LEO Dec 17ni miaka 34 sasa imepita tangu Afrika Mashariki ilipompoteza mwimbaji mahiri kijana, aliyeleta mapinduzi makubwa nchini kwenye uimbaji, NICO ZENGEKALA!! Alikuwa ni mwimbaji mlemavu wa macho. Alikuwa na sauti tamu, nyororo, kali, ambayo alikuwa na uwezo wa kuitetemesha na kusikika kama maporomoko ya maji, wakati mwingine akiishusha sauti kama mtu anayeweseka hivi!!
Alifariki Alfariji saa 11Desemba 17, 1987, nyumbani kwake ghafla Mtaa wa Sikukuu, Dar es Salaam kwa kile madaktari walichosema kuwa ni ugonjwa wa kifafa!! Alifariki akiwa na umri kati ya miaka 20 hadi 24!! Wakati Msondo wakisema alifariki akiwa na miaka 24 tu, lakini kwa mujibu wa mwanamuziki Said Makelele ni kwamba ilibidi wadanganye ni Mtanzania ili aruhusiwe kuvuka mpaka wa Tanzania na Kenya, kwani wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17, hivyo asingeweza kuruhusiwa kuvuka mkapa!! Wakadai ni Mtanzania wa Dodoma na wao ni wanamuziki wanaorejea nyumbani Tanzania!! kwa wito wa Mkuu wa mkoa wa Morogoro Nicodemus Banduka!! Inawezekana Msondo walimpandisha umri ili aweze kuajiriwa na Jumuiya ya Wafanyakazi wa Tanzania JUWATA, kwani wasingeweza kumuajiri mtoto. Inawezekana pia waliogopa kusema ana miaka 18 au 20 kwa sababu wangeweza kuwa na wasiwasi Nico raia wa Kenya, kabila la Wataita nchini Kenya. Alizaliwa katika kijiji cha Wundayi eneo la Mwatate karibu na mji wa Voi, Mombasa nchini Kenya. Alichukuliwa na kuletwa nchini na mabaki wa wanamuziki wa Super Volcano ya Mbaraka Mwinshehe, Simba Wanyika, Les Wanyika, Wanyika Stars, Super Wanyika na Jobiso, ambao walimuona akiimba kwenye bendi moja ya Wataita wenzake Nairobi. Alipokuja nchini alitamba na vibao ya Jackie, Shemango, Mwalimu Nyerere, Suzzy, Bwana Salimu na vingine vingi kwenye bendi ya Les Cubano ambayo hapa nchini hakukaa nayo zaidi ya miaka miwili. Bendi nyingi zilimtaka ikiwemo Maquiz, lakini Msondo ilishinda vita, na kuibuka na vibaoa kama Solemba, akiimba pia nyimbo za Kaka Mahmood, Bahati, Prisila, Kambarage Nyerere. Alijiunga na Msondo mwaka 1985 na kufariki mwaka 1987, akazikwa Mwatate Mombasa nchini Kenya
Ni mwanamuziki ambao alidumu kwa muda mfupi nchini, lakini sauti na uimbaji wake, ulitishia ustaa wa wanamuziki wengi si kwenye bendi ya Msondo tu, bali hata Tanzania nzima. Hakuwa staa kwao Kenya, lakini nyota ilimuwakia nchini na hata mwili yake uliposafirishwa, masafara na heshima kubwa msafara mkubwa ya magari ya serikali ya Tanzania, kama vile anayekwenda kuzikwa ni kiongozi mkubwa wa kitaifa, kutoka kwa Juwata Makao Makuu, Chamudata, uliwashangaza wengi na kuwaliza zaidi wazazi na ndugu zake, kwani aliondoka wa kawaida, lakini maiti yake imerudishwa nyumbani kama shujaa. Hawakuamini!!