Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Kutoka Kushoto: Sheikh Suleiman Takadir, Mbutta Milando, JohnRupia na Julius Nyerere Hao Waliowazunguka na Silaha za Jadi ni Bantu Group Kundi la Vijana wa TANU lililokuwa linatoa Ulinzi kwa Viongozi wa TANU. Picha Hii Ilipigwa Mwaka wa 1955.
Sheikh Suleiman Takadir alikuwa nani na nini ulikuwa umaarufu wake? Sheikh Suleiman Takadir kwanza alikuwa ''alim," mwanazuoni kisha alikuwa Mwenyekiti muasisi wa Baraza la Wazee wa TANU kuanzia TANU ilipoundwa mwaka 1954 hadi "alipotoswa" mwaka 1958 kwa kosa la "kuchanganya dini na siasa.'' Sheikh Takadiri alishiriki vilivyo ndani ya Baraza la Wazee wa TANU katika kutayarisha safari ya Nyerere kwenda UNO mwaka 1955. Wapenzi wake katika harakati za kupigania uhuru walimpachika jina la utani wakimwita "Makarios," wakimlinganisha na Askofu Makarios wa Cyprus na Ugiriki aliyekuwa anapambana na ukoloni wa Waingereza wakati yeye alipokuwa anapambana na Waingereza katika ardhi ya Tanganyika. Sasa kwa kuwa Suleiman Takadir alikuwa sheikh na mpambanaji ndipo walimpa jina hilo la "Makarios" na kwa hakika jina hili lilimkaa, likamwenea vyema na yeye akalipenda.
Baraza la Wazee wa TANU
Sheikh Suleiman Takadir wa Pili Chini Kulia, Wa Pili Waliosimama Dossa Aziz,
Wa Sita Julius Nyerere, Wa Saba John Rupia, Wa Tisa Said Chamwenyewe,
Anaefuatia Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate
Mikutano ya mwanzo ya TANU ilikuwa ikifanyika Mnazi Mmoja mbele ya baadae ilipojengwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Wakati ule pale palikuwa hakuna jengo lolote, palikuwa na kiwanja kitupu na ardhi ile ilikuwa mali ya Mzee John Rupia Makamu wa Rais wa TANU. Kiwanja hiki baaadae Mzee Rupia aliwapa TANU na TANU wakaanzisha Chuo Kikuu pale mara baada ya uhuru. Mikutano ya kwanza ya TANU ikifanyika pale Mnazi Mmoja na kabla Nyerere hajapanda juu kwenye jukwaa kuzungumza na wananchi alikuwa kwanza anatangulia Sheikh Suleiman Takadir kusawazisha uwanja na kuwaweka wananchi tayari kumsikiliza kiongozi wao. Kama alivyokuwa Nyerere, Sheikh Suleiman Takadiri alikuwa na kipaji cha kuongea. Leo hii huenda baadhi ya wasomaji wangu wasiamini lakini ukweli ni kuwa Sheikh Suleiman Takadir alikuwa kabla hajazungumza lolote alikuwa akipiga "fatha," wananchi wakaitika na kwa umoja wao wakasoma, "Surat Fatha," sura ya ufunguzi katika Qur'an Tukufu, kisha Sheikh Takadir akaomba dua na wananchi wakawa wanaitika kwa pamoja, "Amin," Amin," "Amin." Baada ya hapo ndipo atapanda Nyerere na kuanza kuhutubia. (Picha za mwanzo za mikutano hii zipo na zilipigwa na Mzee Shebe ambae katika miaka ile ya 1950 alikuwa na studio yake Mtaa wa Livingstone na Kipata. Picha hizi baadhi nimepata kuziona. Mzee Shebe ndiye alinipiga picha yangu ya kwaza nikiwa na umri wa mwaka mmoja au miwili hivi na picha hii ninayo hadi hii leo. Inaaminika Mzee Shebe ndiye mpiga picha wa kwanza wa TANU na Nyerere).
Mwandishi Akiwa na Mwaka Mmoja Au Miwili Picha Aliyopigwa na Mzee Shebe
1952/53 Kwenye Studio Yake Mtaa wa Livingstone na Kipata
Nyerere Akihutubia Mkutano wa TANU Siku za Mwanzo
Huyu ndiye Sheikh Suleiman Takadir na huyu ndiye Nyerere kama alivyokuja kutambulishwa kwa watu wa Dar es Salaam na Sheikh Suleiman Takadir kwa mara ya kwanza mwaka wa 1954.Kabla ya hapo Nyerere alikuwa akijulikana na watu wachache katika TAA. Sheikh Takadir alimpenda sana Nyerere kiasi kuwa mwaka 1957 katika hotuba aliyotoa katika tafrija moja ya taarab Mtaa wa Mvita, alimwita Nyerere, "Mtume wa Afrika," aliyetumwa na Mungu kuwaokoa Waafrika. Maneno yale ya Sheikh Suleiman Takadir alikuwa kama anamtabiria Nyerere makubwa katika mustabali wa Afrika, kwani miaka mingi baadae Nyerere alikuja kusimama mstari wa mbele katika kuikomboa Afrika kutoka makucha ya wakoloni. Nyerere akawa hapungui nyumbani kwa Sheikh Takadir Mtaa wa Swahili. Nyumba hii iko jirani na kilabu ya mpira ya Pan Africa. Kutembelewa na Nyerere pale nyumbani kwake ikapelekea baba mwenye nyumba, Jumbe bin Jumaa wa Digosi amuhamishe nyumba Sheikh Takadir asije kumponza kwa kwani Nyerere alijulikana kama adui mkubwa wa Waingereza. Hii kwa muhtasari ndiyo historia ya Sheikh Suleiman Takadir na Nyerere. Lakini usuhuba huu ulikuja kuvunjika na watu wawili hawa wakawa mahasimu wakubwa, Sheikh Suleiman kafa hasemi na Nyerere na Nyerere kwa upande wake hakupata hata siku moja kumtaja Sheikh Takadir popote hadi anaingia kaburini. Inaaminika Sheikh Takadir alikufa kihoro baada ya kupigwa pande na TANU na wakazi wote wa Dar es Salaam na wanachama wa TANU kwa kosa la "kuchanganya dini na siasa." (Ikiwa msomaji wangu ulisoma makala yangu ya juma lililopita utakuwa umeona kuwa TANU ikiongozwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir ilipitisha azimio la kupiga vita hisia zozote na chembechembe za Uislam ndani ya TANU). Hakika Uislam ulikuwa na nguvu ndani ya TANU lakini haukuachiwa uvuke mipaka kuwabagua wengine waliokuwa si Waislam.
