BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS K. NYERERE ALIFANYA JITIHADA ANUAI ILI DR. SALIM AHMED SALIM AWE RAIS WA TANZANIA 1985 NA 1995 LAKINI AKAGONGA MWAMBA
-------------------------------------------------------------------
Mzee wa Atikali ✍️✍️✍️
Jumamosi, Oktoba 4, 2025
0754 744 557
"Ukienda huko duniani, hasa hizi nchi za kusini mwa Afrika, Watanzania wanaojulikana zaidi ni Mwalimu Julius Nyerere, Dr. Salim Ahmed Salim na Brigedia Jenerali Hashim Mbita. Hawa ndio watu walioitangaza sana Tanzania internationally. Kwa maoni yangu, aliyeijenga Tanzania nje -iwe UN au iwe OAU ni Dr. Salim. Hakuna Mtanzania anaemzidi. Mwalimu aliwahi kufanya jitihada kubwa ili Dr. Salim awe Rais wa Tanzania lakini ilishindikana. Kwa maoni yangu, Dr. Salim is the greatest President Tanzania never had".
Mhe JOSEPH SINDE WARIOBA, Septemba 30, 2025.
1.
Usuli
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina matukio mengi muhimu ya kisiasa na kihistoria ambayo
"Bongolanderz" wengi, hususan
Dot.com, hawayafahamu.
Hivyo basi, Jumamosi mujarab ya leo, baada ya kutumia hadubini yangu kuvinjari makabrasha yangu yenye thamani sawia na
Tanzanite, nimewiwa kuwahabarisheni jambo moja la kipekee. Jambo hilo ni jitihada anuai za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alizofanya mwaka 1985 na 1995, ili Mtanzania wa kipekee, Dr. Salim Ahmed Salim, awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Atikali" hii itaonesha, sako kwa bako, jinsi Baba wa Taifa alivyofanya jitihada kedekede kwa nyakati tofauti, ikiwemo kuwatumia viongozi wanaoheshimika nchini, ili kufanikisha Dr. Salim kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini akagonga mwamba.
2.
Rais Nyerere Amshawishi Dr. Salim Agombee Urais- 1985
Mwaka 1975, Mwalimu Nyerere, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza, alitangaza kuwa atang'atuka mwaka 1980. Hata hivyo, kutokana na Vita ya Kagera 1978/79, hali ya nchi kiuchumi ilikuwa mbaya sana hivyo akabatilisha uamuzi wake huo na akatoa uamuzi mpya kuwa atang'atuka mwaka 1985. Uamuzi huo aliutangaza Alhamis, Septemba 25, 1980, kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliomchagua kuwa mgombea pekee.
Viongozi wengi wakaanza kumshauri Mwalimu asitekeleze azma hiyo kasoro mmoja tu; Jenerali Mirisho Sarakikya, Mzalendo wa kwanza kuwa Mkuu wa Majeshi nchini, ambaye wakati huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.
