Cute Wife
JF-Expert Member
- Nov 17, 2023
- 1,906
- 5,000
Uchunguzi uliofanyika hadi sasa umefanikisha kumpata binti aliyefanyiwa ukatili huo na amehifadhiwa eneo salama na anaendelea kupata huduma zinazostahili kupewa mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo.
Aidha uchunguzi umebaini tukio hilo lilifanyikia eneo la Swaswa katika Jiji la Dodoma mwezi Mei 2024.
Pia soma: Watuhumiwa wa mande ya Ubakaji na ulawiti waliotumwa na afande wakamatwa
Pia hadi sasa uchunguzi umefanikisha kukamatwa watuhumiwa wanne kati ya sita ambao walipanga na kutekeleza uhalifu huo. Watuhumiwa hao wamekamatiwa mkoani Dodoma na Mkoa wa Pwani ambao ni Clinton Honest Damas kwa jina maarufu Nyundo, Praygod Edwin Mushi, Amini Lord Lema na Nikson Idala Jakson.
Jeshi la Polisi lingependa kueleza pia limefanikiwa kukamata watuhumiwa wanne huko Dar es Salaam waliokiuka sheria na kusambaza picha mjongeo wa tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii ambao ni Frora Mlombola, Aghatha Mchome, Madatha Jeremiah Budodi na James Nyanda Paulo.
Pia watuhumiwa wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza taarifa za uongo mitandaoni zinazosema RIP.
Binti aliyebakwa na kulawitiwa akutwa amefariki. Taarifa nyingine ya uongo inasema Mama wa binti huyo amedondoka na kufariki. Watuhumiwa wawili wamekamatwa huko Arusha na wawili Mkoani Dar es Salaam ambao majina yao ni Amos Lwiza, Adam Dongo, Venance Mallya na Isack Elias.
Uchunguzi unaendelea kukamilishwa sambamba na kuwasaka watuhumiwa wawili ambao bado wamejificha ili wafikishwe mahakamani. Kwa hawa ambao bado wamejificha kama kuna yeyote anayefahamu wamejificha kwake atoe taarifa na asipofanya hivyo wakikamatwa wakiwa nyumbani au kwenye makazi yake atakamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Jeshi la Polisi lingependa kutoa onyo kwa baadhi ya watu ambao hawana mamlaka ya kufanya hivyo waache tabia ya kwenda kwenye eneo ambalo lilitajwa kuwa huyo binti anaishi wakimtafuta yeye na familia yake ili wawahoji au kuwaona. Kufanya vitendo vya aina hiyo ni kuwatweza utu wao na kuwatonesha majeraha waliyonayo mioyoni mwao.
Imetolewa na:
David A. Misime - DCP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania