Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 34,256
- 44,597
Na. M. M. Mwanakijiji
Sioni namna gani Samia anaweza kujiuzulu halafu mambo yakaisha. Video na picha zinazoendelea kutoka sasa hivi na zile zitakazotoka baadaye zinatudokeza uzito, ukubwa na uovu uliofanyika kati ya Oktoba 29 na Nov 3/4. Tunaweza kuona kuwa kilichofanyika hakikuwa suala la kudhibiti waandamanaji au kuzuia vurugu. Ni wazi kabisa kuwa kilichotokea ilikuwa ni kuonesha kile wanachokiita wenzetu "impunity" yaani kutokujali matokeo yoyote. Mauaji yaliyofanyika siku hizi kwa lengo la kuzuia vijana yameonesha bila ya shaka kuwa waliotekeleza mauaji yale walikuwa wanajua wametumwa kufanya nini.
Kwa wale wanaojua taratibu za kutawanya watu kisheria wanajua kabisa kuwa kuna sheria inayoongoza hilo. Jeshi la polisi lina utaratibu ambao hutumika kabla ya kuanza kutumia nguvu dhidi ya mikusanyiko isiyo halali. Ni wazi kuwa siku ile na zile zilizofuatia utaratibu huo haukutumika ikiwemo kutangazwa kwa agizo la rais kwa watu kutawanyika na kutolewa onyo. Kilichotokea ni kuwa vyombo vya dola vilitoka kwenda kuua kama onyo pekee. Lakini kuwa hili la kutokujali matokeo ndiyo liliwapa kiburi cha kuua bila kuuliza. Video nyingi zitakazotoka hasa ndani ya wiki hii zitawafanya hawa wenye mioyo migumu kukubali kuwa yalitokea mauaji ya halaiki.
Miaka mingi nilikuwa najiuliza hivi iliwezekana vipi kwenye mauaji ya Rwanda watu zaidi ya laki nane kuuawa ndani ya siku 100. Yaani, kwa wastani watu 8000 walikuwa wanauawa kila siku wakati wa mauaji yale ndani ya kanchi kadogo kama Rwanda. Sasa tukiangalia yaliyotokea Tanzania na jinsi yalivyotokea si vigumu kukisia namba ya watu waliouawa ndani ya siku nne tu Tanzania. Nimekuwa nikijiuliza kuwa inawezakana wameuawa watu wengi kuliko tunavyodhania? Makisio ya chini kabisa ya watu 2000 tu yanaweza kuwa ni ya chini kweli.
Kutokana na ukweli huu ni wazi kuwa ilipofika ile Jumatatu ya tarehe 3 walijua mara moja kuwa yametokea mauaji makubwa. Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya ndani kabisa (ka-nzi) ni kuwa mara baada ya picha ya mauaji ilivyoanza kuoneakana jambo moja lilikuwa dhahidi - hawawezi kuachia ngazi au kujiuzulu. Lakini la pili ni kuwa haiwezekani kujiuzulu mtu mmoja au watu wawili watatu. Maamuzi ya kuua Watanzania kwa kisingizio cha kuzuia "vurugu" yalifanywa na kikundi cha watu wakubwa sana katika nchi na kupata baraka ya viongozi wa kisiasa. Hesabu waliyokuwa wameipiga ni kuwa watu wangekimbia kujificha mara baada ya risasi za mwanzo. Walifikiria labda watu si zaidi ya 30 wangeuawa; lakini namba ilivyokuwa inakuja hakukuwa na mjadala tena.
Ilibidi wale yamini - viongozi wa kisasa, na wale wa vyombo vya dola. Walijua mapema kuwa wakati utakapokuja kuwajibishwa haitaishia kwa Rais tu bali watendaji wa juu wa vyombo vya usalama watasimamishwa kizimbani na kama watasimamishwa katika mahakama za Tanzania basi adhabu ya kunyongwa itakuja kutumika dhidi yao. Hili limekumbushia baadhi ya viongozi wa nchi zilizosimamia mauaji ya wananchi wao na baadaye kuwajibishwa. Nitatoa mifano michache hapa ili watu wajue hili si suala la kuwajibishwa kwa Samia tu. Litaondoka na wengi.
