Jinsi Nyerere alivyofanyiwa hila hadi kuacha kazi ya ualimu

Jinsi Nyerere alivyofanyiwa hila hadi kuacha kazi ya ualimu

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
11,884
Reaction score
21,175
Kitabu Uamuzi wa busara kinazungumzia maamuzi mbalimbali magumu yaliyofanywa na Mwalimu JK Nyerere na TANU. Kuanzia Mwalimi kujiuzulu kazi ya ualimu, TANU kuamua kutosusia uchaguzi, Mwalimu kujiuzulu ubunge, Mwalimu kujiuzulu Uwaziri Mkuu, Muungano, Azimio la Arusha. Kinapatikana ndani ya app ya Maktaba Sauti. Ipo playstore.
Uamuzi cut.jpg


Siku ya Jumapili tarehe 22/3/1955 Mwalimu Julius K. Nyerere alifanya kitendo kimoja kikubwa cha ushujaa na busara, ambacho kama hakingefanyika labda historia ya nchi yetu hii ingekuwa tofauti kabisa na vile ilivyo leo.

Kitendo hicho ni uamuzi wa kuacha kazi ya Ualimu aliyokuwa akifanya katika Shule ya Sekondari ya Pugu, ambayo iko maili 12 tu kutoka mjini Dar es Salaam.

Mwalimu Nyerere alipewa kazi ya kufundisha katika Shule hiyo tarehe 9/10/1952. Baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Edinburgh. Uingereza, na kujipatia shahada ya digrii ya M.A. mnamo mwezi Julai lakini kuanza kazi hasa alianza mwezi Februari 1953, na tangu wakati huo akaanza kujishughulisha na Chama cha Tanganyika African Association (T.A.A.) mjini Dar es Salaam.

Baada ya miezi miwili tu, yaani mwezi Aprill, 1953, kulikuwa na uchaguzi wa Viongozi wa Chama hicho. Aliyekuwa Rais wa Chama mpaka wakati huo alikuwa Bw. Abdul Sykes, ambaye alisimama tena kugombea uchaguzi, na Mwalimu Nyerere naye akasimama. Kura zilipopigwa Mwalimu Nyerere akapata ushindi, kwa hiyo ikawa amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha T.A.A.

Wale ambao wamepata kusikia habari za Chama cha T.A.A. wanajua kwamba Chama hicho hakikuwa Chama cha siasa. Hali hii haikumridhisha hata kidogo Mwalimu Nyerere, kwa hiyo jitihada yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kukiongoza Chama hicho ikawa ni kukibadili kiwe Chama cha Siasa. Akaanza kuichungua kwa makini Katiba ya T.A.A. na kutafuta njia za kubadilisha iwe na madhumuni ya Kisiasa.

Tarehe 10/10/53 kulikuwa na Mkutano wa T.A.A. katika nyumba iliyoko mtaa wa Lumumba, mjini Dar es Salaam. Kulikuwa na viti viwili tu ndani, Mwalimu Nyerere akakalia kimoja, Mzee John Rupia kakalia kingine, wajumbe wengine. Waheshimiwa kina Abdul Sykes na Ally Sykes na Dossa Azizi ikawabidi wakae kwenye masanduku tu yale ya kusafirishia mizigo. Mheshimiwa Rashidi Kawawa alikuwa mtumishi wa Serikali wakati huo, na tarehe 1/8/1953, Gavana Twining alikuwa amepiga marufuku watumishi wote wa Serikali wasiwe Wanachama wa T.A.A. wala wasiwasaidie shughuli zake.

Katika Mkutano huo ndipo Mwalimu Nyerere akawaeleza wenzake mawazo yake juu ya umuhimu wa kubadilisha T.A.A. kiwe Chama cha Siasa. Wenzake waliyafurahia mawazo hayo, na wakakubaliana wafanye matayarisho yanayohitajika ili waweze kupendekeza mabadiliko hayo katika Mkutano Mkuu waMwaka wa T.A.A., ambao ungefanywa mwezi Julai, 1954.
Jambo mojawapo lililozungumziwa kwa kirefu lilikuwa ni jina la Chama hicho, baada ya kukibadilisha na kukifanya Chama cha Siasa, kiitweje? Bwana Abdul Sykes akatoa wazo kwamba kiitwe Tanganyika African Union, lakini wenzake wakakataa kwamba jina hilo lingefanana mno na Kenya African Union (KAU) ambayo ilikuwa imepigwa marufuku Kenya, konekana pengine kwa sababu hiyo Serikali ingekataa kukiandikisha Chama kwa jina hilo la Tanganyika African Union. Mwalimu Nyerere akatoa wazo kwamba labda likiongezwa neno “National” baada ya Tanganyika, hapo bila shaka litakubaliwa. Yaani Chama kiitwe Tanganyika National African Union. Hapo Ally Sykes akapinga, akasema kifupi cha Tanganyika National African Union ni T.N.A.U. na haipendezi hata kidogo kutamka, kwa hiyo akashauri maneno yapangwe vizuri zaidi yawe Tanganyika African National Union, ambayo kifupi chake kitakuwa T.A.N.U. Kila mtu akatamka TANU na akaona inampendeza, basi wakakubaliana wapendekeze jina la TANU. Na hivyo ndivyo jina letu lilivyopatikana.

