BANZA STONE 'ALIVYOMCHAMBA' MUUMIN NA ELIMU YA MJINGA.
_________________
Na Kado Cool
Wakati muziki wa dansi ukiwa umeshika chati katikati mwa miaka ya 2000, kulitokea vita kali ya maneno kati ya Wanamuziki nyota wawili, Prince Mwinjuma Muumini na mwanamuziki mwenye sauti tamu ya kuvutia Waziri Sonyo.
Chanzo cha vita hiyo iliyofikia hatua mbaya ni kitendo cha mwanamuziki Waziri Sonyo kujiengua ndani ya bendi maarufu ya Double M Sound wana 'Mshike Mshike' iliyokuwa ikiongozwa na Prince Mwinjuma Muumini 'Kocha wa dunia'.
Malumbano yao yalifikia hatua mbaya mpaka wanamuziki wote wawili kuanza kutuhumiana kujihusisha na vitendo vya Ushoga huku kila mmoja akimpiga dongo mwenzie kuwa na tabia hiyo ovu isiyofaa kwenye jamii.
Wakati Muumini akimpiga vijembe Waziri Sonyo kuwa ni shoga kutokana tabia za kupenda kusuka nywele, Sonyo naye alidai Muumini ndiye mwenye tabia hizo kwani alipokuwa jijini Mombasa nchini Kenya aliwahi kusikia akituhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo.
Hatua hiyo ilipelekea gazeti maarufu la Udaku la wakati huo liitwalo 'Ijumaa' kuingilia kati kuwapatanisha wanamuziki hao lakini kila mmoja aliendelea kumtuhumu mwenzie Ushoga, hivyo suluhu iliyoamuliwa wote wawili kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili kufanyiwa vipimo ili kuthibitisha ukweli huo dhidi yao.
Wakati hayo yakiendelea kutokea, aliyekuwa Mkurugenzi wa bendi ya TOT, Marehemu Kapteni John Damian Komba akautumia mwanya huo kuwapeleka wanamuziki wa bendi yake Chuo cha Sanaa Bagamoyo ili kusoma Kozi fupi ya muziki huo.
Hatua hiyo ya ghafla ilipelekea Waandishi wa habari kumuhoji Kapteni Komba, kwanini ameamua kuwapeleka wanamuziki wa bendi yake ya TOT kupata Kozi fupi ya muziki wakati huu na si wakati mwingine.?
Kapteni Komba aliwajibu waandishi kuwa hapendi wanamuziki wake waje wapate aibu inayowakumba sasa wanamuziki Sonyo na Muumini kwa sababu yote yanayowatokea sasa ni tabia ya kubweteka na kutoongeza elimu ya taaluma yao.
Lilikuwa ni jibu lililoonekana kumkera zaidi mwanamuziki Muumini, kwani kama ilivyo kawaida yake ya kutopenda kubaki kimya pale anapohisi kushambuliwa, akaamua kurusha kombola kwa Kapteni Komba kuhusu tuhuma za 'kubweteka' kimuziki.
Muumini alimshambulia Kapteni Komba na bendi yake ya TOT kuwa, kilichowapeleka TOT Bagamoyo si kujifunza muziki, bali kujifunza Ushirikina kwenye muziki, maelezo yaliyoonekana kuwastaajabisha wengi.
Akisisitiza maelezo hayo bila hofu, Muumin alisema kuwa Bagamoyo ni kwao na anazijua kona zote, hivyo tayari anayo taarifa ya wanamuziki hao kupiga kambi kwa Mganga fulani kwa miezi kadhaa ili kufundishwa mambo ya Ushirikina kupitia muziki.
Baada ya bendi ya TOT kumaliza Kozi yao fupi chuoni hapo na wanamuziki wote kuweza kutunukiwa vyeti, bendi hiyo ikaamua kuboresha jina lao kwa kuongeza neno 'Plus' mbele ya TOT na kuanza kutambulika rasmi kama TOT Plus badala ya TOT Band kama ilivyokuwa mwanzo.
Wakati Muumini akiendelea kutamba na vijembe vyake kwa bendi ya TOT Plus kuwa wameenda kujifunza uchawi badala ya muziki, Kiongozi wa TOT Plus, Jenerali Banza Stone 'Mwalimu wa Walimu' akaamua kumjibu Muumini kupitia wimbo badala kuongea na vyombo vya habari kama Muumini anavyofanya.
Banza akakaa chini na kuandika kibao cha 'Elimu ya Mjinga' huku akionekana kumpiga madongo kisawasawa Muumini ndani ya kibao hicho kuwa "ikiwa anaona elimu ni ghali, basi aendelee tu kujaribu ujinga wake wa kuitukana TOT" aone kama utamsaidia.
[emoji443][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445]
Ni usemi wa siku nyingi, mamaa..
Na leo hii nakubali miye, ooh ooh
Elimu ya Mjinga ni Majungu..
Elimu ya Mjinga ni Majungu...
Ni Bora ukose Mali, Upate Akili..
Kwani Elimu ni Bahari na Haina mwisho... (X2)
Majungu si Mtaji
Useme ufanye Utajirike..
Majungu si Biashara
Useme uuze Inunuliwe..
Ikiwa unaona elimu ni ghali
Basi jaribu, Ujinga aaah.. (X2)
Mjinga upenda Majivuno..
Upenda Majisifu..
Asichokijua.. Hujifanya anajua..
Mazuri ya kwake..
Mabaya ya wenzake..
Anaweza akateketeza...
Misingi na Malengo..
Ya Jamii... Yoyote eeeh..!!
[emoji443][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445][emoji445]
Lilikuwa ni shuti kali mno ambalo lilimshinda kabisa Prince Muumin Mwinjuma 'Mwana Buguza' na kuzama nyavuni, hivyo kumaliza kabisa vita vya maneno vilivyokuwa kati yake kupitia bendi anayoimiliki ya Double M Sound Wana 'Mshike Mshike' na TOT Plus ya Kamarade Banza Stone
'Elimu ya Mjinga' ikawa Hit Song bora kabisa mpaka sasa kupitia muziki wa dansi. Inaelezwa kuwa wimbo huu ndiyo wimbo bora kabisa wa muda wote wa mwanamuziki Banza Stone pamoja na kuwa na tungo nyingi mahiri.
Solo ya Elly Chinyama, mtoto wa kiongozi wa zamani "Mchumi" wa bendi ya Ochestra Maquis Original marehemu Chinyama Chiyaza (Chi-Chi) kwangu binafsi ndiyo solo Bora zaidi kupigwa naye katika nyimbo zake nyingi alizoshiriki.
Elliiiiiiii....
Chinyamaaaaa..
Le Side Babaaa....
Mwana Sinzaa... [emoji445][emoji445][emoji445]
Mfunulieeee..
Mfunulieeee..
Mfunulieeee.. Aone.!![emoji445][emoji445][emoji445]
Achana kabisa na hii kitu aisee.! [emoji4]
Endelea kupumzika kwa amani Jenerali Ramadhani Masanja Banza Stone, Mwalimu wa Walimu.
Mungu akupe umri mrefu na afya njema, Prince Muumin Mwinjuma Kocha wa Dunia. Hakika mlijua kuupaisha muziki wa dansi kupitia tungo zenu mahiri.
Acha tuendelee kutoa ushuhuda wa yale tuliyoyashuhudia kwa macho na masikio yetu enzi za muziki wa dansi ulipokuwa mahiri miaka ya 2000