[h=1]Mgogoro wa IPTL kuwatoa kafara mawaziri[/h]Na Mwandishi Wetu
MGOGORO wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), umepangwa kuwatoa kafara baadhi ya viongozi waandamizi wa kisiasa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mamlaka nyingine za utawala ndani ya serikali, Taifa Imara linachambua.
Imebainika kuwa baada ya malumbano kuhusu IPTL kukosa umwelekeo, mikakati imetayarishwa kuwatoa kafara baadhi ya wanasiasa kwa lengo la kutuliza mizimu inayotawala sakata hilo.
Kwa sasa swali linalotawala mjadala wa IPTL ni akina nani watakaotolewa kafara kati ya orodha ndefu ya watuhumiwa inayojumuisha mawaziri, makatibu wakuu, mwanasheria mkuu wa serikali na watendaji wengine.
Kafara si jibu la mgogoro wa IPTL
Wanasiasa wanapogeuka waleta mashitaka, Mahakimu na mabwana Magereza, huchochea migogoro kuendelea kushamiri badala ya kuipatia ufumbuzi. Katika sakata la IPTL baada ya malumbano kukosa mwelekeo, sasa wanatafutwa watu wa kutolewa kafara ili mizimu ya IPTL itulie. Eti wanatafuta mawaziri wa sekta husika na wengine waliopokea michango ya shule zao kuwa hao ndiyo vinara wa ufisadi.
Maswali ya kujiuliza, je kafara inatolewa ili serikali isianguke kama alivyotishia Zitto Kabwe, kwamba kashfa ya IPTL inaweza kuiangusha serikali? Je hizi ni mbinu chafu za makundi ndani na je ya serikali kuhakikisha wanaweka watu wao wanaowataka katika Wizara nyeti za Nishati na Ardhi? Au ni siasa za majitaka katika vita vya kuwania urais ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi? Orodha ya watuhumiwa ni ndefu. Swali ni nani na wangapi watatolewa kafara?
Kama waliotoa ruhusa fedha zichotwe na waliopokea "rushwa" ndiyo watatolewa kafara, je waliochukua fedha (kwamba ni zao) wataunganishwaje, kutokana kwamba haya ni masuala ya kugombea umiliki yako mahakamani na mwenye umiliki anagawa fedha zake, ni sheria gani ya kumzuia?
Na aliyepokea fedha kwa huduma aliyotoa au kwa ufadhili wa jambo fulani, kuna sheria gani ya kuzuia mtu au shirika lisipokee msaada?
Na hao wengine waliopokea wanahusikaje na maamuzi nje ya maeneo yao ya kufanya maamuzi.
Askofu au mchungaji anayepokea misaada anajua msaada alioupokea unatoka kwenye mikono michafu? Nalinganisha msaada kwa shughuli za kidini na msaada uliotolewa kusaidia shule kukamilisha majengo na maabara.
Kinachotafutwa hapa siyo ukweli wa mambo kuhusu chimbuko la kuhujumu uchumi kupitia kampuni ya kufua umeme ya IPTL, bali ni tamaa ya baadhi ya wabunge wanaotaka sifa na wengine ambao wanaendeleza vita vya makundi ya kutafuta urais ndani ya CCM na kwa kutumia baadhi ya wabunge kutoka vyama vya upinzani.
Watanzania wanakumbuka vizuri jinsi mgogoro wa Richmond ulivyozalisha mjadala wa ufisadi na kugeuza dhana ya ufisadi kuwa wimbo badala ya kuwa dhana ya kuchambua matatizo ya uadilifu na jinsi yanavyoathiri uongozi bora wa kisiasa na kijamii.
Kubuniwa kwa msamiati wa ufisadi kulifunika dhana ya rushwa. Dhana ya ufisadi ilitekwa nyara na makundi hasimu ya kisiasa ndani na nje ya Bunge na kulazimisha ubinafsishaji wa jinai badala ya ufisadi kutambuliwa kama kansa inayokula kiini cha uongozi bora katika jamii.
Katika mjadala wa Richmond, yalijadiliwa masuala ya kiufundi, menejimenti, ununuzi na ugavi na nani fisadi. Bunge lilitumia muda mwingi kujadili kashfa ya Richmond. Walitokea Makuhani na Makamanda wa kupambana na ufisadi ambao kila kukicha neno lao lilikuwa linapamba magazeti kwa vichwa vya habari motomoto. Ilikuwa burudani ya pekee.
Mwisho wa siku, mawaziri akiwemo Waziri Mkuu walitolewa kafara. Kashfa ya Richmond ambayo kimsingi iliwalenga watu, ilikufa kama ilivyobuniwa na hakuna anayejali suala hilo kupotea katika mjadala na malumbano ya kisiasa. Waliojipachika ukamanda wa kupambana na ufisadi sasa wamestaafu kazi hiyo. Historia umejirudia tena kama mzaha. Sakata la IPTL ni mkondo ule ule wa Richmond.
Miaka sita imepita sasa tangu sakata la Richmond liteke ulingo wa siasa. Baada ya Richmond kulitokea kashfa ya EPA na sasa tunacho kile kinaitwa kashfa ya IPTL.