Jana Ijumaa, Oktoba 3, 2025, Jenerali Sarakikya alinipigia simu akiwa mkoani kwake,
"Geneva ya Afrika", na kunimegea
ubuyu kuntu kuhusu ujasiri wake huo usio mfanowe:
"Mwaka 1982, Mhe Alex Ekwueme, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Nigeria, alifanya ziara ya kiserikali nchini. Enzi hizo mimi nilikuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria hivyo nikaja nae. Nilipokuwa hapa nchini niliona hali ya maisha imekuwa mbaya sana. Niliporudi Nigeria nikatafakari sana. Nikaamua kuja nchini bila kumwambia Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje. Nikapata "appointment" ya kumuona Rais Nyerere. Nikamueleza kuwa, kwa hali ilivyo, inabidi atekeleze uamuzi wake wa kung'atuka. Nikamwambia kuwa Mawaziri, Kamati Kuu, Jeshi, UWT nk watamshawishi sana abadili uamuzi wake lakini asiwasikilize, hata iweje ! Nikiwa CDF, mara nyingi nilikuwa naongea nae tukiwa wawili tu. Mwalimu alinishukuru sana kisha nikarejea Nigeria. Mwalimu, licha ya kushawishiwa sana, alishikilia msimamo wake. Mwaka 1984, Mwalimu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa OAU. Mwaka 1985 alipokuwa anamaliza muda wake akawaaga Marais wenzie Addis Ababa, Ethiopia na kuwaambia wampokee kwa mikono miwili Rais mpya wa Tanzania ajae. Mwishoni mwa mwaka huo 1985, Mabalozi wote tulienda Ikulu kumuaga Mwalimu. Tulimnunulia zawadi yeye na Mama Maria. Mwenyekiti wetu, Balozi Job Lusinde, alitoa hotuba kwa niaba yetu. Mwalimu alipohutubia alisema "Mabalozi wote mlikuwa mkiniomba sana nising'atuke kasoro mmoja tu, Sarakikya. Yeye tu ndiye aliyekuja na kunieleza kuwa nishikilie msimamo wangu na namshukuru sana".
Viongozi wengi wa nje, akiwemo Mhe Kenneth Kaunda, aliyekuwa Rais wa Zambia, pia walifanya juhudi kubwa kumshauri Mwalimu asing'atuke. Oktoba 1, 1985, Mhe Kaunda alizielezea, kwa weledi mkubwa, juhudi hizo :
"Many Heads of State and Government as well as close colleagues and friends- I am one of them- tried to dissuade President Nyerere from retiring, fearing the irreplaceable gap he would leave behind both nationally and internationally would be difficult to fill. But Mwalimu had made up his mind and there was no going back".
Kwavile Rais Nyerere aliishafanya uamuzi na alikuwa hasikii la mwadhini wala mnadi swala, kizungumkuti kikubwa kikawa ni suala mtambuka la nani awe Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mtazamo wa Rais Nyerere ulikuwa ni kwamba kwavile nchi hii ni ya Muungano na kwavile Rais wa Awamu ya kwanza, ambaye ni yeye, alitoka Tanzania Bara, ingekuwa vizuri Rais wa Awamu ya Pili atoke Zanzibar.
Mtu wa kwanza aliyemfikiria alikuwa Mhe Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Zanzibar. Hata hivyo, Mwalimu aliona kwamba kwavile mwaka 1984 hali ya hewa ilikuwa imechafuka sana huko Zanzibar na Rais Mwinyi alikuwa amefanya kazi nzuri sana kuisafisha na pia hali ya kiuchumi ilikuwa imeimarika sana, ingekuwa busara akaachwa aendelee kuwa Rais wa Zanzibar.
Mwalimu Nyerere akaona mtu anaefaa na mwenye vigezo vyote ni Dr. Salim ambaye wakati huo alikuwa Waziri Mkuu.
Rais Nyerere akamwita Dr. Salim nyumbani kwake Msasani na kumweleza jambo hilo. Dr. Salim akakataa katakata na kuomba kikombe hicho kimpitie pembeni. Dr. Salim aliona kuwa ameishi sana nje ya nchi na akashauri nafasi hiyo apewe mwingine (Dr. Salim alienda nje kama Balozi mwaka 1964 na akarejea mwaka 1980).
Kwavile Dr. Salim alikuwa ameshikilia msimamo wake, Mwalimu alimruhusu aondoke Msasani.
3.
Rais Nyerere Amwita Tena Dr. Salim na Kumshawishi Agombee
Rais Nyerere hakukata tamaa. Baada ya mwezi, akamwita tena Dr. Salim. Mwalimu alitumia kila aina ya ushawishi. Akamwambia uongozi ni jumuishi hivyo atakuwa na wenzake, hatimaye Dr. Salim akakubali.
