Haya baada ya kuwa na mji wa viwanda na biashara tic wanaongea 👇👇👇👇👇👇Mkoa wa Njombe ni mkoa unaokuwa kwa kasi kiuchumi hasa kupitia uwekezaji wa viwanda.
Miongoni mwa viwanda vinavyoleta mageuzi makubwa ni Avo Africa Tanzania Ltd, kiwanda cha kuchakata parachichi ambacho kimekuwa chachu ya maendeleo kwa wakulima na wananchi wa Njombe kwa ujumla.
Kiwanda hiki, kilichosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mwaka 2021, kimeleta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kutoa soko la uhakika kwa wakulima wa parachichi.
Wakulima zaidi ya 4,000 wamenufaika moja kwa moja kwa kuuza mazao katika mradi huu, huku wengine wakijipatia ajira katika kiwanda hicho.
Kupitia Avo Africa Tanzania Ltd, wakulima wa Njombe sasa wana mahali salama pa kuuza parachichi zao, wakihakikishiwa kipato endelevu.
Kiwanda hiki kinajihusisha na uzalishaji wa mafuta ya parachichi, bidhaa inayopata soko kubwa ndani na nje ya nchi. Kwa njia hii, thamani ya zao hili imeongezeka, na wakulima hawalazimiki tena kuuza parachichi kwa bei ya hasara.
Zaidi ya hayo, kiwanda hiki kimetengeneza fursa mpya za ajira kwa wakazi wa Njombe. Wafanyakazi wa viwandani, wasambazaji wa malighafi, na hata wajasiriamali wanaoendesha biashara zinazohusiana na uzalishaji wa mafuta ya parachichi wote wamenufaika kwa namna moja au nyingine.
Afisa Uwekezaji wa kanda hiyo Bi. Privata Simon amesema kuwa pamoja na mchango huo mkubwa kiuchumi mnamo mwaka 2024, Avo Africa Tanzania Ltd ilitunukiwa tuzo ya mlipaji bora wa kodi wa mwaka kwa mkoa wa Njombe.
Hii ni ishara kuwa mbali na kusaidia wakulima na wafanyakazi wa mkoa wa Njombe, kiwanda hiki kimechangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kupitia kodi na mapato mengine yanayotokana na biashara yake.