Oljoro na Mgulani - Operation vyama vingi 1991 - 1992.Sanctus,
Mimi niliamua kukwepa kwenda Tabora na kuamua kwenda Oljoro kwasababu nilikuwa na kakangu mjini Arusha. Nikajua nikitoroka nitakuwa na sehemu kwa kubugia ugali.
Basi kufika Oljoro, tukamkuta afande Dauda, (sijui kama linaandikwa hivyo) alikuwa ndio mkuu wa mafunzo. Akasema mwaka jana alitoa kibali cha kuua kruta watano, akasema aligundua haikutosha, anawaamrisha maafande mwaka huu kuua kruta mpaka 15.
Kesho yake watu kibao wakatoroka na kwenda ku report kambi zingine. Isingelikuwa kuwa na brother hapo mjini na mimi ningelirudi kule Tabora usiku huo. Baada ya muda tukaja gundua kumbe Dauda ndiye alikuwa afande poa kuliko wengine wote.
Tulikuwa na afande mmoja Mhehe alikuwa anaitwa Mduda. Alikuwa anajifanya anajua jeshi kweli kweli. Akaopoa mtoto wa maana sana. Siku moja tumemaliza jeshi tuko mlimani, akaingia mlimani hall D na magwanda, kaja kufuata mtoto wake. Maskini yule msichana alikuwa terrified, akajificha. Jamaa akasubiri pale wee, mpaka akaamua kujikata. Alifikiri yale ya jeshini yanaendelea uraiani. Tulimsanifu kweli siku hiyo.
Looh! ni miaka karibu 20 toka wengine tuondoke JKT lakini naona michapo yake inakuja tu. Waswahili tungelikuwa tunaandika vitabu, tuna mengi ya kusimulia.
Commanding Officer (CO), Major Miruddy (RIP)
Kombania D (Danger Coy). Mkuu wa kombania, sajenti Kinama.
Mgulani - CO, Colonel Sanga (RIP)
RSM, Warranty Officer I Kitomari (RIP).
Oljoro ilikuwa ni marufuku kula bila kachumbari. Nyanya zilikuwa kibao. Tulilima shamba 'dunia' na kuchonga tofari kwenye miamba. Tofali zilijenga nyumba za askari pale kikosini. Kuni tulifuata 'shimo la Mungu'. Mwanzo maisha yalikuwa magumu kwani tulitoka mjini. Baadae maisha yalikuwa safi mno mpaka tukanenepa. Chakula kingi, unapiga kazi mwili unajengeka. Hakuna unachowaza zaidi ya kula na kazi tu. Wasichana unawaona kama 'wanaume' wenzio tu. Matamanio hakuna kabisa. Tumeiba sana mahindi shambani kwa tajiri Lasseko na kuyakaanga bisi porini kwenye madebe. Kulenga shabaha tulitumia Semi Automatic Rifle (SAR), Sub Machine Gun (SMG) AK47, 'silaha ya msaada' Light Machine Gun (LMG), G3 na machine pistol (MP7). Wengine hizo mnaziona kwenye 'action movies' tu!
Kilimo kilivyochachamaa Oljoro 'nikatorokea' mjini Mgulani. Maisha ya mjini yakawa magumu mno. Chakula hakikuwa makini kama Oljoro! Maharage yana wadudu na ugali 'mchinjo' mpaka nilikonda! Kazi ilikuwa ni kukata michongoma mpaka unanukia 'majani'! Deal ya maana ilikuwa kwenda kwenye sherehe kufunga mahema hasa majumbani kwa VIPs. Nakumbuka mzee Kingunge alikuwa na sherehe kwake akaja kikosini kwa ajili ya mahema. Tukaambiwa twende kwake tufunge mahema kisha turudi kikosini mara moja. Kufika kwa mzee Kingunge (RIP), tukapiga kazi tukamaliza baada ya masaa machache tu. Tukaenda kumuaga mzee turudi kikosini. Mzee akatuambia tubaki kwenye sherehe tumsaidie kufanya doria wakati wa sherehe pale nyumbani. Tukapewa 'mtungi' wa kufa mtu! Sherehe ikaisha usiku wa manane mzee akaturuhusu turudi kikosini Mgulani tuko 'mchupa' mbaya! Kufika 'mlangoni' mzee MP akashtukia tuko pombe. Wacha tugaragazwe!
Haya ni machache tu! Sijuti kupitia JKT!