni kitu kama hikihiki kilichotokea Rombo.
MATETEMEKO YA ARDHI
Bado Rombo na maeneo mengine kando kando ya Kilimanjaro kuna nyakati hutokea matetemeko ya ardhi, ishara nyingine kwamba shughuli za kivolcano chini ya eneo zima na ukanda wa bonde la ufa la Afrika Mashariki bado zinaendelea. Tetemeko la ardhi la mwisho lilitokea Rombo mwaka jana.
Tafiti nyingi sana zimeshafanyika na wanasayansi kuhusiana na uwezekano wa kulipuka tena kwa mlima Kilimanjaro, unaweza kutafuta
“google’ na kuona ingawa karibu kila mtafiti anasema kwamba hamna uwezekano mkubwa wa mlima huo kulipuka tena hivi karibuni na hata yawezekana kilele cha Kibo kikaja kufa kabisa kama wenzake Shira na Mawenzi. Hili lakini halina uhakika kwa asilimia mia moja.
Wakaazi wa Kilimanjaro tukio kama hili la Rombo halipaswi kutupa taharuki, badala yake tutulie tukichukua tahadhari pamoja na ushauri serikali itakaoutoa baada ya Wataalamu wake kumaliza uchunguzi.
Ingawa Wataalamu wengi wameshafanya tafiti mbalimbali na kuthibitisha volcano ya mlima Kilimanjaro kutokuweza kulipuka hivi karibuni na hata hivyo kungelikuwa na viashiria vikubwa zaidi kama matetemeko na gesi nyingi kuonekana katika crater ya Kibo. Mabadiliko makubwa ya kijiolojia huchukua mamilioni ya miaka hivyo ukilinganisha na umri wa vizazi vyetu usiozidi hata miaka 100 unaweza kuona ni sawa tu na tone dogo sana la maji baharini.
Hata hivyo serikali ina wajibu wataalamu wake kuchunguza na kutoa maelezo ya uhakika zaidi kwetu wananchi ikiwa ni pamoja na tahadhari za kuchukua ikiwa kama kuna hatari zozote zile zinazoweza kuambatana na mabadiliko ya kijiolojia hata kama yatakuwa ni madogo kama haya ya Rombo ili kuepusha Wananchi kuingia taharuki au kwenye imani zingine potofu mfano za ushirikina nk.
View attachment 1960785
Makala hii imeandikwa na mtafiti wa masuala ya kijamii kwa msaada wa vyanzo mbalimbali mtandaoni.