Na Ramadhan Semtawa
JESHI la Polisi limeanza kuwachunguza mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa chama hicho Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa tuhuma za uchochezi.
Tuhuma hizo zinatokana na maneno ambayo wanasiasa hao, wamekuwa wakiyatoa sehemu mbalimbali kabla na katika ziara zao zinazoendelea mikoani hivi sasa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Kamishna Robert Manumba, alilisema uamuzi huo hauna maana ya kuingilia uhuru wa raia kutoa maoni, bali kuhakikisha kuwa sheria za nchi hazikiukwi.
Akifafanua kuhusu tuhuma hizo, Kamishna Manumba alisema Agosti 14, mwaka huu, Kabwe akizungumza katika kituo cha televisheni ya Channel Ten, alisikika akiwashawishi wananchi wayashambulie kwa mawe malori yanayobeba mchanga kutoka machimbo ya Bulyanhulu, mkoani Shinyanga.
Aliongeza kwamba, Septemba 9, mwaka huu, Mbowe akiwa katika ziara ya viongozi wa vyama vya upinzani mjini Tabora, alisikika akiwataka askari wa majeshi yote, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla, kuachana na dhana ya amani na utulivu na kwamba wapo tayari kuwasha moto.
Kutokana na matamshi hayo, kamishna Manumba alisema tayari polisi makao makuu imemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora kuanza uchunguzi mara moja.
"Jeshi la Polisi lenye dhamana ya kulinda amani na utulivu nchini, linachukua hatua za kuchunguza matamshi ya viongozi hao kama yamekiuka sheria," alisema na kuongeza:
"Kwa kuanzia, tumemwelekeza Mkuu wa Polisi Mkoa wa Tabora kuanza uchunguzi mara moja kuhusu matamshi ya uchochezi yanayodaiwa kutamkwa na viongozi hao walipokuwa mikoani humo.
"Jeshi la polisi limekuwa likifuatilia kwa makini kauli zinazotolewa na viongozi hao wa kisiasa ili kuhakikisha kuwa malumbano ya kisiasa yanayoendelea hayakiuki sheria za nchi, kwa lengo la kudumisha amani na utulivu nchini."
Kamishna huyo alifafanua kwamba, kama Kabwe na Mbowe wana taarifa zozote zenye mwelekeo wa uhalifu wanapaswa kuzipeleka kwenye vyombo husika ili zifanyiwe kazi.
"Ni mategemeo ya Jeshi la Polisi kwamba viongozi wenye dhamana kama walivyo wao, wangetumia taratibu za kisheria zilizowekwa kushughulikia taarifa za uhalifu walizonazo," alisisitiza na kuongeza:
"Pamoja na uhuru wa kutoa mawazo walionao viongozi wetu wa kisiasa, tunawasihi wajiepushe kutoa kauli au matamshi yenye mwelekeo wa uchochoezi," alitahadharisha Kamishna Manumba.
Tangu kusimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge, Kabwe akiwa na viongozi wengine wa vyama vya siasa, wamekuwa wakizunguuka Mikoani kueleza mambo mbalimbali kuhusu nchi.
Kabwe alisimamishwa na Bunge kufuatia hoja yake ya kuliomba Bunge kuunda tume ya kuchunguza mkataba wa mgodi wa Buzwagi ambao ulisaininwa na Waziri wa Nishati na Madini kinyume na maagizo ya Rais Jakaya Kikwete ya kusimamisha mikataba yote mipya hadi hapo sheria ya madini itakapotiwa na kufanyiwa marekebisho
source:
http://www.mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=1562