Mjadala wa IPTL licha kwamba unayo mambo mengi, wahusika wengi, tuhuma nyingi na maeneo mengi; kinachojitokeza kama hoja kuu ambayo baadhi ya wabunge na vyombo vya habari ni akaunti ya ESCROW iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili fedha ambazo kampuni ya IPTL ilipaswa kulipwa ziwe zinawekwa baada ya wabia walioanzisha IPTL kuingia katika mtafaruku na kutofautiana. Serikali kwa kawaida haiweki pesa zake katika akaunti ya ESCROW.
Kisheria na kiuhalisia, fedha zilizoko kwenye Akaunti ya ESCROW ni za IPTL.Hoja zinazotolewa kwamba fedha za Akaunti ya ESCROW ni za serikali si za kweli. Ni propaganda za kisiasa ambazo mwisho wa siku hazimsaidii mwenezaji wa uongo huo. Kuonyesha kwamba wale wanaolivalia njuga suala la IPTL bila simile wanautazama mgogoro wa IPTL kama vile umeanza na kufunguliwa Akaunti ya ESCROW na fedha kuchukuliwa kutoka kwenye Akaunti hiyo. Hawahoji kwa nini Kampuni ya Mechmar ambayo ndiyo ilikuwa inafanya maamuzi yote yanayohusu kutafuta mtaji wa kuwekeza, kwa nini na kwa vipi madeni ya mabenki hayakulipwa ili kupunguza gharama za uwekezaji na hivvo hivyo kupunguza bei ya umeme kwa wateja.
Rekodi za TANESCO zinaonesha kwamba IPTL ililipwa dola za kimarekani milioni 190 kati ya mwaka 2002 mpaka 2006 wakati akaunti ya ESCROW ilipofunguliwa. Kiasi hicho cha pesa kilikuwa kinatosha kulipa kiasi kikubwa cha deni mpaka kufuta deni lote. Ujanja uliofanywa na wafanyabiashara wa Malaysia waliokuwa na hisa nyingi katika IPTL ni kubakiza deni lilivyokuwa ili waendelee kupata kiasi hicho hicho cha tozo ( capacity charge) kwa sababu deni halipungui.
Hata sasa wakati ambao Benki ya Standard Chartered inadai kwamba ilinunua madeni ya kampuni ya Mechmar ambayo ilikuwa inaimiliki IPTL, bado inadai kiasi cha dola za kimarekani milioni 150 bila kuonesha ni kiasi gani cha deni ilinunua na pia kwamba IPTL tayari ilishalipa dola za kimarekani milioni 54 kwa benki ambazo zilikuwa zimetoa mikopo ya kuanzisha mradi wa kufua umeme Tanzania. Ukimya unaoonyeshwa na Zitto na Kafulila kuhusu madhambi ya Mechmar na Benki ya Standard Chartered katika kuhujumu uchumi wa nchi kupitia kampuni ya IPTL unatia shaka kuhusu uzalendo wao na ukamanda wao wa kupambana na ufisadi.
Hoja nyingine ni kwamba fedha za Akaunti ya ESCROW siyo za mmiliki wa kampuni ya PAP ambaye ansema kwamba anamiliki IPTL mia kwa mia. Ni vigumu kujibu swali hilo kwani anayeuliza hawezi kutwambia kama anayesema ni mmiliki si mmiliki basi nani mmiliki? Kuna maswali ya Bunge na kuna maswali ya Mahakama.Suala la umiliki wa IPTL liko mahakamani na ni Mahakama ndiyo inaweza ikatamka huyu ndiye mmiliki.
Baada ya kuonekana kwamba kashfa ya IPTL haiwezi kamwe kuiangusha serikali, kama alivyokuwa ameonya Zitto Kabwe, mambo mapya yanaibuliwa ili kuweka wazi msimamo na kuendeleza malumbano. Kwa mfano kampuni ya VIP Engineering and Marketing ambayo ilikuwa na aslimia 30% katika IPTL. Kampuni ya VIP iliamua kuuza hisa zake kwa PAP. Kuna tatizo gani katika kuuza hisa? Na VIP iliamua kuwalipa watu mbalimbali ambao wametoa huduma za kisheria na pia kutoa mchango wa kusaidia jamii kama ujenzi wa shule na Maabara. Mwenye shule amekula rushwa gani au anahusika na maamuzi gani katika sekta ya Nishati, Benki Kuu na Wizara ya Sheria?
Ni wazi kwamba taasisi za serikali zenye wajibu na majukumu ya kuchunguza suala la IPTL zimekuwa katika wakati mgumu katika kutafuta ukweli. Ugumu huo unaongezeka kutokana kwamba suala hili limeingiliwa na wanasiasa ambao wanachotaka ni kumkamata mwizi.
Madai mapya kwamba kashfa ya IPTL ni ukwepaji kodi hayana maana. TANESCO imesema bado IPTL inaidai madeni ya mabilioni mpaka kufikia mwisho wa mkataba wao wa miaka 20 tangu 1995 mkataba wa kufua umeme uliposainiwa. Kuna fedha zilizobaki katika akaunti ya ESCROW. Kama hizo si za kulipa kodi ni za nini?