Mtoto wa Rais wa Uganda Gen. Muhoozi Kainerugaba amesema yeye na vikosi vya majeshi yake vinaweza kuuteka mji wa Nairobi, Kenya kwa kutumia muda usiozidi wiki mbili kisha kuufanya kuwa sehemu ya nchi yake.
Kupitia mtandao wa Twitter, Gen. Muhoozi amesema hajali mipaka ya nchi iliyowekwa tangu enzi za ukoloni na ametoa hakikisho kuwa ikiwa vita itatokea katika harakati za kuichukua Nairobi basi itachukua muda mfupi kuisha.
Jumbe hizi zinaweza kuleta mgogoro wa kidoplomasia kati ya nchi hizi japo bado haifahamiki kama anafanya utani, amedukuliwa au maandiko yake yana maana ipi.
Amesema kuwa wao kama Uganda hawajali Katiba au utawala bora isipokuwa mapinduzi pekee, na kama Kenya haijui yalivyo basi wasubirie kujifunza kutoka kwao.
“Baada ya majeshi yetu kuiteka Nairobi, mimi nitaishi wapi, Westlands au Riverside?” Amehoji Gen. Muhoozi.
Katika hatua nyingine ameelezea furaha yake baada ya kuzungumza na Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye amenuahidi kutembelea nchi ya Uganda siku chache zijazo. Amesikitika kwa nini Rais huyo mwenye uelewa mkubwa wa mambo, jasiri na muungwana hakugombea mhula wa tatu wa urais kwa kuwa yeye anayo imani kuwa angeshinda.