Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

Watu wakiacha kurushia maneno wanaoadithia story zitakua nyingi...
Jamani kuadithia ni shuhuli msiwasimange watu.
Mimi nina story kuna mtu wetu wa karibu alikua mnywaji pombe ya kutoshayaani yule hajiwezi.sasa kapelekwa kwa mtaalamu kachinjwa msukule.
Kwa sasa ana 3 weeks tumeambiwa tusubiri miez mi3 kama atarudia.
Kama asiporudia nitaadithia..
Ukihadithia niite rafiki yangu
 
Big akikatiza kariakoo
FB_IMG_16766492295787268.jpg
 
Yule Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - Usiku wa mateso.



Usiku ule sitakuja kuusahau maana yale nloshuhudia yalikuwa nje kabisa ya ulimwengu huu wa nyama na damu, sijui niseme ni ulimwengu gani ule lakini itoshe kusema ni ulimwengu wa ajabu mno nilioonyeshwa na bwana yule ...

Nilikurupuka usiku baada ya kusikia mtu anagonga hodi mlangoni nikadhani nipo ndotoni lakini kumbe haikuwa hivyo, ilikuwa ni kweli mtu anagonga mlangoni, wala sio kwamba masikio yangu yalisikia vibaya, lah, ilikuwa ni uhalisia.

Kabla ya kunyanyuka kitandani nikatazama nje dirishani, huko palikuwa shwari, kumetulia tuli-tuli, hata nilipoangaza mlangoni niliona mlango wa grill umefungwa, basi nikatulia kidogo nikijiuliza yanayoendelea, bado hapo mlango wangu ukiwa unaendelea kugongwa na kugongwa.

Mwishowe wa kufikiri niliamua kupiga moyo konde nikaenda sebuleni, nikawasha taa kisha nikaufuata mlango na kuufungua, kutazama simwoni mtu! Nilitazama korido nzima nisiambulie kitu wala mdudu yoyote anayetembea ukutani, nikatazama milangoni, nikaona kila mlango kwa chini yake ukiwa ni kiza totoro, taa zimezimwa huko ndani, ni kimya cha mwituni! Moyo wangu unapiga kana kwamba unataka kutoka kifuani.

Kabla sijaufunga mlango, yaani nikiwa hapohapo bado naangaza, mara nilisikia sauti ya kikombe kikidondoka - puuh!- alafu ikafuatia na kilio kikali cha mtoto kule chumbani! Basi haraka nikaurejesha mlango wangu pasipo hata kuufunga na funguo, nikakimbilia kule chumbani kama mwendawazimu, kufika huko nikawasha taa upesi, kurusha macho kitandani namwona mtoto ameegamia ukuta, uso wake ameufinyaga kwa kilio na hofu. Chini kuna maji yaloyomwagika pamoja nayo kikombe cha plastiki ambacho huwa tunatumia kunywea maji.

Mtoto aliponiona alinikimbilia akanikumbatia kwanguvu akinambia baba kuna mtu baba kuna mtu ... Nikamuuliza mtu gani? Yuko wapi? Hakusema cha kueleweka.

Alikuwa anatetemeka mwili mzima, macho yake hayakomi kumwaga machozi, hapo amening'ang'ania kana kwamba nilimuahidi nitamrushia korongoni.

Nilitazama kila kona ya chumba lakini sikuona chochote kilichomtisha, kidogo nilipotazama dirishani, ndo' nikaona kivuli cha mtu akiwa anachungulia, kivuli kipana katika kingo ya dirisha langu la kaskazini, lakini kivuli hicho -kufumba na kufumbua - kilitokomea kwa kushuka chini! Nikastaajabu kuona.

