Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Pwani kutumia fursa za ubia na Serikali kuwekeza katika miradi mbalimbali ya miundombinu ya huduma za umma, badala ya kuiachia Serikali pekee jukumu la kugharamia miradi hiyo.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Kafulila alisema katika mazingira ya sasa ya maendeleo, si lazima Serikali ikope au kutafuta fedha za kujenga kila mradi wa huduma za kijamii na kiuchumi, ikiwemo maegesho ya magari, masoko, machinjio, majosho ya mifugo na hosteli za wanafunzi.
"Katika dunia ya leo, si lazima Serikali itafute au kukopa fedha za kujenga maegesho ya magari, masoko, machinjio, majosho au hosteli za wanafunzi. Hivi ni vitu ambavyo kwa kawaida kabisa vinaweza kujengwa na sekta binafsi, na wananchi wakalipia huduma wanazozitumia," alisema Kafulila.
Alifafanua kuwa hata pale ambapo Serikali ndiyo inayojenga miundombinu hiyo, wananchi hulazimika kulipia huduma hizo, hivyo hakuna sababu ya kutoshirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wake.
Kwa mujibu wa Kafulila, mfumo wa ubia unaipa Serikali nafasi ya kuelekeza rasilimali zake katika maeneo mengine muhimu ya maendeleo ambayo hayana mvuto mkubwa wa kibiashara, huku wawekezaji wakichangia maendeleo ya miundombinu yenye uwezo wa kujigharamia.
Aidha, alisema sababu nyingine muhimu ya kuhamasisha ubia ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Sababu ya pili ya kufanya ubia ni kuleta ufanisi. Sekta binafsi mara nyingi ina uwezo mkubwa wa kusimamia miradi na huduma kwa ufanisi zaidi, jambo ambalo huongeza tija na ubora wa huduma kwa wananchi," alisisitiza.
Kafulila alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Pwani kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi ya ubia, akieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.