Jeshi la Polisi Wilaya ya Ulanga limeendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yake na wananchi kupitia programu ya “ONGEA NA KAMANDA”, iliyotekelezwa katika Kata ya Ketaketa na Kijiji cha Ketaketa, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro.
Programu hiyo imelenga kuwapa wananchi fursa ya kueleza kero na changamoto zinazowakabili, huku ikiimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali katika kudumisha amani na usalama wa jamii.
Katika mkutano huo, uliofanyika octoba mwaka huu 2026 wananchi walitoa pongezi kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ulanga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Deogratius Challe, pamoja na askari wake kwa juhudi zinazofanyika katika kuimarisha ulinzi na usalama, hususan katika kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Wananchi walieleza kuridhishwa na doria za mara kwa mara zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika maeneo yao, wakibainisha kuwa zimechangia kupunguza changamoto ya mifugo kuingia na kula mazao mashambani, pamoja na kuongeza hali ya usalama katika jamii.
Aidha, wananchi waliomba Jeshi la Polisi kuendelea na doria hizo na kuimarisha ushirikiano na wananchi pamoja na viongozi wa maeneo husika ili kuzuia migogoro, kulinda mali na kudumisha amani na mahusiano mema kati ya wakulima na wafugaji.
Programu hiyo ilishirikisha maafisa na askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wadau kutoka Serikali ya Kijiji, Ofisi ya Mtendaji wa Kata na Kijiji, elimu, kilimo na mifugo, Baraza la Ardhi la Kata na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Jeshi la Polisi linaendelea kuhimiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu na viashiria vya uvunjifu wa amani kwa wakati, kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, na kuwa sehemu ya kudumisha amani na usalama katika maeneo yao.