Nilitulia hapo kidogo nikitazama, kila kitu mbele ya macho nikiona kama miujiza ama ndoto hivi, yaani muujiza mbele ya mboni zangu, niliporadhi ndipo nikasogea taratibu dirishani kutazama nje. Huko palikuwa pametulia tuli, hamna mtu wala kiumbe ninayemwona, lakini niliporusha macho kule kwenye mlango wa grill, nikaona mlango huo uko wazi! Sikujua nani nani aliufungua na ni muda gani alifanya hivyo maana sikusikia mlango huo ukipiga kelele zake za siku zote, nikabaki tu nikiutazama kwa kama dakika moja, sikuona kitu wala mtu hapo, kidogo nikasikia tena mtu akiugonga mlango wangu kwa mtindo uleule --- ngo ngo ngo ngo! "Nataka tuongee, nina shida na wewe!"

Aisee nikahisi tumbo linakoroga, miguu yangu inapoteza nguvu, pumzi yangu mwenyewe inanikaba. Kwa muda huo nilitamani pakuche lakini wapi! Nilihisi muda umekwama kunikomoa na mateso ya usiku ule. Nilitazama saa ya simu yangu nikaona zimepita dakika tano tu tangu nikurupuke toka usingizini, nikaamini kabisa muda unashirikiana vema na mtesi wangu. Ule ulikuwa usiku wangu wa adhabu.

Nikajitahidi kutulia kadiri nilivyoweza lakini sikufua dafu abadan, mlango wangu uliendelea kugongwa pasipo kukoma huku mtu anayegonga akinitaka tukaongee tena akitumia sauti yangu, moyoni nikaapa siendi popote, nitabaki palepale kitandani na mtoto wangu mpaka nione nini kitakachojiri.

Baada ya dakika moja ya kuvumilia, nasikia kabisa mlango unagongwa lakini napuuzia, mara nilisikia kitasa cha mlango kikitenguka - 'klap!'- alafu ikafuatiwa na sauti za bawaba za mlango 'kkrrriiiiiiiiii!' ... sauti zilizoashiria mlango wangu unafunguka alafu sauti hizo zikakoma ghafla na kuwa kimya! Kimya cha kaburi. Kwa kama dakika tatu hivi ni kimya, sikusikia kitu chochote kile, nipo tu kitandani nimemkumbatia mwanangu.

Kwa kipindi chote hicho,sikuwa najua nifanye nini maana ubongo wangu uligeuka kuwa uwanja wa fujo, moyo nao unapiga mpaka nausikia masikioni kana kwamba ngoma za turufu! Jasho nalo linanichuruza nalisikia kabisa likishuka mgongoni chii-chii-chii kuangukia chini.

Sasa baada ya kimya hicho cha muda, nilisikia vishindo vya miguu vikipita sebuleni, vinakatiza hapa na pale, pale na hapa, alafu baada ya sekunde kumi na tano hivi, mlango wangu wa chumbani ukagongwa mara moja, "ngo!" ... Ile 'Ngo' ya kuashiria mgeni ameshafika ndani kisha kukarudi kuwa kimya tena, kimya cha awali.Sasa nikawaza,kama mtu huyu amengia ndani kwangu, je, mimi sina budi kujihami na kitu chochote nilichonacho?

Upesi nikatazama kwenye pembe ya kitanda changu, kule nilazapo miguu, hapo kulikuwa na fimbo moja ndefu nene, nikaichomoa na kuishika mkononi barabara kama lolote likitokea basi nipate kujihami, lakini nilishika fimbo hiyo mpaka nikachoka, hamna nilichokiona wala hamna kilichoingia ndani.

Nilimaliza sala zote ninazozijua, nilimuita Mungu wangu kwa majina yote niliyofunzwa kanisani na mtaani lakini bado nilijihisi niko mwenyewe, dunia imenipa mgongo.

