Subash Patel nilimjua katika miaka ya mwishoni 1970 au mwanzoni 1980 kupitia rafiki yake Said Ibrahim ambaye mimi pia ni rafiki ndugu.
Said ndiye alinipeleka nyumbani kwake.
Miaka hiyo alikuwa anaishi nyuma ya Zanzibar Guest House Mtaa wa Zanaki na Libya Street sehemu za Kisutu. Siku hizo Subash hakuwa tajiri lakini mfanyabiashara kijana anaeinukia. Ninachokumbuka kila nilipokuwa nasoma jina la Subash katika magazeti au kumuona katika TV ni kuwa ilikuwa nyumbani kwake ndipo nilipoiona movie mashuhuri, "The Message," kwa mara ya kwanza.
Hii ilikuwa sinema maarufu sana kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (SAW). Sinema hii tukiisoma sifa na "reviews," zake kwenye magazeti tu kwani enzi hizo Tanzania ilikuwa hoi na taaban kwa kila kitu.
Sinema za Holywood zilikuwa haziingii nchini. Waagizaji wa filamu Tanzania Film Company (TFC) kazi iliwashinda kabla hata hawajaianza. Kwangu Mimi kupata nafasi ya kuangalia sInema hii halikuwa jambo dogo.
Iko siku Subash alikuja ofisini kwetu alikuwa na miadi na Mkurugenzi wa Idara tukaonana na kusalimiana lakini hakunikumbuka. Ilikuwa miaka mingi imepita na ilikuwa tumeonana mara moja tu.