Kilitokea nini hadi kupelekea Sheikh Suleiman Takadir agombane na Nyerere? Chanzo cha mtafaruku huu ni Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka 1958. Waingereza waliweka masharti ambayo kwa hakika yalikuwa ya kibaguzi na yalifanya wananchi wengi wasiweze kukidhi sifa zilizowekwa za kuweza mtu kupiga au kupigiwa kura. Kulikuwa na sifa ya elimu, kipato na kazi ya kukubalika na kupiga kura kwa tabaka za rangi. Mpiga kura Mwafrika alitakiwa ampigie kura Mzungu, Muasia na Mwafrika. Masharti haya yalikuwa kisiki kigumu kwa uongozi wa TANU na wanachama wake kutimiza. TANU na viongozi wake wengi hawakuwa na hiyo elimu iliyokuwa ikitakikana wala kipato cha maana. Ili mtu asimame kama mgombea kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria au awe angalau mpiga kura ilibidi azikusanye sifa zote hizo mahali pamoja. Wapiga Kura na wagombea walitakiwa wawe na kisomo cha darasa la 10 au kipato cha pauni 400 kwa mwaka na kuwa na kazi ya maana. Waafrika waliokuwa na sifa hizi hawakuwa wengi katika TANU. Wengi katika TANU kama walivyokuwa wakipenda kujiita wenyewe walikuwa, "Baba Kabwela." Ikawa sasa ili TANU iweze kuweka wagombea ilibidi iwatafute watu nje ya uongozi wa TANU. Hapa ndipo lilipokuwa tatizo.
[TABLE="class: tr-caption-container, align: center"]
[TR]
[TD="class: tr-caption"]Nyerere Akitia Sahihi Azimio la Tabora[/TD]
[/TR]
[/TABLE]
Hofu aliyokuwanayo Sheikh Takadir ilikuwa kuwa watu walioingia katika TANU kuchukua uongozi ni Wakristo. Sheikh Takadir alikuwa anajua nguvu ya madaraka waliyokuwa wanakabidhiwa akawa na hofu kama uongozi huu mpya utakuja kutoa haki kwa Waislam uhuru utakapopatikana. Sheikh Takadir alitaka uhakika wa hali ya baadae ya Waislam katika Tanganyika huru. Katika mkutano wa Halmashauri Kuu Makao Makuu ya TANU, New Street Sheikh Takadir alimkabili Nyerere akamshutumu kuwa hakuwa na nia nzuri na Waislam, atakuja wapendelea ndugu zake Wakristo katika Tanganyika huru. Sheikh Takadir akawageukia wenzake katika Baraza la Wazee wa TANU akasema, "Tuzibe ufa tusije tukajenga ukuta." Jambo lile lilikuwa zito. Nyerere alijiinamia na aliponyanyua uso wake machozi yalikua yanambubujika. Mkutano haukuweza kujadili jambo lile na kikako kile kikavunjika pale pale na wajumbe wakawatawanyika.
Sheikh Takadir ''akatoswa,'' kwani alikuwa amevunja mwiko mkubwa katika TANU. Mzee Iddi Tulio akachaguliwa kushika nafasi yake. Huku ''kutoswa'' na kutengwa na jamii ndiko kulikosababisha kifo cha Sheikh Takadir. Alikuwa hata akitoa salamu hakuna aliyeitika. Akienda sokoni Kariakoo kununua chochote kile hakuna aliyekuwa tayari kupokea hela yake. Haikuchukua muda mrefu Sheikh Takadir akaaga dunia. Kabla Sheikh Takadir hajafa TANU ilifanya mkutano mkubwa sana na Nyerere akamshambulia Sheikh Takadir kwa kutaka kuwagawa Watanganyika katika misingi ya dini. Baada ya mkutano kundi kubwa lilikwenda nyumbani kwa Sheikh Takadir Mtaa wa Msimbazi kuzomea huku wakiimba, "Takadir Mtaka Dini." Sheikh Takadir alitoka nje akasimama kizingitini akasema maneno haya, "Ndugu zangu In Sha Allah iko siku mtakuja kunikumbuka." Haukupita muda mrefu Sheikh Takadir akatangulia mbele ya haki na kwa kipindi kirefu katika historia ya uhuru wa Tanganyika hakuna aliyemkumbuka Sheikh Suleiman Takadir, Askofu Makarios wa Tanganyika. Hivi sasa Sheikh Suleiman Takadir anatajwa sana na kizazi cha leo. Utabiri wake kuwa ndugu zake watakuja kumkumbuka umetimia. Swali la kujiuliza ni iweje hii leo baada ya miaka 57 kupita Sheikh Suleiman Takadir anarejeshwa upya katika historia ya kupigani uhuru wa Tanganyika? Hiki ni kitendawili kinachongoja kuteguliwa.