Baada ya kifo chake, Petro alizikwa mahali ambapo leo hii kanisa linalojulikana kama kanisa la Mt Petro limejengwa yaani huko Vatican Roma. Kinachotuthibitishia hilo ni kile kilichotokea mwaka 1939 hadi 1949 wakati kanisa hilo la Mt.Petro lilipokuwa likifanyiwa ukarabati. Wajenzi waliligundua kaburi lake na kwa uhakika wote walielewa kwamba ndilo hasa lenyewe walipokuta ukuta mwekundu wenye maandishi ya kigiriki yaliyosomeka, “PETROS ENI ” tafsiri yake kwa kiingereza ni“PETER IS INSIDE”,na kwa kiswahili,“PETRO YUMO NDANI”.
Mwaka 1950 siku ya Krismasi Baba mtakatifu Papa Pius XII alithibitisha hilo.Mambo haya ya kale sisi tunashindwa kuyaelewa kwa urahisi kwa sababu hatujihusishi sana nayo kama ndugu zetu wa nchi zilizoendelea wale wanaoitwa archeologists.
MWISHO NAOMBA UELEWE KUWA BABA MTAKATIFU AU PAPA NI NANI HASA
naomba nieleze kinagaubaga kuhusu Baba Mtakatifu au Papa ni nani, sawia na mamlaka yake katika Kanisa Katoliki.
Papa au Baba Mtakatifu ni wakili wa Yesu Kristo, Halifa wa Mtume Petro, Mkuu wa Kanisa Katoliki, Askofu wa jimbo la Roma, na Baba wa Kanisa la Magharibi ambalo kabla ya Mtaguso wa Mkuu wa pili wa Vaticano, lilitumia lugha ya Kilatini katika Ibada zake. Zaidi ya hapo Baba Mtakatifu ni Mkuu wa Jimbo la Kanisa la Italia na ni Rais wa Nchi ndogo ya Vaticani.
Kadiri ya Imani Katoliki, cheo cha Baba Mtakatifu kinatokana na ujumbe aliopewa Mtume Petro na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe. Mtume Petro, kufuatana na ushahidi dhahiri alikufa Roma, na kaburi lake liligunduliwa chini ya Altare kuu ya Kanisa la Mtakatifu Petro huko Roma.
Tukirejea kwenye sheria za Kanisa Katoliki ambazo ni ufafanuzi wa zile amri Kumi za Mungu, sheria namba 331, inasema hivi nanukuu; “Askofu wa Kanisa la Roma ambaye katika yeye inadumu ofisi iliyokabidhiwa na Bwana kwa Petro mwenyewe, wa kwanza katika Mitume na inayopaswa kupitishwa kwa Mahalifa wake ni Mkuu wa jopo la Maaskofu, wakili wa Kristo na mchungaji wa Kanisa zima hapa duniani; hivyo kwa dhati ya ofisi yake anayo madaraka ya kawaida, ya juu, kamili, yanayojitegemea, naya jumla katika Kanisa, ambayo anaweza daima kuyatumia kwa uhuru”. Mwisho wa nukuu. Pia sheria ya Kanisa Katoliki namba 333, inasema, nanukuu; “Baba Mtakatifu hupata madaraka kamili na ya juu katika Kanisa kwa njia ya uchaguzi halali alioukubali mwenyewe pamoja na kupewa uaskofu. Hivyo Yule aliye Askofu tayari hupata madaraka hayo tangu wakati anapokubali uchaguzi wake kuwa Baba Mtakatifu. Lakini kama Yule aliyechaguliwa hana uaskofu, anabidika kupewa uaskofu mara moja”. Mwisho wa nukuu, hata hivyo kifungu cha pili cha sheria hiyo namba 333, kinasema hivi, nanukuu, “Ikitokea kuwa Baba Mtakatifu anajiuzulu ofisi yake, ili iwe halali inatakiwa ajiuzulu kwa hiari na tendo hilo lidhihirishwe ipaswavyo, lakini si kwamba likubaliwe na yeyote”. Mwisho wa nukuu.
baada ya maelezo hayo mafupi kuhusu Baba Mtakatifu kama ni nani na wadhifa wake katika Kanisa Katoliki, naomba sasa twnde kwenye chimbuko la jina papa
chimbuko la jina hili Papa, hadi wakawa wanapewa viongozi hawa wa dunia wa Kanisa Katoliki, ni kwamba jina hili Papa ni neno la Kiitaliano ambalo limetokana na neno la Kigiriki Pappas, ambalo kwa kiingereza ni Fadher na Baba kwa lugha yetu ya Kiswahili.
Neno hili Papa lilitumiwa na Mapadre wa Makanisa ya Kigiriki. Na hapo ndipo sasa Mababa wa Kanisa Katoliki wakaona ni jina linalofaa apewe kiongozi wa dunia wa Kanisa Katoliki, yaani Baba Mtakatifu, kulingana na hadhi yake kama Baba wa Wakatoliki wote duniani.
Baba Mtakatifu ni kilele cha muundo wote wa daraja za Kanisa, na uwezo wote wa kimuundo katika Kanisa unatoka kwake, na hivyo tunaweza kusema ni sawa na Baba wa familia katika hali ya kawaida, kuwa yeye ni kichwa cha familia na anayo madaraka yote ya ndani ya familia ile. Ndivyo ilivyo kwa Baba Mtakatifu kama halifa wa Mtume Petro, Askofu wa Roma, wakili wa Yesu Kristo hapa duniani na mkubwa wa Kanisa Katoliki (rej. Mt 16:18-19; Yn 10:16). Nanukuu, “Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni”. Mwisho wa nukuu (rej. Mt 16:18-19).