Mzee Mwinyi alikuwa sahihi alipoandika kwenye ukurasa wa 146 wa Tawasifu yake,
"Safari ya Maisha yangu" :
"Si siri hata kidogo kuwa 1985 Mwalimu Nyerere alikuwa amemfikiria Dr. Salim Ahmed Salim kuwa mrithi wake kuongoza Taifa".
Ijumaa, Agosti 2, 1985, Rais Nyerere alipokuwa anafungua mkutano wa chama kwenye JWTZ aliweka msimamo wake :
"Ni kweli ninaye mtu ambaye nadhani anafaa, lakini wenzangu kwenye CC & NEC wanaweza kuwa na maoni tofauti".
Kwa mujibu wa utaratibu wa enzi zile, Mwenyekiti ndiye alikuwa anapendekeza majina. Kamati Kuu ikakutana Ikulu, Magogoni. Mwalimu Nyerere akawataka wajumbe wapendekeze sifa za Rais ajae. Wakapendekeza sifa takriban 30 na kisha Mwalimu Nyerere akataja majina 3, Mzee Mwinyi, Dr. Salim na Mhe Kawawa. Wajumbe toka Zanzibar wakamkataa katakata Dr. Salim na kusema hawawezi kuongozwa na
"Hizbu". Kwa upeo wao walihisi kuwa kwavile Dr Salim ni mwarabu na waarabu wengi waliuawa wakati wa Mapinduzi ya 1964 hivyo akiwa Rais atalipiza kisasi. Kama vile hiyo haitoshi, kwavile Dr. Salim aliwahi kuwa mwanachama wa
Umma party wakamhusisha, bila ushahidi, na mauaji ya Rais Abeid Aman Karume Aprili 7, 1972 na mwisho wakadai kuwa Dr. Salim sio mwenzao kwani huwa hatamki kauli ya
"Mapinduzi Daima".
Mhe Kawawa aliamua kujitoa ili kupisha damu mpya. Mwalimu Nyerere akasema wawili waliobaki wajadiliwe kwa kuanza na mwandamizi, Mhe Mwinyi. Wajumbe waliona Mwinyi anatosha hivyo Dr. Salim hakujadiliwa.
Mhe Joseph Sinde Warioba alitambaa mulemule Septemba 30, 2025 :
"Dr. Salim alikuwa ndiye chaguo la Mwalimu Nyerere lakini ndoto hiyo ikazimwa na Wazanzibar wenzie waliyesema huyu ni "Hizbu !".
Al marhum Seif Sharrif Hamad naye alisimulia hivyohivyo kwenye kitabu
"Race, Revolution and the struggle for Human rights in Zanzibar: The memoirs of Ali Muhsin & Seif Sharrif Hamad":
"Mwalimu thought Dr. Salim was the best candidate. Dr. Salim told me that Mwalimu told him openly "I am leaving, I think you are the proper person to succeed me".
Rais wa awamu ya tatu, Mhe Ben Mkapa, ameandika, kwenye Tawasifu yake,
"My Life, My Purpose", kuwa chaguo la Rais Nyerere lilikuwa ni Dr. Salim na akaeleza kuwa hata hotuba yake ilikuwa na jina hilo ila baada ya jina la Mhe Mwinyi kupitishwa ikabidi alibadili.
Prof. Shivji nae amesimulia hivyo hivyo kwenye kitabu chake
"A Biography of Julius Nyerere" :
"There was no doubt that Dr. Salim was Mwalimu's preferred candidate to succeed him. Dr. Salim fell victim to some parochial elements in the Central Committee who successfully manoeuvred against Dr. Salim's candidature".
Hivyo, jitihada za Mwalimu Nyerere kutaka Dr. Salim kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985 zikagonga mwamba.
Afrika ilimuhitaji Dr. Salim hivyo mwaka 1989 akachaguliwa, kwa kishindo, kuwa Katibu Mkuu wa OAU. Mwandishi hodari, Jasper "Kido" Sabuni, alielezea kwa umahiri mkubwa Septemba 2, 2024 :
"The leaders of liberation struggles- particularly then- Zimbabwe President Robert Mugabe, pushed for Dr. Salim candidacy and for the Tanzania government to release him and to contest the position of the Secretary General of the OAU in 1989. Dr. Salim won the respective position and went ahead to serve at the OAU leaving a massive imprint on the African region".
