Mchoro wa ukutani wenye urefu wa mita 80 unaoonyesha ndege wa taifa wa Uganda, korongo, pamoja na dragon wa China anayeashiria maelewano, ulisimama kama kitovu cha tamasha la jadi lililofanyika hivi majuzi katika Kijiji cha Kasinyi, jamii iliyopo mbali katika Wilaya ya Buliisa magharibi mwa Uganda.
Hafla hiyo, iliyoandaliwa na kampuni ya mafuta ya China Sinopec, iliwaleta pamoja wanafunzi na walimu wao 42 kutoka shule tano za msingi za huko ili kusherehekea mawasiliano ya utamaduni na ushirikiano katika sekta ya nishati kupitia kupaka rangi kwenye mchoro na mashindano ya kuchora.
Pia ilikwenda sambamba na Siku Wazi ya Umma ya kampuni hiyo katika Eneo la Mafuta wa Tilenga, ambapo kampuni ya Sinopec inajenga Kituo Kikuu cha Uchakataji (CPF), sehemu muhimu ya sekta ya mafuta inayoibukia nchini Uganda.
Mradi wa Tilenga ni mradi wa kwanza wa kibiashara wa mafuta nchini Uganda wenye uwekezaji wa jumla unaozidi dola bilioni 2 za Kimarekani. Mara baada ya kuanza kazi, kituo cha CPF kinatarajiwa kushughulikia zaidi ya mapipa 200,000 ya mafuta ghafi kwa siku, na kuiweka Uganda kama kitovu muhimu katika mtandao wa nishati wa Afrika Mashariki.
Miongoni mwa washiriki hao vijana, Benon Atuhaire mwenye umri wa miaka 14 alionesha mtambo wa kuchimba mafuta na mashine licha ya hali ya maisha ya kijijini, wakati Tolbert Tumukwaise alionesha jiji la kisasa linaloinuka kutokana na ukuaji unaotokana na mafuta. Kazi nyingine za sanaa zilionesha udesturi ya uvuvi wa Ziwa Albert ukistawi pamoja na miradi inayoendelea ya mafuta.
Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong alisema tukio hilo ni sikukuu ya kitamaduni na pia ni ishara ya kukuza uhusiano kati ya watu na watu.
"Tukio la leo linawapa wakazi wa eneo hili nafasi ya kuelewa utamaduni wa Kichina na kujionea haiba yake, na pia kuchunguza njia mpya za kampuni za China kutangamana zaidi katika jamii ya wenyeji na kutimiza majukumu yao ya kijamii," Zhang alisema.
"Mradi wa Tilenga sio tu kielelezo cha ushirikiano wa kiuchumi bali pia ni daraja la urafiki kati ya China na Uganda. Unabeba matarajio yetu ya pamoja ya mustakabali mwema na unashuhudia kuimarika kwa uhusiano wa pande zote wa ushirikiano kati ya China na Uganda," Zhang aliongeza.
Yi Xuhui, mwakilishi wa kampuni ya Sinopec Uganda, alisema zaidi ya miundombinu, kampuni yao imejitolea kujenga uwezo wa muda mrefu. Wakati wa ujenzi wa kituo cha CPF, kampuni ya Sinopec itaajiri zaidi ya Waganda 4,000 kufanya kazi pamoja na wenzao wa China wapatao 1,000.
"Baada ya kampuni ya Sinopec kuacha mradi wa Tilenga, tunaacha nyuma timu nzima ambayo inajua jinsi ya kushughulikia ujenzi katika eneo la mafuta na gesi," Yi alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Buliisa, Baheebwa Byagagaire alisema sekta hiyo imeleta ajira na miundombinu.
“Wananchi wengi wa Buliisa wamenufaika kwa sababu wale waliosoma na ambao hawajaajiriwa wamepata kuajiriwa, mtu ambaye alikuja hapa mara ya mwisho 2017 na kurudi tena sasa ataona tofauti kubwa kabisa, Buliisa imebadilika kutokana na mtandao mpya wa barabara,” alisema Byagagaire.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini, Uganda iligundua kadiri ya mapipa bilioni 6.5 ya mafuta mwaka 2006, ambapo mapipa bilioni 1.4 yanachukuliwa kuwa yanafaa kibiashara.
Kwa sasa nchi hiyo inajenga kiwanda cha kusafisha mafuta na bomba la kusafirisha mafuta ghafi kama sehemu ya mkakati wake mpana wa kufungua uwezo wa maliasili hiyo.