Kwa wale wanaolalamika au kutofurahishwa na CAG au ripoti yake, aidha kwa makusudi au kutokuelewa, ni kuwa ripoti ya CAG (hii na zilizopita) sio ripoti za kutunga, bali ni ripoti za yaliyojiri katika mwaka wa fedha husika, Julai 2019 hadi June 2020:-
1) Jukumu la kuandaa mahesabu ni la Taasisi, Wizara, Mashirika, Halmashauri husika halafu yeye CAG (na Ofisi yake) anatoa tu maoni/tathmini ya kitaalam (kikaguzi, kiufundi na kisayansi) juu ya alicholetewa. Ni kama vile wewe ukipeleka damu au choo maabara halafu mtaalam anapima na kukupa majibu kuwa kwenye damu/choo amekuta nini, sasa hapo kosa la Lab Technician ni kukupa mrejesho au?
2) Na ndio maana ukisoma ripoti hii utaona CAG alisema kuna mashirika/taasisi hazijapeleka hesabu kwake kwa ukaguzi na hivyo huoni maoni ya CAG kuwahusu. Kwa hiyo Ripoti ya CAG isijengewe mizengwe na hisia hasi ambazo hazina mashiko wala sababu. Wamemplekea mahesabu wenyewe (kwa mujibu wa Sheria zilizopo), na yeye kwa kutumia utaalam wake akathibitisha na kutoa majibu (kwa mujibu wa Sheria za Nchi).
3) Kuhusisha Ripoti na mambo ya mwendazake au hujuma nk nayo ni hoja mfu. CAG ameagizwa kwenye Katiba na Sheria za nchi kuandaa ripoti ya mwaka ulioisha wa fedha na kuikabidhi kwa Mh Rais (aliyeko) kabla ya tarehe 31 Machi kila mwaka na kwa Bunge la JMT. Kwa hiyo hakuna hila au njama kwamba labda hayati Rais wa awamu ya Tano, Joseph Magufuli angekuwepo angekabidhiwa? Ndio, maana hilo ni takwa la Kikatiba na Kisheria na muda wake ni sasa, sio suala la hisia au utashi wa mtu hapo.
4) Wengine wamefika mbali na kuuliza je kama Mwendazake angekuwepo nini kingetokea? Je CAG angekabidhi ripoti hii? Majibu ni kwamba kwa vile kila mwaka CAG (huyu na Assad) alikuwa anaandaa na kukabidhi ripoti basi yangetokea yale yale yaliyotokea miaka 5 iliyopita. Angekabidhi tu. Tofauti nayoiona ni pengine CAG asingekuwa na uwanja mpana na huru wa kusoma ripoti yake mbele ya Magufuli kama sasa kwa Rais Samia. Bali "angeelekezwa" cha kusoma, halafu "Kitengo" na wale wa propaganda wangeendelea kutokea hapo mara moja.
NB: Hivi mnakumbuka CAG Asssad alisomea wapi ripoti yake ya mwisho? Mnakumbuka mazingira ya ndani na nje ya Bunge kumhusu CAG na Ripoti yake? Sasa ikiwa Rais na Bunge walikuwa "hostile" kiasi kile kwa nini leo idhaniwe kuwa CAG ana lake jambo au kuna mkono wa mtu nyuma ya ripoti hii?
5) Hayati Magufuli alipenda na alipewa sifa nyingi mno kwa namna ya uongozi wake, kauli zake, miradi na yote aliyoyafanya (mema na mabaya). Sasa kwa vile kanuni za maisha zinasema kila shilingi ina pande mbili, na kila kitu kina kinyume (opposite); basi kwa kadiri alivyopenda na kupokea sifa, basi kwa kadiri hiyo hiyo anastahili na atapokea lawama na hukumu ya haki katika yote aliyoyasema na kufanya. Ni haki na ni sahihi. Kuna hotuba yake aliwahi kusema hivi (NAMNUKUU):-
"....Hela ya Serikali haipotei...anaweza kupotea binadam lakini hela haipotei (kicheko/makofi).....
Na katika kipindi changu hela ya Serikali haipotei (makofi zaidi).....Na nasema ukweli kabisa, HAITAPOTEA...."
kadiri Hivyo basi, kwa kauli, ahadi, haiba na matendo yake anastahili kupokea mzigo huu, na wa mwaka 2020/21 utakaokuja mwakani.
6) Katika miaka yote ya utawala wake kama Rais wa Tanzania, sikuwahi kusikia wasaidizi au washauri wake wakisifiwa wazi wazi lakini yeye alisifiwa mara zote na mahali kote, ndio tena sana tu! Sasa kwa nini mnataka wakati wa lawama na adhabu yeye apate kidogo? Ni uhalisia tu, wanaita natural course.
Hayati Magufuli aliwahi kusema yeye hashauriki....na mtu akimshauri ndio ameharibu kabisa.... sasa je hao "washauri" mnaowatuhumu leo ni akina nani? Yaani kivipi labda?? Au hamkuwa mnamsikiliza na kumwelewa hayati alichosema? Hataki ushauri. PERIOD!
Alifika mahali akasema yeye ni mwamba, jiwe, mgumu....hatishwi, hatishiki nk hizo kauli na matendo yake ndio vinaakisiwa na ripoti ya CAG. Yaani ni boga na ua lake.
Ukisoma ripoti ya CAG inataja "nika..." "mimi" "nili.." nk - CAG anafanya kitu kinaitwa uwajibikaji na haki. CAG atabeba lawama zote au atabeba sifa zote za Ripoti hii (ingawa ni timu ya wataalam wa Ofisi yake na nje waliondaa ripoti). Aliyeapa na kupewa mamlaka ndiye anayewajibika kwanza kisha wa chini yake, hivyo tusilete ngonjera na sarakasi, mhusika mkuu ni Rais wa Awamu ya Tano. Wengine wanafuatia.