Dr. Salim, kama ilivyo kawaida yake, akaweka rekodi. Akawa ndiye Mwafrika wa kwanza kuhudumu kama Katibu Mkuu wa OAU kwa muda mrefu zaidi, mihula mitatu.
4.
Rais Nyerere Amuibukia Dr. Salim Masaki- 1995
Baba wa Taifa hakuwa na simile kwenye masuala nyeti ya Kitaifa. Mojawapo ya masuala nyeti ni kumpata Mtanzania afaaye kuwa Rais. Mwalimu aliona kuwa sio kila
"Tom, Dick & Harry aweza kuwa Rais ndio maana mwaka 1995 aliwatimua viongozi wa NCCR walipoenda Msasani na mgombea Urais wao, Mhe Augustine Mrema, ili kupata
"endorsement" yake ambapo, bila kupepesa macho, akawajibu
"I cannot go to sleep in Butiama and let my country go to the dogs".
Mwaka huo wa 1995, Baba wa Taifa alimfuata Dr. Salim nyumbani kwake Masaki. Wakati huo, Dr. Salim, aliyekuwa Katibu Mkuu wa OAU, alikuwa likizo. Mwalimu alijitahidi sana kumshawishi Dr. Salim agombee Urais wa Tanzania lakini Dr. Salim akakataa.
5.
Baba wa Taifa Amwambia Mhe RC Dotopile kuwa Amtaka Dr. Salim
Miongo 3 iliyopita, nilikuwa mjumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani nchini. Mwenyekiti wa Kamati hii alikuwa RC wa Dar Es Salaam, Mhe Ditopile Mzuzuri "Mtoto wa mjini".
Siku moja, Mhe Ditopile aliitisha kikao. Mimi nikawa mtu wa kwanza kufika, nikaingia ofisini kwake. Mhe Ditopile alikuwa mtu wa
ubuyu sana. Siku hiyo alinipa
ubuyu niukumbukao hadi leo :
"Mwaka huu kuna kinyang'anyiro kikubwa cha Urais. Baba wa Taifa akija Dar es Salaam hupenda kuniita na huniambia "wewe ukiwa Mkuu wa Mkoa huu, lazma unaskia mengi". Je, wananchi wanamtaka nani kuwa Rais"? Mimi nikamueleza Mwalimu kuwa ni ngumu kujua kwani kila mtu anampenda mtu wake. Mwalimu akasema "mimi namfikiria Dr. Salim lakini haonekani kuitaka nafasi hiyo".
6.
Baba wa Taifa Akutana na Dr. Salim USA na kumshawishi Agombee
Baba wa Taifa alisafiri kwenda Marekani na akiwa huko alibahatika kukutana na Dr. Salim aliyekwenda huko kuhudhuria mkutano wa UN kwa niaba ya OAU. Mwalimu alitumia fursa hiyo adimu kumshawishi Dr. Salim agombee Urais lakini Dr. Salim akakataa. Dr. Salim alimueleza Mwalimu, kwa utuo, kuwa awamu yake ya 3 ya Ukatibu Mkuu wa OAU ilitokana na kampeni kubwa iliyofanywa na
"French speaking countries". Kikawaida, nchi hizi hupenda Katibu Mkuu atoke kwenye moja ya nchi hizo lakini kutokana na uwezo mkubwa uliooneshwa na Dr. Salim, ndio maana walitaka aendelee. Hivyo, Dr. Salim akasema haitakuwa busara kuwatelekeza na akashauri atafutwe mwingine.
7.
