SIMULIZI FUPI YA ZIARA YA MFALME WA POP DUNIANI MICHAEL JACKSON NCHINI NA ALIPOTEMBELEA SINZA MWAKA 1992
Februari 18, 1992, wananchi wa kitongoji cha Sinza, jijini Dar es Salaam, walipata mgeni ambaye wengi walimzoea kumuona kwenye televisheni: Michael Jackson, Mfalme wa Pop duniani.
Alitembelea shule ya watoto wenye mahitaji maalumu, akafurahi nao na walezi wao, kisha akatoka kuwasalimia wananchi waliofurika hapo kumwona.
Michael aliwasili Tanzania kwa ndege yake binafsi akitokea Ivory Coast, katika ziara iliyopangwa kuhusisha nchi 11 za Afrika akiwa Balozi wa Umoja wa Mataifa. Alipokelewa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, marehemu Hassan Diria, na alikutana na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Akiwa amefikia Hoteli ya Kilimanjaro pamoja na ujumbe wake wa watu 90, alikuwa na matembezi mengine yaliyomwacha mwenyeji mmoja mdomo wazi. Usiku wa manane, Michael alikwenda Empire Cinema, duka la kukodisha mikanda ya video. Hakutosheka kuchungulia dirishani; aliingia ndani, akachagua mikanda kadhaa ya vikatuni na kuondoka.
Muuzaji, kwa mshangao wa kumwona nyota huyo dukani kwake, alisahau hata kudai malipo, kwa butwaa ya kukutana uso kwa uso na Mfalme wa Pop.
Hata hivyo, maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje alioongozana nao, wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Itifaki, Cisco Mtiro, walilipa kwa niaba yake.
Februari 19, Michael aliondoka kwenda London, akikatisha ziara badala ya kuelekea Kenya kama ilivyopangwa.
View attachment 3702450View attachment 3702452View attachment 3702451