1. Iliyokuwa Yugoslavia - Mbosnia huyu alikuwa Rais na akashitakiwa kwa mauaji ya halaiki na uhalifu wakati wa vita (war crimes). Mmoja wa maafisa wake wa Usalama kutoka Jeshi la Bosnia Radko Mladic naye alishtakiwa kwa mauaji ya halaika, uhalifu wa kivita na makosa mengine. Wote walihukumiwa kifungo cha maisha.
2. Rwanda - aliyekuwa Meya wa mji wa Taba Jean Paul Akayesu alishtakiwa mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita. Pamoja na huyo aliyekuwa Kanali katika Wizara ya Ulinzi Theoneste Bagosora na Meja Jenerali Augustin Bizimungu wote walikutwa na hatia ya mauaji ya halaiki na wakala vifungo virefu..
3. Liberia/Sierra Leone - wengi tunakumbuka sakata la Charles Taylor alikuwa Rais wa Liberia. Yeye na maafisa wengine wa RUF walikula miaka mingi kufuatia vita ya Sierra Leone. Charles Taylor akiwa Rais wa zamani kushtakiwa makosa ya uhalifu wa kivita. Ikumbukwe kuwa kinga ya rais inamzuia kushtakiwa ndani ya Tanzania kwa vitendo alivyofanya akiwa madarakani; haivizuii vyomo vya kimataifa kumshtaki.
4. Chad - huku kunalingana sana na mambo ya hapa kwetu. Aliyekuwa Rais wa Chad Hissene Habre alishtakiwa kwa mauaji ya wananchi wake na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Wakuu wake wa vikundi vya watekaji na watesaji kama Saleh Yunus na Mahamat Djibrine wote walishtakiwa tena na mahakama za ndani na kuhukumiwa vifungo vya maisha.
Ipo mifano mingine ya kule Mynmar, Guatemala, Argentina, n.k ambako viongozi wa kisiasa na watendaji wao kwenye vyombo vya usalama walidhania wako salama kwa vile waliendelea kuendesha magari ya kunesanesa na kupepewa bendera huku wakipigiana saluti na kutinga tai zenye kung'ara. Walidhani kwa vile bado wanaitana 'waheshimiwa' basi makosa yao yatasahauliwa.
Katika sakata hili la Tanzania na dhambi hii kuu tunayoishuhudia tukumbuke majina ya wahusika wa mauaji haya na kuwa wakumbuke kabisa watakuja kuwajibishwa. Inaweza kuwa Disemba 9 hii lakini haitaishia Disemba 9 hii. Wamekula yamini kulindana kwa ile kanuni ya wahenga kuwa "panya hawakamatani'. Geresha ya uundwaji wa tume ni matusi na kejeli kwa utawala wa haki. Ni wazi tume hiyo haiwezi kamwe kumnyoshea mkono Samia wala watendaji wa juu - na tunaweza kukisia mojawapo ya kauli watakuja nazo ni kuwa
"Tume imefanya uchunguzi na imehojiana na watu mbalimbali na katika uchunguzi wowote hatukuona ushahidi wowote wa maagizo ya mauaji kutolewa na uongozi wa juu wa nchi. Mauaji yaliyofanyika hayakuagizwa na Rais au watendaji wake na ni matukio yaliyofanywa na askari walijichukulia sheria mkononi".
Kauli hii itakapotoka ndiyo itafungua mwanya wa wao kuwafukuza kazi maafisa wa polisi na kuwashtaki kwa mtindo wa kuwatoa kafara - wao wenyewe wakiombea kuwa hawataguswa. Wamekula yamini kuwa wao na watoto wao ni lazima waendelee kukaa madarakani kwa miaka hamsini ijayo hadi kizazi chao kitakapokuwa kimekufa bila kufishwa mahakamani kwa makosa ya Oktoba 30.
Na sisi tule yamini; na sisi tuapizane na tuapizane na watoto wetu. Ni lazima tuwawajibishe wauaji hawa, ni lazima wajibu mashtaka ya mauaji haya na ni lazima wakati utakapofika Chama cha Mapinduzi kifutwe, viongozi wake wakuu na familia zao kupigwa marufuku kushika nafasi yoyote ya uongozi wa nchi, na mali zake kufisiliwa. Ni lazima tule yamini kuwa damu ya watoto wetu, mama zetu, vijana wetu ambayo imemwaga kihalifu hivi ni lazima ilipwe. Wao wamekula yamini na sisi tule yamini.
Nawaapiza!!