Baba wa Taifa Ampa Jukumu Mhe Warioba kumshawishi Dr. Salim
Baba wa Taifa, aliporejea nchini, alimwita Mhe Joseph Sinde Warioba kwani alijua ni rafiki mkubwa wa Dr. Salim
"Mzigo Mzito Mtwishe Mnyamwezi". Mwalimu akamsimulia Mhe Warioba mazungumzo yake na Dr. Salim Marekani na akamtaka atafiti utaratibu wa OAU kama Dr. Salim angeweza kuchukua
"Leave without pay" ahudhurie kwenye mchakato wa Urais; akiteuliwa abaki, asipoteuliwa arudi OAU. Mwalimu alitoa mfano wa 1983 ambaoo Rais Shehu Shagari wa Nigeria alimchukua Mhe Chifu Emeka Anyaoku aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola toka 1977 na kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Rais Shagari alipopinduliwa mwishoni mwa 1983, huyo Chifu Anyeoka akarudi kuendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.
Mhe Warioba akafanya utafiti wa kutosha kisha akaenda kumshawishi Dr Salim. Hata hivyo, Mhe Warioba akagonga mwamba na akamjuza Mwalimu kuwa Dr. Salim amekataa kabisa.
Mhe Mkapa ameeleza kwenye Tawasifu yake kuwa alipoenda Butiama kumweleza Baba wa Taifa kuhusu azma yake ya kutaka kugombea Urais, Mwalimu alimwambia kuwa chaguo lake ni Dr. Salim. Hata hivyo, Mwalimu alimwambia kuwa amefanya jitihada mbalimbali kumshawishi Dr Salim arudi nchini kugombea lakini anasitasita.
Mwalimu akamalizia kwa kumwambia kuwa iwapo Dr Salim atashikilia msimamo wake, basi yeye Mwalimu atamuunga mkono Mhe Mkapa.
8.
Baba wa Taifa Ampa Jukumu Mhe JK kumshawishi Dr Salim
Baba wa Taifa alidhamiria kwelikweli kuhakikisha Dr. Salim anarudi kuja kugombea. Hivyo, hakukata tamaa.
Mwalimu alipobaini kuwa Dr Salim ameenda Nairobi, Kenya kwenye mkutano, akamtuma Mhe Jakaya Kikwete, aliyekuwa Waziri wa Fedha, ili aende akamshawishi aje kugombea. Mhe Kikwete akaenda. Hii ni kwa mujibu ya maelezo ya Mhe Kikwete aliyoyasimulia Septemba 20, 2020.
Dr. Salim alishikilia msimamo wake hivyo Mhe Kikwete akarudi na kumtaarifu Mwalimu Nyerere kuhusu uamuzi huo wa Dr Salim usioteteleka.
Hatimaye, Baba wa Taifa akaona hamna namna kwani jitihada zake zote zilikuwa zimekwama. Hivyo, akaamua kumuunga mkono Mhe Mkapa na akamfanyia kampeni nchi nzima hadi akafanikiwa kuwa Rais wa Awamu ya Tatu.
9.
Dr. Salim ni Mtanzania wa kipekee
Dr. Salim Ahmed Salim ni Mtanzania wa kipekee. Ni wa kipekee kwelikweli.
Baba wa Taifa na Dr Salim walionana kwa mara ya kwanza mwaka 1959 Dr. Salim akiwa kijana mdogo wa miaka 17 tu. Dr. Salim aliwahi kusimulia :
"I met Mwalimu Nyerere for the first time in 1959 at Mnazi mmoja, Zanzibar when I was 17. ".
Wakati huo, Dr Salim alikuwa Makamu wa Rais wa chama cha wanafunzi (AZSO) :
"At the young age of just 17, I was the First Vice president of AZSO. Also, I was Deputy Secretary of 9 parties, the chairman was Mzee Abeid Aman Karume".
Rais Nyerere alimuamini sana Dr Salim na kumpa vyeo vikubwa baada ya Muungano.