Mkutano wa Mwaka wa T.A.A. ulipofanyika tarehe 7.7.1954, mapendekezo ya mabadiliko hayo yakatolewa na kukubaliwa, na TANU ikawa IMEZALIWA, vile vile chini ya Uongozi wa Mwalimu Nyerere. Wakati huo wote lakini, alikuwa anaendelea na kazi yake ya Ualimu katika shule ya Pugu.
Mwezi Februari, 1955, Mwalimu Julius Nyerere, Kiongozi wa TANU alisafiri kwenda New York, Amerika, kwenye Umoja wa Mataifa kuhutubia Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa.
Nyakati hizo Tanganyika ilikuwa chini ya Umoja wa Mataifa, na Uingereza ilikuwa inatutawala kwa niaba tu ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa ulikuwa na mtindo wa kutumia ujumbe kuja Tanganyika karibu kila miaka miwili, kukagua utawala wake unavyoendeshwa na kutoa taarifa kamili kwenye Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa. Mwezi Agosti, 1954 ulikuja Ujumbe wa aina hiyo hapa Tanganyika, na taarifa yao ni kama ilivyoelezwa hapo awali.
TANU ilifurahishwa na taarifa hiyo. Kwa hiyo ikaamua kupeleka Ujumbe wake huko huko kwenyeUmoja wa Mataifa wakati ambapo taarifa hiyo ingejadiliwa, ili aweze kutilia mkazo zaidi na kueleza kwa kirefu zaidi nia na matumaini ya watu wa Tanganyika, na juu ya Chama kipya cha TANU kilichokuwa kimeanzishwa, na kueleza makusudio ya Chama chetu ya kuwatayarisha Watanganyika kujitawala wenyewe. Mwalimu Nyerere akachaguliwa kwenda kufanya kazi hiyo.

Gavana alipopata habari hizo akastuka sana. Yeye na Serikali ya Uingereza kwanza hawakuipenda taarifa ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, sasa kusikia TANU inapeleka Mjumbe New York, na mjumbe mwenyewe ni Julius Nyerere, Gavana akaamua naye apeleke Ujumbe mzito wa watu watatu wakubwa sana kumpinga Mwalimu Nyerere huko kwenye Mkutano wa Baraza la Wadhamini. Jambo hilo likapitishwa haraka katika Baraza la Kutunga Sheria (Legco), lakini Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria wakakatazwa kabisa wasitoe siri hiyo kwa Mwalimu Nyerere au kwa kiongozi yeyote wa TANU.

Baada ya Mkutano huo wa Baraza la Kutunga Sheria, wajumbe watatu Waafrika wakapanda gari mojakurudi pale “Chiefs Quarters” walipokuwa wamefikia. Hiyo ilikuwa ni Februari tarehe 10, 1955. Walipofika Morogoro Road, wakamwona Mwalimu Nyerere anatembea kwa miguu. Akawapungia mkono wakasimamisha gari, akawaambia kwamba alikuwa njiani anakwenda huko huko kambini kwao, kwa sababu alihitaji kuwaona. Mmoja haraka akajibu “haya vema utatukuta gari ikapigwa moto wakaendelea. Mmoja wao akauliza “kwa nini tusimchukue, naye kasema anakuja kutuona?” Akajibu “hapana, yeye amezoea kutembea kwa miguu”. Lakini huyo mmoja akasisitiza kwamba wamchukue, basi wale wenzake wawili wakasema haidhuru wamchukue, lakini wakasisitiza kwamba asiambiwe juu ya Azimio la Baraza la Kutunga Sheria la kupeleka New York Ujumbe wa kumpinga! Hawa walikuwa ni Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, waliochaguliwa na Gavana.
Pamoja na matatizo yote hayo Mwalimu Julius K. Nyerere, Kiongozi wa TANU, aliondoka kwenda New York, shilingi 12,000/- za nauli zilichangwa katika muda wa siku chache tu zikapatikana, akaondoka. Akafanya kazi yake aliyotumwa naTANU kufanya, akarudi salama Dar es Salaam.
Aliporudi kutoka New York, Mwalimu Nyerere alikuta Wakoloni wamekwisha jiandaa kumuondoa katika Uongozi wa TANU kwa njia ya hila sana. Kwa baraka za Mwenyezi Mungu hawakufanikiwa, na ndiyo bahati yetu sisi Watanzania, tukaweza kuwa katika hali hii ya Uhuru tulio nao leo. Ndiyo sababu TANU imeamua kuwa inafanya sherehe ya kukumbuka siku hiyo.