Nilingoja hapo kwa muda ambao niliona unatosha, nikanyanyuka kwenda kuufungua mlango wa chumbani kutazama sebuleni kama kuna mtu niliyemuhisi,kufika huko na kuangaza sioni mtu, lakini nilipotazama mlango wa sebuleni nikauona uko wazi, tena wazi ya kuachama haswa, nikarusha macho huko nje ya mlango, yaani koridoni, napo sikuona kitu wala mtu, lakini kitambo kidogo nikaanza kuhisi naishiwa nguvu katika namna ya ajabu, kichwa kinakuwa kizito na macho yananielemea, sijakaa vema nikaanguka chini, hoi taabani, hata kuusogeza mkono wangu mwenyewe nashindwa, sijiwezi kabisa, kitu pekee nilichokuwa namudu ni kusikia na kuona tu!

Nikiwa hapo chini, nimelala kifudifudi,sijui nini kinaendelea, macho yangu yanatazama kule koridoni, mara nilisikia sauti ya mlango unafunguka, haukuwa mlango mwingine bali mlango wa BIGI, na kitambo kidogo nikamwona mwanaume huyo anatoka sasa akija mwelekeo wangu.

Bwana huyo alikuwa amevalia kaniki nyeusi kiunoni, mithili ya taulo la kwendea bafuni, na kichwa chake amekiveka kiremba kikubwa chekundu, kiremba ambacho baki yake aliilazia kwa nyuma kana kwamba mwanamke mwenye nywele ndefu.

Kumwona bwana huyo akinijia, nikajaribu kwa nguvu zangu zote ninyanyuke lakini sikuweza kabisa kabisa, nilikuwa kama mtu aliyepigwa nusu kaputi kwaajili ya upasuaji, kitu pekee nilichokuwa naweza kufanya ni kugeuza shingo yangu huku na kule, hata nilipojaribu kutoa sauti kupiga yowe nayo hakuna! Nilikuwa mithili ya samaki majini, naachama tu mdomo lakini hamna chochote kinachotoka.

Bwana yule, nikiwa namshuhudia kwa macho yangu, aliingia ndani akaelekea moja kwa moja chumbani, kule ambapo mwanangu alikuwamo, huko sijui akawa anafanya nini, hata mtoto alikuwa kimya, baada ya muda kidogo akatoka akiwa amembeba mtoto begani huyoo anajiendea zake.

Aliuruka mwili wangu akatoka mlangoni kisha moja kwa moja akaenda kwake ... Nimebaki tu namtazama, macho yanavuja machozi ... naona kabisa mwanangu akienda kuuawa na huku sina la kufanya.

Nilifurukuta nikafurukuta ... nilifurukuta tena na tena. Nilifurukuta kwanguvu zangu zote na za akiba, nikatahamaki niko kitandani nimeketi nahema kama mbwa wa mashindano, nikajaribu kuunyanyua mkono wangu wa kulia, mkono ukanyanyuka, nikausogeza mguu, nao ukasogea, nikajiuliza ina maana yale yote niliyoyaona nilikuwa ndotoni?

Nilijikuta nafsi yangu inakataa.

Nilitazama kando yangu nikastaajabu mtoto hayupo, kitanda cheupe pe, nikanyanyuka upesi kama nakimbizwa kwenda kuwasha taa, nikawasha na kuangaza sikuona kitu, chumba kizima nilikuwapo mwenyewe. Nikakimbilia sebuleni kutazama, napo sikuona kitu, hata mlango wake umefungwa na funguo! Sasa nikahisi kurukwa na akili, mtoto yuko wapi?

Hapana! Nilizungumza mwenyewe kama mwehu ... hapana haiwezekani! Nikaufungua mlango wangu nikaenda moja kwa moja mpaka mbele ya mlango wa BIGI, nikaugonga mlango huo kwanguvu BAM-BAM-BAM-BAM! Fungua, namtaka mwanangu! BAM-BAM-BAM!- niliubamiza mlango huo bila huruma na bila kukoma, nafoka na kuchonga, namtaka mtoto wangu!

Kelele hizo zikawaamsha watu walokuwamo kwenye makazi ya Tarimo. Niliona wamewasha taa ndani wakiwa wanazozazoza, bila shaka walikuwa wanajiuliza ni nini kinachoendelea, lakini mimi sikujali, nikaendelea kuubamiza mlango wa BIGI niking'aka, kidogo mlango huo ukafunguliwa akatoka mwanaume huyo mpana akiwa amevalia kaushi yake pana na bukta.