Mwaka 1964, Rais Nyerere alimteua Dr Salim kuwa Balozi wetu nchini Masri akiwa kijana wa miaka 22 tu. Awali, Februari 15, 1964, Rais Abeid Aman Karume alikuwa amemteua Dr. Salim kuwa Balozi wa Zanzibar nchini Masri na akampa Hati za utambulisho za Kiswahili. Dr. Salim akaenda Masri lakini kabla hajawasilisha Hati hizo, Tanganyika na Zanzibar zikaungana Aprili 26, 1964. Rais Nyerere akamteua Dr Salim na kumpa Hati za Kiingereza ambazo ndizo aliziwasilisha. Dr. Salim akaweka rekodi ya kuwa Balozi mdogo zaidi barani Afrika.
Hakuna Mtanzania mwingine yeyote aliyeivunja rekodi hiyo kuntu ya Dr. Salim kuwa Balozi katika umri mdogo hadi leo. Mwaka 1964, Dr. Salim si tu alikuwa mdogo bali pia alikuwa ndiye Balozi pekee ambaye hakuwa na ujuzi wowote wa mambo ya Ubalozi:
"I was the only ambassador who wasn't trained in any way in this role. All my colleagues had received training and attachments".
Dr. Salim, baada ya kupewa jukumu hilo zito la Ubalozi, ikabidi amuoe laazizi wake, Bi Amne Ali Rifai. Harusi ikafanyika Aprili 17, 1964 kwani Dr. Salim hakutaka kuwa Balozi- Msela.
Dr Salim, licha ya udogo wake na kutokuwa na uzoefu, alifanya kazi nzuri kwenye kituo hicho cha Cairo ambacho kilikuwa moja ya vituo muhimu :
Hata
Al marhum Seif Sharrif Hamad, kiongozi wa zamani wa upinzani, aliwahi kukiri ukweli huo kwenye kitabu chake kilichotajwa hapo juu :
"President Nyerere was very impressed by how seriously Salim took his responsibilities in Cairo. Although very young, Salim was one of our best ambassadors. He was hardworking and incorruptible".
Licha ya umri wake mdogo, Rais Nyerere alimpeleka Dr. Salim, kutokana na umahiri wake, kuwa Balozi wa Tanzania India na kisha China, nchi mbili zilizokuwa na umuhimu mkubwa kwetu.
Mwaka 1970, Rais Nyerere alimteua Dr Salim kuwa Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa. Dr. Salim akawasilisha Hati za Utambulisho kwa Mhe U Thant, aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN. Akiwa na miaka 28 tu, Dr. Salim akawa ndiye Balozi mdogo kuliko wote toka Afrika. Nimebahatika kuona picha mjongeo mbili za Dr. Salim akiwa UN enzi hizo- alikuwa machachari sana. Mnooo !
Oktoba 25, 1971, Dr. Salim alikonga nyoyo za nchi nyingi zinazoendelea kwa kufanikisha kuifanya China kuwa moja ya Mataifa 5 yenye kura za
"Veto" kupitia
UNGA Resolution 2758. Septemba 30, 2019, Rais Xi Jinping alimtunuku Dr. Salim
"Friendship Medal", ambayo ni medali ya juu zaidi nchini humo iliyopokelewa na mwanae, Maryam, kutokana na mchango wake usio mfanowe kwa Taifa hilo mwaka 1971.
Dr. Salim aliandika historia nyingine kuntu mwaka 1976. Januari 10, 1976, akiwa kijana mdogo tu wa miaka 33, alichaguliwa kuwa Rais wa UNSC na kuweka rekodi ya kuwa Rais mdogo kuwahi kushika cheo hicho kikubwa UN. Dr. Salim alikuwa akiheshimika mno hadi Balozi mmoja akasema kuwa, enzi hizo, hakuna Mwafrika duniani ambaye alikuwa maarufu zaidi ya Dr. Salim. Enzi hizo, Dr. Salim aliyashupalia na kuyasimamia vilivyo masuala ya ukombozi wa nchi zilizokuwa zikitawaliwa.
