- Source #1
- View Source #1
Je, ni upi uhalisia wa chapisho hili linalosambaa kwa kasi sana kwenye mitandao ya kijamii?
- Tunachokijua
- Ukurasa wa Mambwene Babamzazi, katika mtandao wa Facebook Aprili 18, 2026 ulichapisha taarifa kuwa Marekani imeshambulia meli ya Korea Kaskazini iliyokuwa imebeba takribani askari 13,000 waliokuwa wakielekea Urusi.
Taarifa hiyo inaelezwa kuwa ndege za kivita aina ya F-35 za Jeshi la Anga la Marekani zilifanya operesheni hiyo baharini, ambapo zilitekeleza shambulio la haraka na lenye nguvu kwa kutumia uwezo wake wa hali ya juu wa kugundua na kushambulia kwa usahihi mkubwa.
Aidha, chapisho hilo linadai kuwa meli hiyo ilikuwa sehemu ya msaada wa kijeshi kutoka Pyongyang kwenda Moscow. Inadaiwa kuwa askari hao walikuwa wamepangiwa kujiunga na operesheni za Urusi katika mzozo unaoendelea. Hata hivyo, kulingana na taarifa hizo, upelelezi wa Marekani ulifanikiwa kubaini harakati hizo mapema, na hivyo ndege za F-35 zinazojulikana kwa uwezo wake wa kutoonekana kirahisi kwenye rada pamoja na kubeba silaha za kisasa zikaamriwa kuizuia safari hiyo.
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa JamiiCheck umebaini taarifa kuhusu wanajeshi wa Korea Kaskazini kuelekea Urusi ni za mwishoni mwa mwaka 2024 na mwanzoni mwa 2025, hakuna ushahidi unaoonesha kuwa Marekani imeshambulia moja kwa moja meli ya Korea Kaskazini iliyokuwa imebeba askari kuelekea Urusi hivi karibuni.
White House, NATO, na vyombo vya kijasusi vya Korea Kusini vilithibitisha kuwa Korea Kaskazini ilituma maelfu ya wanajeshi kwenda Urusi mwezi Oktoba 2024 (makadirio ya awali yalikuwa takribani 3,000 na baadaye kuongezeka hadi zaidi ya 10,000), wakisafirishwa kwa meli hadi Vladivostok.
Aidha nyenzo za kidigitali za utambuzi wa maudhui yaliyotengenezwa kwa Akili Unde zinabainisha kuwa upo uwezekano wa zaidi ya asilimia 90 ya picha ya kulipuliwa kwa meli hiyo imetengenezwa kwa AI.