Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Jukwaa la kimataifa la kutetea haki za Wamasai, Maasai International Solidarity Alliance (MISA), limetangaza kupinga vikali ripoti mbili za tume za rais zilizowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 12, 2026 katika Ikulu ya Chamwino State House.
Katika taarifa yake ya Machi 18, 2026, MISA ilisema “inakataa kabisa mapendekezo ya tume hizo” na kuitaka Serikali ya Tanzania kutoyatekeleza.
Machi 13, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa jijini Dodoma alipokea ripoti za tume zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliotokana na kuwahamisha wakazi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro. Ripoti hizo zimebainisha kasoro kadhaa.
Soma: Rais Samia apokea taarifa ya Tume za Rais kuhusu mgogoro wa ardhi na uhamaji wa hiari, Ngorongoro
Ripoti hizo zilibaini kuwa wananchi hawakushirikishwa vya kutosha, kukosekana kwa sheria na sera zinazoongoza mpango wa kuwahamisha wakazi hao, na mpango wa kuwahamisha ukitumia zaidi ushawishi badala ya utashi.
Hata hivyo Rais Samia alisema Serikali itaendelea na mpango wa kuwahamisha wakazi hao kwa kutumia mfumo unaosisitiza hiari ya wananchi na ushirikishwaji mpana wa jamii.
Moja ya tume hizo ilichunguza migogoro ya matumizi ya ardhi katika Ngorongoro Conservation Area (NCA) na maeneo jirani na nyingine iliyopitia zoezi la serikali la uhamishaji wa hiari wa wakazi.
Ziliundwa Desemba 2024 na kuzinduliwa Februari 2025 kufuatia maandamano makubwa ya jamii ya Wamasai yaliyofanyika Agosti 2024.
Mchakato Wenye Dosari
MISA imedai kuwa tume hizo hazikuundwa kutatua changamoto za jamii bali kuthibitisha maamuzi yaliyokuwa tayari yamefanywa na serikali.
Kwa mujibu wa MISA, hadidu za rejea (ToR) zililenga kuhalalisha uhamishaji wa wakazi badala ya kuhoji kama uhamishaji huo unapaswa kufanyika.
“Watu wetu walijitokeza kwa wingi kutoa ushahidi wakiamini mchakato huu ungeleta suluhisho la migogoro ya ardhi, lakini tangu mwanzo ulikuwa umeelekezwa kuthibitisha maamuzi yaliyokwishafanywa,” ilisema taarifa hiyo.
Tuhuma za Upendeleo
MISA pia inapinga uhalali wa ripoti hizo, ikidai zilitegemea nyaraka zilizokwisha kupingwa kama ripoti ya mwaka 2019 ya Multiple Land Use Model (MLUM), na kurudia hoja zinazotumika kuhalalisha kuwaondoa wafugaji wa Kimasai.
Imedai kuwa tume zimetumia takwimu zilizokuzwa kuhusu idadi ya watu, mifugo na wanyamapori, kuchagua taarifa kwa upendeleo na kupuuza ushahidi wa kisayansi unaopingana na msimamo wa serikali.
Hoja Kuhusu Uhifadhi
MISA inapinga vikali hoja kuwa uwepo wa Wamasai ndani ya Ngorongoro Conservation Area hauendani na uhifadhi wa mazingira.
Imesema kwa karne nyingi Wamasai wameishi sambamba na wanyamapori na mifumo yao ya jadi imechangia kulinda mfumo huo wa ikolojia.
Aidha, ilidai ripoti hizo zimepuuza athari za utalii wa kibiashara, ikitaja ongezeko la hoteli za kifahari, barabara, uwindaji na shughuli za safari ambazo hazikujadiliwa ipasavyo.
Uhamishaji na Uwajibikaji
MISA imesema imepokea kwa tahadhari hitimisho la tume mojawapo lililokiri kuwa uhamishaji tangu 2021 haukuwa wa hiari kikamilifu.
Imesema jamii zililazimishwa kuondoka kutokana na kunyimwa huduma za msingi, vikwazo vya matumizi ya ardhi, kupungua kwa miundombinu ya kijamii.
Hata hivyo, ilikosoa tume kwa kushindwa kuwawajibisha viongozi au taasisi zozote za serikali kwa madai ya ukandamizaji huo.
Migogoro ya Maeneo
Kuhusu Pololeti Game Reserve, MISA imesema ardhi ya vijiji ilibadilishwa kinyume cha sheria kuwa hifadhi mwaka 2022.
Pia imepinga uainishaji wa Lake Natron kama Game Controlled Area, ikisema eneo hilo lina vijiji 26 na wakazi zaidi ya 70,000, na sheria hairuhusu hadhi hiyo kwenye ardhi ya vijiji.
Kukamatwa na Propaganda
MISA imeeleza wasiwasi wake kuhusu matukio yaliyofuata baada ya ripoti kuwasilishwa, ikiwemo waraka wa televisheni uliotolewa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) uliodaiwa kueneza propaganda.
Pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu kukamatwa kwa wakazi watatu wa Ngorongoro Machi 15, 2026 na askari wa Ngorongoro Conservation Area Authority katika eneo la Ndutu na kuamriwa kuondoka kupisha upanuzi wa utalii.
Msimamo
MISA imesisitiza kuwa haitakubali uhamishaji kutoka ardhi za mababu, haitakubali mabadiliko ya sheria yatakayorahisisha kufukuzwa kwa jamii na itachukua hatua za amani kupinga maamuzi hayo.
Pia ilitoa wito kwa serikali kusitisha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wafugaji katika maeneo kama Pololeti, Ndutu na Oldupai, na kutaka usimamizi wa Ngorongoro Conservation Area urejeshwe mikononi mwa jamii za asili.
Kwa upande wa kimataifa, MISA imezitaka taasisi kama International Union for Conservation of Nature na UNESCO kuunga mkono mifumo ya uhifadhi inayoheshimu haki za watu wa asili.
“Msimamo wetu uko wazi—tutabaki kwenye ardhi yetu. Tunahitaji mazungumzo ya kweli, si ukandamizaji,” imehitimisha taarifa ya MISA.
Source: The Chanzo