Kabla hajasema kitu nikamwambia, "brother, namwomba mwanangu! Tena namwomba upesi kabla hatujajaza umati wa watu hapa."

Akawa ananitazama, hasemi kitu. Mara nikasikia mlango wa makazi ya Tarimo unafunguka, kutazama ni Mama Tarimo, mama huyo anatoka huku akiwa anatengenezea khanga yake kifuani, nyuma yake yuko dada mmoja hivi ambaye sikuwa namfahamu wana mahusiano naye gani, wote hao wawili nyuso zao zimeparwa kwa maulizo.

Mama Tarimo aliuliza, "Shemeji, kuna nini?" Nami upesi nikamwambia yule bwana BIGI amemchukua mwanangu kimazingara na mimi nimekuja hapo kumfuata. Kwa jazba nilokuwa nayo sikuwa najali chochote kile, niliyamwaga maneno mengi na vitisho, nikiapa siondoki pale mpaka pale nitakapompata mwanangu.

BIGI aliuliza, "Una uhakika mwanao yumo humu ndani?" Nikamwambia ndio, nikamtaka asogee pembeni mimi niingie ndani kutazama. Katikati ya hayo, mara Mama Tarimo akaniita: baba fulani, nilipomgeukia akaniuliza,"yule pale si mtoto?"

Kuangalia kwangu, nikamwona mtoto akiwa amesimama mlangoni ananitolea macho. Nikastaajabu. Nini hiki? Nilimwendea mwanangu upesi nikamkagua na kumuuliza alipokuwapo,akasema ndani, ndani gani na mimi niliangaza kila kona ninayoijua?

Niligeuka kumtazama BIGI, nikamwona bwana huyo ananiangazia, kama kawaida macho yake hayakuwa hata na tone la hisia ndani yake, hakusema kitu, ameegamia tu kingo ya mlango wake, nikaurejesha uso wangu kwa mtoto, nikamwona akiwa amejibana kwangu, amenishikilia nguo, anachungulia kwa woga.

Kidogo bwana BIGI akaingia ndani mwake, pia na Mama Tarimo, mimi nikawa wa mwisho kuufunga mlango.

Nilimpeleka mtoto kitandani nikamtaka alale lakini mimi nikiwa nasumbuka sana na mawazo kichwani, ina maana ni kweli mimi nilikuwa ndotoni? Ina maana yale yote ni mambo tu yaliyotungwa na ubongo wangu?

Sikuridhika...

Nilikagua mazingira ya mule chumbani, na hata sebuleni, nikaamini kabisa sikuwa ndotoni. Yale yote nloshuhudia yalikuwa halisia. Moja, kikombe kile cha maji bado kilikuwapo chini na maji yale bado sikuyadeki, lakini pili jasho nililomwaga nikiwa pale sakafuni sijiwezi kabisa, bado lilikuwapo, sasa halikuwa kimiminika bali limeganda pananata.

Sasa ilikuaje? Sijawahi kuelewa mpaka leo hii.

Baadae Jua lilipochomoza nikalishuhudia kama ukombozi, tena ukombozi nilioupambania kwa muda mrefu, mbali na kwamba nilihisi maumivu ya hapa na pale ya taya yangu ya chini, mimi sikujali sana na nilichofanya, pasipo kupoteza muda, nilidamka nikamwandaa mtoto na mimi pia kisha safari ikaanza kuelekea Massana hospitali, huko nilionana na mke wangu na pia mama yangu ambaye alifika muda si mrefu hapo, nikamwachia mtoto mama yangu nikimtaka aende naye kwake kule Mbezi Beach, Afrikana, mimi nitakuja kumpa habari vizuri nikitoka kazini, uzuri kumbe siku hiyo ndo' ilikuwa siku ambayo mke wangu alikuwa anategemea kutoka hospitali, hivyo basi wakaona ni vema wakienda huko Afrikana kwa pamoja. Mimi niliwaahidi nikitoka tu kazini nitaonana nao.

