Mgao wa walimu usitishwe Dar, Kilimanjaro- Wabunge
2008-07-16 09:45:01
Na Mashaka Mgeta, Dodoma
Serikali imeshauriwa kusitisha mgawo wa walimu kwa mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, badala yake waelekezwe katika mikoa mingine inayokabiliwa na upungufu wa wataalamu hao.
Hayo yalisemwa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bungeni, mjini hapa jana.
Mbunge wa Kibiti (CCM), Bw. Abdul Marombwa, alisema takwimu zinaonyesha kuwepo idadi ya walimu yenye uwiano wa mwalimu mmoja kwa wananfunzi 38 katika mikoa hiyo, hali ambayo ni tofauti na mikoa mingine yenye uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi zaidi ya 100.
Alisema kama kuna maeneo yenye walimu wachache jijini Dar es Salaam na mkoani Kilimanjaro, inatokana na upungufu katika mgawanyo wa walimu waliopo.
Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi, Dk. Lukas Siyame, alisema jimbo hilo ni miongoni mwa maeneo ya pembezoni yanayokabiliwa na uhaba wa walimu, ambapo kuna wastani wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 200.
Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Bw. Charles Mlingwa, alishauri Serikali kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu na kupanua wigo wa elimu ya juu nchini.
Aidha, Bw. Mlingwa, alisema mfumo wa elimu unapaswa kuruhusu pawepo mabadiliko yatakayofuta mitahani ya kidato cha pili.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, alipendekeza kuwepo mabadiliko katika Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ili kutoa fursa kwa watoto hasa wanaotoka kwenye familia maskini, kupata elimu.
Bw. Hamad, ambaye pia ni Kiongozi wa upinzani bungeni, alisema mfumo uliopo sasa, unaomtaka mwanafunzi kutanguliza asilimia 20 ya malipo yanayohitajika, unawanyima watoto wengi kupata elimu hiyo, hivyo kukinzana na ibara ya 11 ya Katiba.
Kwa mujibu wa maelezo ya Bw. Hamad bungeni, ibara hiyo inazungumzia haki ya raia kupata elimu.
Pia, Bw. Hamad, alisema vigezo vinavyotumika kupitia mtandao wa kompyuta katika kupata uhalisi wa hali ya kiuchumi katika familia wanapotoka wanafunzi hao, vinaweza visitoke majawabu yanayokidhi ukweli kuhusina na suala hilo.
Hivyo, alipendekeza mfumo huo upitiwe upya kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Bw. Hamad, alisema ili kuhamasisha ushiriki wa wanafunzi wengi katika masomo ya sayansi, kuna haja ya kuweka mazingira bora, kama vile kuongeza fedha kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
Mbunge wa Ubungo (CCM), Bw. Charles Keenja, alipongeza serikali kwa kufanikisha ujenzi wa shule za sekondari katika ngazi za kata, na kupinga hoja za watu wanaozikejeli.
Hata hivyo, Bw. Keenja, alisema ujenzi wa shule hizo jijini Dar es Salaam, unafanyika kwenye maeneo yaliyo nje ya makazi ya watu, na hivyo kusababisha tatizo la usafiri kwa walimu na wanafunzi.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuwekeza katika ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu.
Mbunge wa Mkwajuni (CCM), Bw. Mzee Ngwali Zubeir, alisema mfumo wa mitaala ya ufundishaji kati ya Zanzibar na Tanzania Bara una matatizo yanayohitaji kushughulikiwa, ili kupata suluhu.
Bw. Zubeir, alitoa mfano kuwa wanafunzi wa shule za msingi visiwani Zanzibar, wanatumia mitaala inayoandaliwa visiwani humo, lakini wakijiunga sekondari, wanatumie inayotumika katika Muungano na kufanya mitihani ya Baraza la Mitihani.
Alisema tofauti hiyo inaweza kuondolewa kwa kuweka utaratibu unawezesha wanafunzi wa pande mbili za Muungano, kutumia mitaala inayofanana tangu elimu ya awali.
Aidha, Bw. Zubeir, alisema takwimu zilizopo, zinaonyesha wanafunzi wa Zanzibar kufanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne na sita, ikilinganishwa na wale wa Tanzania Bara.
Pia, alizungumzia umuhimu wa kuwajali na kuwathamini walimu, kwa kuwajengea mazingira bora ya kazi na kuwaepusha na vitendo visivyokidhi ridhaa yao, kama kuwakata michango bila kuwashirikisha.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Bi. Merce Mussa Emmael, alipendekeza kutolewa adhabu kwa wanafunzi wanaopata mimba, kama inavyofanyika kwa wanafunzi wa kiume wanaowapa mimba wanafunzi wa kike.
Alisema hali hiyo itawezesha wanafunzi wa kike kuwa makini katika kufanya mahusiano yasiyofaa na wanafunzi wa kiume.
Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wameilalamikia serikali kwa kushindwa kuboresha elimu na mazingira ya kazi kwa walimu nchini.
Mbunge wa Wete (CUF), Bw. Mwadini Jecha, alisema ubora wa elimu si suala linalothibitishwa kwa maneno ama kuwepo kwa vitu kama madawati na madarasa, bali kuwepo walimu bora na mazingira mazuri ya utendaji kazi.
Bw. Jecha, alisema ubora wa elimu hautakuwa na manufaa ama kufanikiwa ikiwa walimu hawatathaminiwa.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bi. Bernadeta Mushashu, alisema baada ya kutekeleza mpango wa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi katika shule za umma, jitihaza inayotakiwa sasa ni kuboresha elimu inayotolewa nchini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Bi. Mkiwa Kimwanga, alisema uboreshaji wa elimu unapaswa kufanyika kwa kuwahusisha walimu, maeneo ya ufundishaji na mazingira ya kazi.
Awali, akiwasilisha hoja za upinzani, Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Suzan Lyimo, alisema uboreshaji wa elimu ni sehemu ya vigezo vinavyochangia ukuaji wa uchumi.
Bi. Susan alisema mfumo wa elimu hivi sasa unatoa fursa za kuwepo dhana ya ubaguzi kutokana na walio wachache kupata elimu bora wakati masikini walio wengi wanapata elimu ya kati ama kuikosa kabisa, hivyo kubaki katika mazingira ya umasikini.
Mbunge wa Kibondo (CCM), Bw. Felix Kijiko, alisema kuna haja kwa serikali kushughulikia kwa undani matatizo yanayowakabili walimu na sekta ya elimu nchini.
Alisema katika kufanikisha hilo, serikali inapaswa kufanya kazi kwa karibu na Chama Cha Walimu (CWT) chenye mtandao wake nchi nzima, ili kubaini matatizo yanayowakabili walimu.