Nyota ya Dr. Salim iliendelea kung'aa vilivyo kimataifa. Septemba 18, 1979, Dr. Salim akaweka rekodi nyingine mujarab baada ya kuteuliwa kuwa Rais wa UNGA akiwa na miaka 37 tu. Akawa ndiye Rais kijana zaidi kuwahi kuchaguliwa kushika kiti hicho.
Mwaka 1980, Rais Nyerere alimteua Dr. Salim kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Mwaka 1981, Dr. Salim akagombea kuwa Katibu Mkuu wa UN. Mimi, nikiwa mtoto mdogo tu, nilikuwa nikifuatilia upigaji kura hadi usiku wa maanani kupitia BBC na asubuhi naenda shule macho yakiwa mekuuuuundu! Marehemu baba yangu akawa akinitania kwa kuniita
"Dr. Salim" ! Dr. Salim
alimpelekea moto sana Dr. Kurt Waldheim na kuonekana angeshinda lakini Marekani ikamuwekea Veto. Mchuano ulienda raundi 16. Marekani ilikuwa ikimuwekea veto Dr. Salim na China ikimuwekea veto Dr. Waldheim. Ikabidi atafutwe mtu mwingine ndipo akapatikana Javier Perez de Cuellar.
Dr. Salim, akiwa UN miaka ya 1970s, aliliheshimisha sana Taifa letu, kama alivyowahi kutiririka :
"In the 1970s, I was the Tanzania Ambassador to the UN and Hon. John Malecela was our foreign minister and we were under President Nyerere. I am proud to say that we did an excellent job internationally and brought great repute to our nation".
Baba wa Taifa alipohutubia Agosti 31, 1995 viwanja vya Jangwani kwenye uzinduzi wa kampeni za Mhe Ben Mkapa, aliyekuwa mgombea wa CCM, alilielezea hilo ingawa alichekesha sana umati aliponena :
"Kwenye miaka ya 70, mimi nilipokuwa Rais na Dr Salim alipokuwa Balozi wetu kwenye Umoja wa Mataifa, Tanzania ilikuwa ikiheshimika sana. Mjumbe wa Tanzania alipokuwa akitoa hotuba, kila nchi ilisikiliza kwa makini kutaka kujua msimamo wa Tanzania. Lakini naambiwa sasa hali ni tofauti; Tanzania ikiongea ndio muda wajumbe wa nchi nyingine hupata fursa ya kwenda nje kuvuta sigara !. Nataka hali hiyo ibadilike na hakuna wa kuibadilisha zaidi ya Ben".
Rais Nyerere alipomteua Dr. Salim kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dr. Salim alifanya kazi kubwa na kuheshimika sana. Ndio maana, Mhe Richard Viets, aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania (1978-1981),
alimfagilia Dr Salim:
"In my final months in Tanzania, the Foreign minister was a gentleman named Dr. Salim Ahmed Salim. I found him to be a very, very bright and interesting man".
Baada ya Mhe Edward Sokoine kufariki Aprili 12, 1984 kwa ajali, Rais Nyerere alimwita Dr Salim Msasani Aprili 24, 1984. Dr. Salim aliwahi kusimulia ;
"On April 24, 1984, President Nyerere summoned me. So, I went to Msasani. He told me that he had planned to appoint me new Prime Minister. With great humility, I politely refused. However, Mwalimu was having none of it. He didn't take no for an answer. He insisted and appointed me Prime Minister the same day. My fellow ministers teased me that I was a TX- PM because I had lived more outside the country than inside!".
Dr. Salim, kama kawaida yake, alifanya kazi nzuri na ya kukumbukwa akiwa Waziri Mkuu.
"Watoto wa 2,000" hawajui kuwa hapa nchini, Dr. Salim ndiye muasisi wa nguo za Mitumba "Sagula-Sagula"
, "Za Leo-Leo". Je, ilikuwaje? Dr. Salim aliwahi kuhabarisha :
"As Prime Minister, I once went to Lindi and Mtwara. In public rallies, I was shocked that people were wearing tree barks. I successfully convinced President Nyerere to allow importation of second hand clothes "Mitumba" and the rest is history".