Baada ya kuachana nao, nilielekea kazini, huko niliweza kufanya kazi kwa kama masaa mawili ya mwanzoni lakini baada ya hapo nikaelemewa. Kichwa kilikuwa kizito kwa kukosa usingizi wa usiku ulopita kiasi nikawa naona kazi ni adhabu. Macho yananiwasha na niko 'slow' sana.

Nilitafuta 'kamuda' fulani, mbali na kubanwa hapa na pale, nikajipumzisha kidogo kwa kuegamia meza, usingizi ukanikomba bila huruma, kuja kuamka nimelala masaa mawili kama utani, na kama si kuamshwa sijui ningeamka saa ngapi? Kutazama simu yangu, naona 'missed call' na ujumbe mmoja, vyote vimetoka namba ngeni.

Ujumbe huo nilipoufungua ulikuwa unasomeka hivi: "Mimi Bembela nimesharudi nyumbani fanya tuongee." Nikapiga namba hiyo mara moja, simu ikaita kidogo na kupokelewa na sauti ya mwanamke, sauti ya Bembela, akanisalimu na kunijuza kuwa amefika nyumbani muda si mrefu, kila kitu amekiweka sawa lakini kuna jambo moja tu amekwama, anataka kuona kama naweza nikawa na msaada.

Alisema: "baba fulani, hapa sasa ili kila kitu kiende sawa, nahitaji nipate kitu kimoja ambacho ni mali ya yule bwana. Kitu kimoja tu, kama vile yeye achukuavyo vyetu na kuvitendea kazi, ndivyo na mimi pia. Je, unaweza nisaidia?"

Nikawaza vile viroba vya BIGI kule korongoni, je, mule hatuwezi kupata kitu? Nilipomweleza hayo akanielezea hofu lake ya kwamba vitu vile havina uhakika kama ni vyake au vya watu wengine, tusije tukawaingiza waso na makosa katika adhabu ya mtu mwingine, hivyo yatupasa kuwa na hakika asilimia zote.

Nilipofikiria vema, nikaikumbuka ile sarafu ya hamsini katika mfuko wangu wa suruali. Nilikuwa na hakika kabisa ile ilikuwa ni mali ya BIGI lakini ubaya ni kwamba sarafu hiyo siku ile nilivyotoka hospitali baada ya kunisababishia majanga sikukumbuka niliiweka wapi haswa, sikuibakiza nguoni mwangu.

Ila kitu kilichonipa moyo ni kwamba mke wangu hakuwapo nyumbani, na mimi sikuwahi kufanya usafi mule ndani chumbani tangu siku ile, hivyo niliamini naweza nikaipata nikiitafuta.

Nikamwahidi Bembela na yeye akakata simu tulipomaliza maongezi.

Mbali na kwamba, nilikuwa nimeokoa salio langu la simu kwa simu ile kukatwa na Bembela, nilikuwa pia nimejipunguzia maumivu ya kinywa changu ambacho kilikuwa kinanivuta sana, haswa taya ya chini, kila nilipokuwa nazungumza neno.

Sikufahamu maumivu hayo yalisababishwa na nini na sikudhani kama yangeendelea kuwa makali vile, kipindi nayahisi pale asubuhi niliyachulia kiwepesi tu nikidhani labda nililala vibaya na hivyo yatakoma lakini kadiri muda ulivyoenda nilianza kuhisi hiyo kitu ni 'serious'.

Na kweli ilikuwa ni 'serious'.

Mpaka kufikia majira ya usiku, taya yangu ya chini ilianza kupinda ikielekea upande wangu wa kushoto wa mwili! Kila nilipoivuta kuiweka sawa, nilihisi maumivu makali yasokuwa na mfano!




***

1
 
Back
Top Bottom