ZITTO azidi kuwaka, asisitiza Kagoda mali ya CCM
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, bado anasisitiza kuwa Kampuni ya Kagoda ni mali ya chama tawala CCM.
* Adai fedha ilizochotwa EPA zilitumika uchaguzi mkuu 2005
Na Kizitto Noya
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kukataa uhusiano wake na Kampuni ya Kagoda Agricultural Limited iliyochota zaidi ya Sh40 bilioni kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.
Zitto aliyekuwa anajibu mapigo ya CCM iliyomshutumu juzi kwa kuipaka matope kwa kuihusisha na Kagoda, alisisitiza kuwa CCM haiwezi kujivua gamba la Kagoda kwa kuwa ndiyo inayomiliki kampuni hiyo, ikiwa miongoni mwa kampuni 22 zilizochota jumla ya Sh133 bilioni katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
"CCM ndiyo inayomiliki Kagoda na Kagoda ni ya CCM. Fedha za Kagoda ndizo zilizotumika kwenye kampeni za CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Huu ndio ukweli," alilisitiza Zitto.
Alisema kauli ya chama hicho iliyotolewa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati kuikana kampuni ya Kagoda, ililenga kujisafisha lakini pamoja na jitihada hizo, ukweli utaendelea kubaki kuwa kampuni ya Kagoda ni mali ya CCM.
Kwa mujibu wa Kabwe, endapo CCM inataka kutakata inatakiwa kumruhusu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua hesabu zake za mwaka 2004/2005 na ieleze wapi ilipata fedha za uchaguzi mkuu mwaka 2005 uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani.
"Kama ni kujisafisha njia nzuri kwao si kutoa matamko, chama hicho kinatakiwa kumruhusu Mkaguzi Mkuu akikague na baadaye waseme fedha walizotumia katika uchaguzi mkuu mwaka 2005 zilizotoka wapi," alisema.
Alisema hakuna mantiki wala uhalali kuwaondoa mafisadi wa EPA katika uhusiano na CCM, kwani sehemu ya fedha iliyochotwa kwenye akaunti hiyo, zilitumiwa na CCM kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2005.
"Mimi nasema hii ni spinning (kupindisha ukweli), kama mtu amechota Sh40 bilioni na sehemu ya fedha hizo zikatumika kwenye uchaguzi wa CCM utawezaje kukiondoa chama hicho kwenye ufisadi huo?" alihoji na kuendela:
"Kama CCM wataweza kuthibitisha kwa ushahidi kwamba hawahusiki na ufisadi huo na kwa ushahidi wa taarifa ya mkaguzi mkuu kuhusu chama hicho, niko tayari kuwajibika na maelezo yangu," alisema.
Katika hatua nyingine Zitto alisema Chadema inatarajia kutoa tamko kuhusu kauli ya Chiligati kwamba vijana wanatakiwa kuacha kuifuatafuata CCM kwa kuwa walizaliwa wakaikuta ikiwa imara na watakufa na kuiacha ikiwa imara.
Alisema kauli hiyo ni hatari kwa usalama wa vijana wa aina yake wanaotetea maslahi ya umma hivyo chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lazima kitoe msimamo wake katika hilo.
"Labda nimalizie kwa kusema kwamba Chiligati anaposema sisi vijana tunaoifuata fuata CCM tutakufa na kuiacha CCM imara ni very serious. Kama chama (Chadema), leo (jana) tutaitolea tamko kauli hiyo kwani tunahisi wanataka kutuua," alisema.
Kabwe alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa tamko rasmi kuiruka kampuni ya Kagoda Agricultral Limited ikisema kuwa haina uhusiano nayo.
Chiligati aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa chama hicho hakina uhusiano wa aina yoyote na kampuni hiyo na kwamba hata kama kuna mwanachama anayehusika, ni suala lake binafsi na sio kwa mwavuli wa chama.
Tangu kuibuliwa kwa tuhuma hizo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiihusisha CCM na Kampuni ya Kagoda inayodaiwa kuchota Sh40 bilioni kwenye akaunti hiyo na miongoni mwa watuhumiwa wa EPA waliokwishafikishwa mahakamani, yumo Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Shaaban Maranda
Juzi Chiligati ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM alitoa tamko la kukisafisha chama hicho na kashfa hiyo akisema haina uhusiano wowote na wala hawaitambui kampuni ya Kagoda.
"Vita dhidi ya ufisadi na rushwa nyingine ielekezwe kwa mtu mmoja mmoja na siyo CCM kwani haiwezekani wana-CCM wote wakaenda benki kuiba fedha hizo pamoja," alisema Chiligati na kuongeza: "kampuni ya Kagoda haina uhusiano wa aina yoyote na CCM na wala CCM hatuijui".
Alisema kwa muda mrefu viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakifanya juhudi za makusudi kutaka kuihusisha kampuni hiyo na CCM na kutoa mfano kwamba, hivi karibuni Kabwe alinukuliwa akisema kwamba kuisha kwa suala la EPA kwa kiwango kikubwa kunategemea Kagoda itakavyochukuliwa hatua za kisheria.
Chiligati alisema Zitto pia alinukuliwa akisema kushindwa kwa serikali kuchukua hatua dhidi ya Kagoda kuna maana moja tu na kwamba kampuni hiyo ndiyo inayoijengea CCM Kaburi.
Katibu mwenezi huyo alisema shutuma zinazotolewa na Zitto na wapinzani wengine ni siasa zenye takataka zinazolenga kuipaka matope CCM na kwamba ni za uzushi na uzandiki.
Alisema CCM ni chama chenye kuheshimika, makini na safi, hivyo vijana wadogo iliowalea kuanza kukipaka matope ni kutafuta laana na njama zao hazitafanikiwa.