Machi 11, 2021, rafiki yangu, Prof. Chris Maina Peter, alinielezea kwa umahiri mkubwa, kupitia
"WhatsApp", jinsi Dr. Salim alivyoutendea haki uwaziri mkuu :
"Many politicians were very worried when Dr. Salim was appointed Prime minister. They saw him as a flamboyant ambassador who was not accustomed to our Tanzanian environment. But Dr. Salim's work ethic left them dumb struck! Dr. Salim was never in Dar es Salaam. He spent most of his time up country. He wore "Khaki" apparel and "Raba mtoni" and spent the whole day in the farms, building schools and roads in the remotest villages never reached by any leader. Eventually, all his detractors came to respect him as he was more than the "Champagne ambassador" they had initially thought him to be".
Novemba 5, 1985, Rais Nyerere alipokuwa aking'atuka, alimtunuku Dr. Salim Tuzo maalum ya
"The Order of the United Republic of Tanzania" kutokana na mchango wake mkubwa kwa Taifa letu.
Hiyo si tuzo pekee kwa Dr. Salim. La hasha. Alizipata nyingi sana mf Desemba 7, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alimkabidhi Dr. Salim
Tuzo ya Heshima ya Utatuzi wa Migogoro iliyotolewa na Taasisi ya Kemel Butros Ghali kuenzi utumishi wake ulioacha alama kama Katibu Mkuu wa OAU/A toka 1989 hadi 2001. Hiyo ilikuwa ni heshima kubwa sana kwa Dr. Salim, Rais Samia na Tanzania.
Aidha, Septemba 30, 2023, Rais Samia
alimfagilia vilivyo Dr. Salim:
"Dr. Salim aliliwakilisha vizuri sana Taifa letu kwenye nchi na majukwaa aliyohudumu. Kwakuwa Dr. Salim ni Mwanadiplomasia mahiri sana, chuo cha Diplomasia sasa rasmi kitaitwa Dr. Salim Ahmed Salim Center for Foreign Relations".
10.
Tamati
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alimpenda sana Dr Salim Ahmed Salim na akafanya jitihada kubwa ili awe Rais mwaka 1985 na 1995 lakini akagonga mwamba.
11.
Tafakuri Jadidi:
Wanazuoni na
"Bongolanderz" wote wakiwemo Diaspora, ni muda wenu sasa kujadili :
11.1 Je, ni jambo zuri kwa Baba wa Taifa au Rais amalizae muda wake kumshawishi Mtanzania mmoja agombee Urais ? Je, huu ni utamaduni mzuri ? Ninachomaanisha hapa ni kuwa mf Mhe Rais Samia akimaliza ngwe yake 2030, itakuwa jambo zuri akimwendea mf RC Anthony Mtaka au Mhe Waziri George Simbachawene na kumshawishi agombee Urais ?
11.2 Je, ni kweli kuwa
"Dr. Salim is the greatest President Tanzania never had"?
12.3 Je,
"Bongolanderz" kwanini tunaacha
kujimwambafy kwa kusema
"Dr. Salim Ahmed Salim ni wetu Watanzania na tunatamba naye" ?
Mwandishi Sabuni alinikosha mno alipoandika Septemba 2, 2024 :
"Africa may have been blessed and enriched with many things but I would presume that one of the continent's proudest and most valuable blessings is the pure, genuine and remarkable soul and gem, in the name of Dr. Salim Ahmed Salim- an incredible treasure born in the islands of Zanzibar and indeed a proud son of Africa. Just how I admired Zinedine Zidane Zizzou's eloquence, artistry and touch of finesse on the football pitch, I developed similar, if not extraordinary admiration for Dr. Salim's brilliance, charisma, and silky and unreal touches within the political and diplomatic fields. Salim is, to me, the Zizzou of diplomacy, and Zizzou is the Salim of football ".