Vigogo waanza kumalizana kimya kimya
HOFU imezidi kutawala kwa baadhi ya vigogo wa siasa, hasa kuwepo kwa taarifa za kulishwa sumu kwa baadhi ya vigogo na watu wanaoijua siri ya uanzishwaji wa Kampuni ya Kagoda Agricultural iliyochota sh bilioni 40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mmoja wa wafanyabiashara na wanasiasa maarufu hapa nchini (jina tunalo), anadaiwa naye kulishwa sumu na mwenzake ambaye inasemekana amekuwa na siri nzito kuhusu uanzishwaji wa kampuni hiyo, mahali fedha zilipopelekwa na matumizi yake.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha Tanzania Daima Jumapili, kimesema kupewa sumu hiyo kunatokana na hofu waliyonayo baadhi ya vigogo kuwa kuna uwezekano mkubwa baadhi ya watu wakatoa siri kuhusu uchotwaji wa fedha.
Hofu hiyo imeongezeka zaidi hivi sasa baada ya kuwepo kwa taarifa za wakili maarufu hapa nchini, Beredi Maregesi, wa Kampuni ya Maregesi Law Chambers kulishwa sumu kama ile anayodaiwa kupewa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), marehemu Daudi Ballali, aliyefariki dunia mwaka jana huku akikabiliwa na shutuma nzito za uidhinishaji wa fedha za EPA kwa kampuni 22.
Ballali ambaye alilazimika kukimbilia nchini Marekani kwa matibabu, inadaiwa aliwahi kueleza kiini cha kuumwa kwake kuwa ni kupewa sumu na mwanasiasa mmoja ambaye inadaiwa kuwa ni miongoni mwa watu waliochota fedha BoT.
Taarifa ambazo Tanzania Daima Jumapili, imezipata zinadai hivi sasa baadhi ya wanasheria walioshiriki au kujua siri za Kagoda wamekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya maisha yao, kutokana na mwenendo wa mambo ulivyo hivi sasa. Wakati wanasheria hao wakiwa na wasiwasi huo, kigogo wa siasa anayedaiwa kulishwa sumu hiyo inayofanya kazi taratibu, amekuwa akipata matatizo ya kiafya na huenda katika siku za hivi karibuni akapelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi, baada ya hospitali za hapa nchini kuonekana kutokuwa na uwezo wa kumtibu.
Chanzo cha habari kimedai kuwa kama kweli kigogo huyo atakuwa amelishwa sumu hiyo, uwezekano wa kupona ni mdogo, kwani sumu hiyo huenda mbali zaidi kwa kuingia kwenye mifupa.
Kama kweli amelishwa sumu ninayoijua, uponaji wake utakuwa mdogo, hata kama atapelekwa katika hospitali za nje, kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina lake.
Kigogo huyo inasemekana ndiye aliyekuwa na mipango imara ya kuwaokoa baadhi ya vigogo waliodaiwa kuhusika na Kampuni ya Kagoda ambayo katika siku za hivi karibuni wamiliki wake wametajwa lakini baadhi ya watu wanapinga kuwa si wamiliki halisi, bali ni kivuli cha vigogo wa siasa ambao walichukua fedha hizo kwa ajili ya kuwasaidia katika masuala yao ya siasa.
Baadhi ya wanasheria walio karibu na Maregesi wameweka bayana kuwa matumizi ya kijasusi, hasa ya kuwekeana sumu si mazuri na ni vema serikali ikachunguza madai hayo ili kubaini kama yana ukweli wowote kuliko kuyapuuza, kwa kudai kuwa huo ni uzushi.
Maregesi anadaiwa kuwa mtu wa karibu wa marehemu Ballali na anazijua siri nyingi, pamoja na mali za gavana huyo, jambo linalomfanya kuonekana mtu muhimu katika ushahidi endapo kampuni ya Kagoda ingefikishwa mahakamani.
Pamoja na wasiwasi huo wa kufikishwa mahakamani kwa Kampuni ya Kagoda, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, wamekwisha kuweka bayana kuwa hawajapata ushahidi wa kutosha wa kuweza kuifikisha mahakamani Kampuni ya Kagoda.
Kagoda ni miongoni mwa kampuni 22 zilizochota kiasi cha sh bilioni 133 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ambapo mpaka sasa watuhumiwa 20 na kampuni zao wameshafikishwa mahakamani, huku Kagoda iliyochota kiasi cha sh bilioni 40 ikiwa haijafikishwa mahakamani kwa kile kinachodaiwa kutokuwapo kwa ushahidi wa kuiburuza mahakamani.
Hawa TANZANIA DAIMA wameanza lini huu UPUMBAVU wa kutoa amnesty kwa criminals????? anayezungumzwa hapa ni rostam, wanajaribu kujenga sababu ili ionekane ana sababu ya kwenda nje ya nchi kwa kigezo cha matibabu, then baadae kdg iwe rahisi kupoteza idendities zake kama ilivyotokea kwa balali... nani atajua kama amekufa au hajafa????
Acheni ujinga huu!!