Zaidi ya hapo, zamani hizo, jina hili Papa (yaani Baba), lilitolewa kwa Maaskofu, na lilitumiwa sana katika mzingo wa Kimonaki na likawa jina la kawaida kwa Mapadre wa Kanisa la Orthodoksi na pia Mapadre wa sehemu fulani za Kanisa Katoliki la Roma.
Na huko Misri jina hilo Papa lilikuwa ni haki ya Askofu wa Alexandria tu. Lakini kuanzia katikati ya karne ya sita (6th c), na kuendelea hadi hivi leo, jina hilo Papa limewekwa maalumu kwa ajili ya Askofu wa Roma tu, yaani kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Na utume huo uliwekwa kisheria na Baba Mtakatifu Gregori wa VII.
Sanjali na hilo kuna sababu za kimazingira kuwa Waitaliano ndiyo waliopokea mafundisho ya Mitume wenye sifa bora, nao ni Mtume Paulo na Mtume Petro ambaye alikuwa kiongozi wa Mitume na halifa wa Yesu Kristo. Inasadikika kwamba Mitume hao wakuu yaani Perto na Paulo waliacha mafundisho ya Yesu mikononi mwa Waroma na ndiyo maana mpaka leo hii makao makuu ya Kanisa Katoliki yapo Roma. Kutokana na mapokeo ya Kanisa sisi tunajua kwamba Mtume Petro kama kiongozi wa Kanisa la Roma alikamatwa na Mfalme Nero pamoja na Paulo Mtume na Wakristo wengine wengi.
Na baada ya kufungwa katika gereza la Mamertino, Petro alisulubiwa katika shamba la kuzikia lililokuwa katika ukingo wa mlima Vatikano mwaka Sitini na Saba (67), na hivyo Wakristo wa zamani walijenga kumbukumbu hapo.
Tena, mara baada ya Mfalme Mkuu Konstantino kutoa uhuru wa dini, Wakristo kwa msaada wa Kaisari huyo walijenga Kanisa la kwanza juu ya kaburi la Mtume Petro, wakiliacha kaburi chini ya Altare. Na kwa udhibitisho walichimba kwa miaka mingi chini ya Altare ya Kanisa la Mtume Petro, na mwisho wakafika kwenye kaburi lenyewe kwa kukuta maneno “Petro iki” yaani Petro yu hapa.
Ndugu ili kudhibitisha ukuu wa Kanisa la Roma mapokeo yanasema ;
Askofu wa Lione (Ufaransa), mwaka 115, Mt. Ireneo aliyekuwa mfuasi wa Mt. Polycarpi ambaye ni mwanafunzi wa Mtume Yohane, aliandika maneno yafuatayo katika kitabu chake kinachoitwa Dhidi ya Waasi sura ya II.
Nanukuu, “Mafundisho ya Mitume duniani kote yaweza kupatikana katika kila Kanisa, na kila mtu anaweza kuyapata, sisi tunaweza kuleta orodha ya Maaskofu waliopata cheo kutoka kwa mitume na mahalifa wao, mfuatano hadi siku hizi zetu. Lakini ingekuwa kazi ya kuchosha mno kuleta katika kitabu hiki mfuatano huo wa Mitume katika Kanisa. Ni bora nilete mapokea ya kitume na mafundisho ya imani ya Kanisa kubwa zaidi, ya zamani zaidi na lililojulikana kwa watu wote, ambalo liliwekwa kwa kimsingi huko Roma na Mitume wenye sifa bora, yaani Petro na Paulo. Kanisa hili limefika kwetu hadi leo kwa njia ya mfuatano wa Maaskofu na Mahalifa wao. Sasa basi kila Kanisa, yaani waamini wa duniani kote lazima wakubaliane na kushirikiana na Kanisa la Roma, kwa sababu ya cheo chake bora sana”. Mwisho wa nukuu.
Na zaidi ya hapo kuna uhakika kuwa mapokeo ya Mitume yanahifadhiwa huko Roma na baada ya Mitume waadhama kuweka misingi ya Kanisa la Roma na kuliongoza, uaskofu walipitisha wao kwa Linus kwa ajili ya uongozi wa Kanisa zima. Linus huyu ni Yule anayekumbukwa na Mtume Paulo katika waraka wake wa pili kwa Timotheo, (rej. 2Tim 4:21).
ndugu kutokana na ukweli huo kuwa misingi ya Kanisa Katoliki iliwekwa Roma na Mitume hao maarufu, yaani Petro na Paulo, bila shaka utakubaliana nami kuwa Waitaliano ni moja ya watu walioachiwa Kanisa na kuchukua jukumu la kuendeleza kazi ya uenezaji wa neno la Mungu duniani kote, kama ilivyokuwa ujumbe wa Kristo mwenyewe kwa Mitume wake.
Nanukuu, “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”. Mwisho wa nukuu (rej. Mt 28:19-20). Kwa udhibitisho wa hilo na mengi zaidi ya hayo nilio kueleza toka mwanzo unaweza kutafuta na kukisoma kitabu chenye kichwa cha habari PAPA NI NANI, kilichoandikwa na Padre Medri na Padre Magnus Lunyungu
From
SALA NA KAZI