Lowassa amwokoa Mramba Julai 5, 2007
Mbunge ataka aadhibiwe kwa kuliongopea Bunge
Ambiwa bajeti imeandaliwa hovyo, kwa ubabaishaji
Mwandishi Wetu, Dar na Martha Mtangoo, Dodoma
WAZIRI wa Miundombinu, Basil Mramba, jana alihenyeshwa na wabunge, kiasi cha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuingilia kati kumwokoa.
Pamoja na Lowassa, mawaziri wengine walilazimika kusimama kumsaidia kujibu hoja nzito za wabunge.
Miongoni mwa mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, John Magufuli; na mwanasiasa mkongwe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano wa Jamii, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Pamoja nao, mwingine aliyejitwika jukumu la kumwokoa Mramba ni Waziri wa Fedha, Zakia Meghji.
Dalili za Mramba kubanwa zilianza kujionyesha mapema, hata kabla ya kuwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007.
Baadhi ya waliombana barabara ni Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM); Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP); Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir (CCM) na Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi (CCM).
Bunge likiwa limekaa kama kamati, ili kupitia kifungu kwa kifungu cha bajeti ya wizara hiyo, Selelii, alimbana Mramba kwa kusema anachozungumza na kilichoandikwa kwenye bajeti yake ni tofauti.
Awali, Mramba aliliambia Bunge kwamba, Barabara ya Manyoni-Itigi- Tabora-Kigoma imetengewa sh milioni 535 kwa ajili ya usanifu.
Selelii alipinga maelezo hayo, na kuyaita ya ubabaishaji kwa vile fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya Barabara ya Nzega-Tabora.
Mramba alijitafuna tafuna kwa maneno, na akawa anashikilia msimamo wake kwamba barabara zilizotajwa na Selelii, zitatafutiwa fedha.
Mbunge huyo alitaka Mramba aeleze kifungu kinachoonyesha fedha zilizotengwa, lakini Mramba aliposimama, alishindwa kuthibitisha maneno yake.
Selelii alisema wabunge wanapodai maendeleo katika maeneo yao hawamaanishi kuwa wanaleta mambo ya ukanda.
Alisema ni serikali inayoleta mambo ya ukanda kwa kuwa fedha zinatengwa kuendeleza sehemu kadhaa, na kuacha sehemu nyingine ambazo hazina usafiri wa barabara, treni au ndege.
Kutokana na majibu mengi ya ubabaishaji, mbunge mmoja alisimama na kutaka mwongozo wa Spika ili Mramba ashughulikiwe kwa maelezo kwamba alikuwa ameliongopea Bunge.
Hoja hiyo ilizimwa ‘kisayansi' na Spika, Samuel Sitta, ambaye alisema alichofanya Mramba si kuliongopea Bunge, bali kubabaika tu wakati wa kujibu maswali ya wabunge hao.
Katika harakati za kuhakikisha bajeti inapitishwa, Lowassa alisimama na kulihakikishia Bunge kuwa, ujenzi wa barabara zilizotajwa na Selelii, utakamilika ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Sitta, naye alilazimika kumpooza Selelii ili aachie shilingi, bajeti ipite. Alisema atasaidiana na serikali katika kuhakikisha kuwa barabara hizo zinajengwa.
Baada ya wabunge kumbana vilivyo Mramba, Ngombale-Mwiru, alisimama bungeni kabla ya Mramba katika kilichoonyesha kuwa ni kujaribu kupooza makali ya wabunge.
Alisema hakusimama kwa ajili ya kujibu hoja za wabunge, bali baada ya kusisimuliwa na hoja zao.
Alisema umefika wakati sasa kwa serikali kupanga bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kero za Watanzania.
Alisema dhana iliyoibuka bungeni ya kutaka serikali kutenga fedha za ujenzi wa barabara kikanda, haifai kwa maelezo kwamba italeta matatizo katika kanda zitakazotengewa fedha nyingi.
"Dhana ya kanda ambayo imejitokeza katika mijadala hapa bungeni, italeta matatizo ya kisiasa na hasa katika mikoa ambayo itatengewa fedha nyingi na mikoa ambayo itatengewa fedha kidogo," alisema.
Alisema suala la barabara kutengewa fedha kikanda haliafiki kwa kuwa linaweza kuleta matatizo makubwa hapo baadaye na hasa katika suala la siasa na linaweza kuwagawa watu kisiasa.
Alisema iwapo fedha hizo zitatolewa kikanda, basi isitumiwe katika dhana ya kisiasa.
Akijibu hoja zilizotolewa na wabunge, Mramba alisema Barabara ya Marangu- Tarakea, yenye kilometa kenda, na ambayo imetengewa sh bilioni 17, imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mramba alisema wizara yake itazipa kipaumbele barabara zilizoanza kushughulikiwa tangu uongozi wa awamu ya tatu.
Alisema tayari ameshakabidhiwa kitabu cha maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM chenye ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Kuhusu wabunge waliokuwa wametangaza kugoma kupitisha bajeti yake, Mramba alisema kesho ataondoka kwenda nje ya nchi kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zao.
"Mheshimiwa Spika, natarajia kwenda ng'ambo kutafuta wafadhili kwa ajili ya kupata fedha za kutengenezea barabara alizozizungumzia Mheshimiwa Selelii," alisema.
Aliomba wabunge wapitishe bajeti yake ili aweze kupata usingizi mzuri na kuamka vizuri kwa ajili ya kuonana na wafadhili hao.
Alisema anatambua uchungu wanaoupata wabunge ambao barabara kwao bado ni tatizo, na kwamba ushauri wao ameupokea bila kinyongo kwa moyo safi, bila kutazama nyuma.
"Waheshimiwa wabunge, naomba mnielewe kwa kuwa hata mimi pia ni mbunge mwenzenu, nitakaporudi kuwa kama ninyi nitazungumza, huu uwaziri ni sawa na mazungumzo baada ya habari, nimepata somo, nimejifunza na nitaingia kazini kwa kasi, ari na nguvu mpya," alisema kwa unyenyekevu.
Pamoja na vikwazo vyote, mwishoni wabunge walipitisha bajeti hiyo kwa wengine kutoa sauti za "siyooo!"