Habari JamiiCheck, ni upi uhalisia wa madai haya kuwa iwapo mwanamke atakula ndizi pacha atapata ama atakuwa na uwezekano wa kupata watoto mapacha?
- Tunachokijua
- Ujauzito ni kipindi ambacho kijusi kimoja au zaidi hukua ndani ya kizazi. Mara nyingi ujauzito hutokea baada ya kufanya tendo la ndoa, lakini unaweza pia kutokea kupitia njia za kiteknolojia za kusaidia uzazi.
Mayai ya uzazi huhifadhiwa kwenye ovari. Katika kila mzunguko wa hedhi, ovari hutoa yai moja. Yai hilo husafiri taratibu kupitia mrija wa uzazi (fallopian tube), ambako husubiri mbegu ya kiume. Mchakato huu, unaoitwa ovulation, huchukua takribani saa 12 hadi 24.
Madai
Kumekuwapo na nadharia ya muda mrefu kuwa ukila ndizi pacha haswa kwa mwanamke kuna uwezekano wa kupata watoto mapacha. Nadharia hiyo inaenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hali hiyo inaweza kutokea iwapo atakula chakula chochote chenye pacha ikiwemo pia mayai.
Uhalisia wa madai haya ni upi.
Kama ilivyoelezwa ujauzito unatokana na urutubishaji unaofanywa na mbegu za mwanaume kwenye yai la mwanamke, na si kwa matunda.
Tovuti ya cleverland clinic inabainisha kuwa ujauzito wa mapacha huwa unatokea bila mtu kutarajia lakini zipo sababu ambazo zinapelekea kuchangia mtu kupata mapacha ikiwemo;
- Umri; Inaelezwa kuna uwezekano wa mwanamke kutoa yai zaidi ya moja anapokuwa kwenye umri wa kuanzia miaka 30.
- Historia ya familia; Kuna nafasi kubwa ya kupata mapacha iwapo mwanamke huyo anatokea kwenye familia ambayo mama yake pia amewahi kupata mapacha
- Aina ya mwili; Ikiwa BMI yako ni zaidi ya 30, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ujauzito wa mapacha.
- Matibabu ya kuongeza uwezo wa kushika mimba; Ujauzito wa mapacha hutokea kwa uwezekano mkubwa zaidi kwa wanawake wanaotumia dawa za kuongeza uzazi au wanaopitia matibabu kama IVF (urutubishaji wa yai nje ya mwili).
- Ujauzito wa nyuma; Kama uliwahi kupata ujauzito wa mapcha hapo awali kuna uwezekani mkubwa wa kupata mapacha tena.