Wakoloni walipanga mtego wao na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Pugu, kuwa Mwalimu Nyerere atakaporudi kutoka New York, mara moja apewe kuchagua mojawapo kati ya mawili; ama afanye kazi ya Ualimu tu aache kabisa siasa; au afanye kazi ya Siasa tu aache kabisa Ualimu. Matumaini yao makubwa yalikuwa ni kwamba atachagua kazi ya Ualimu, yenye mshahara, kwa sababu walijua wazi kwamba TANU haikuwa na fedha ya kumlipa mshahara.

Mwalimu Nyerere alirejea kutoka New York siku ya Jumamosi tarehe 21/3/1955, jioni. Akaenda nyumbani kwake Pugu. Asubuhi yake, Jumapili, tarehe 22/3/1955, Padri Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari yaPugu akamwita Mwalimu Julius Nyerere katika chumba cha Shule hiyo, akamwambia kwamba kutokana na jinsi yeye Julius Nyerere alivyokuwa akijishughulisha sana na Siasa, haingewezekana kumruhusu aendelee na kazi ya Ualimu; kwa hiyo alikuwa amemwita ili achague moja kati ya haya mawili: Kazi ya Ualimu, au kazi ya Siasa. Padri huyo akamshauri Mwalimu Nyerere hivi: -“Mwanangu Julius, Ualimu na Siasa havipatani hata kidogo, fuata oni langu, uache kabisa mambo ya Siasa na uzingatie kazi yako ya Ualimu”.

Baada ya Mkutano huo na Padri Mkuu wa Shule, Mwalimu Nyerere alitoka nje, fikra zimemjaa kichwani, akaenda nyumbani akiyafikiri maneno hayo na akijiuliza afanye nini sasa. Swali lililokuwa mbele yake lilikuwa gumu, maana aliambiwa achague kati ya sifa na usalama wa kazi ya Ualimu au kujitosa katika bahari ya Siasa. Mwalimu Nyerere alitafuta kichwani mwake jibu la swali hili kwa makini sana.
Lakini haikuchukua muda mrefu, akapiga moyo konde, akamwendea Padri Mkuu wa Shule, AKAMPA BARUA YA KUJIUZULU. Hivyo akawa amefanya uamuzi wa kuacha kaziya heshima na mapato na usalama, mambo ambayo angeyapata akiwa ni Mwafrika wa kwanza Tanganyika kupata Shahada ya digrii. Badala ya kazi hii nzuri, Mwalimu akakubali kushika kazi ya Uongozi wa Siasa, kazi ambayo wakati huo ilikuwa na hatari ya kufungwa wakati wo wote, kazi ambayo haikuwa hata na uhakika wa mafanikio, kazi ya unabii wa kuwaunganisha watu wote wa nchi ya Tanganyika kuwa Taifa moja.

Hatuna budi tukumbuke Uamuzi huo wa busara alioufanya Kiongozi wetu siku hiyo ya Jumapili tarehe 22/3/1955. Kwa sababu kama angeamua vingine yaani kuacha Uongozi wa Siasa na kuendelea na kazi ya Ualimu, pengine Historia ya Tanzania ingekuwa tofauti kabisa na vile ilivyo leo. Majira yetu haya yangekuwaje sasa.

Watanzania na Wana-TANU tukumbuke tulikotoka, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa busara na hekima aliyompa Mwalimu Julius Nyerere siku hiyo, busara na hekima ambayo ilimwezesha kufanya uamuzi mkubwa uliozishinda hila za Wakoloni za kujaribu kumwondoa katika Uongozi wa Siasa ya nchi hii. Tunapofurahia matunda yaUhuru wetu yatubidi kila mara tukumbuke jasho la Mashujaa, kama Mwalimu Julius Nyerere, jasho ambalo lilituletea matunda haya.
 
Back
Top Bottom