Maana yake baada ya hayati Magufuli, wote waliohusika (moja kwa moja au kwa maelekezo yake) nao watawajibika, na nasisitiza wanapaswa kuwajiba WOTE.
7) Kwa nini, nauliza tena kwa nini.....
a) Magufuli alichukia kukosolewa yeye au Serikali yake?
b) Kwa nini alikataa na kuua transparency governance ambayo ni msingi wa good governance?......
c) Kwa nini alifanya mambo gizani? Kwa mfano alinunua ndege kinyume cha Sheria za Nchi na kinyume hata cha biashara ya ndege (aviation industry) ya ndege duniani. Tena alinunua CASH! Hapo anakwepaje lawama? Akateua Bodi ya Wakurugenzi wasiokuwa na ujuzi wala uzoefu na biashara ya usafiri wa ndege! Anakwepaje lawama hapo? Hizo ndege alishauriwa lakini hakusikia....hivi mnaojaribu kumtetea hayati huwa wanawazajewazaje lakini?
NB: Kwenye ripoti hii ndio nimesoma kwa mara ya kwanza, rasmi, kwamba ndege 8 zilinunuliwa kwa Shs 1 Trillion na ushee! Yaani ndege 1 kwa wastani wa Shs 125 Billion! Where is the value for money there? Was it a national priority? Isn't he accountable and guilty?
d) Kwa nini alichukia uhuru wa vyombo vya habari? Kwa nini aliminya na kusigina Katiba na Sheria za nchi katika kutekeleza matakwa yake aliyoyaita "maono" "sacrifice"?
e) Kwa nini alikuwa jeuri na mbabe mbele ya mihimili mingine ya dola? Kwa nini alikiuka sheria za manunuzi na miongozo mingine yote kuhusu miradi na uendeshaji wa Serikali?
f) Kwa nini alidanganya kuwa miradi inajengwa kwa fedha za ndani ilihali alikuwa anakopa- aliingia deni la Taifa likiwa Trilioni ngapi na ameondoka likiwa Trilioni ngapi?
g) Kwa nini aliendesha nchi kwa propaganda, uongo, vitisho na uhalifu???
h) Kwa nini hakulipa mishahara, posho, kupandisha madaraja watumishi wa Umma kwa muda wote wa utawala wake? Na kwa nini alipenda kuogopwa? Na kwa nini hakuona kuwa kimya hakimaanishi utii, na wafanyakazi wenye motisha ndogo ya kazi hawawezi kuzalisha kwa tija wala kutoa huduma bora kwa mwajiri?
i) Kwa nini alijaza watu wake wa karibu au wenye nasaba za ukabila au ukanda (upendeleo) kwenye nafasi nyingi za juu kuanzia Serikali kuu, Mashirika mpaka Serikali za Mitaa???
j) Kwa nini alipinga siasa za ushidani? Kwa nini alitesa, kupoteza na kutisha wapinzani wake wa kisiasa? Na alienda mbali mpaka akaharibu chaguzi za 2019 S/Mitaa na 2020 Uchaguzi mkuu?
Kwa nini alisababisha hasara, maumivu na usumbufu wote ule kujaribu kuhalalisha utawala wa kiimla ili kuendeleza na kuficha mambo kama yalivyoibuliwa na CAG??
8) Kwa haya yaliyotokea katika siku hizi 24,tangu kifo cha Magufuli, kuingia kwa Rais Samia na sasa Ripoti ya CAG - tumepata majibu yote ya maswali magumu yaliyotusumbua kwa miaka mingi. Pengine hapatakaa paweko na siku 24 za aina hii katika historia ya maisha yetu na ya taifa letu Tanzania. Yako mengi sana yaliyojitokeza na tunayopaswa kujifunza. Leo nitaangalia machache tu:-
a) Tatizo la nchi yetu ni nini hasa - ni CCM na Ujamaa, mtawalia.
Mniwie radhi niseme, Ujamaa ni sera ovu iliyo kinyume cha maumbile ya fikra na mifumo ya uzalishaji mali wa binadam. Kama unabisha soma critical history ya nchi na falme za ulimwengu toka Adam mpaka sasa. Sio suala la hisia au mapenzi, ni factuality. Ni realities za maisha ulimwenguni humu.
b) Kwa nini rushwa,ufisadi, maradhi, ujinga na umaskin vimeendelea kutusumbua kama nchi maiaka yote 60 ya Utaifa wetu? - ni kwa sababu ya ubovu na udhaifu wa katiba yetu ya sasa. Msingi wa utawala bora ni Katiba nzuri. Msingi wa Uongozi bora ni Katiba nzuri. Hapo ndio pa kuanzia kuweka tofali la kwanza la ujenzi mathubuti. Viraka viraka na hila ndio vimetupa matokeo tuliyo nayo hadi sasa, tukibadilika na kubadilisha, basi matokeo nayo yatabadilika. Tukiktaa tutabaki hapo hapo.
c) Siasa chafu. Hili halihitaji maelezo wala ufafanuzi, Awamu ya Kwanza mpaka ya Tano, siasa hazikuwa safi, zina hila na unafiki mwingi. Tujirekebishe sasa.
Kwa kumalizia, naomba Rais wa JMT Mh Samia afikiri na kutenda nje ya mfumo na utamaduni wa kulindana wa CCM. Aweke Taifa mbele, hata kama itamgharim yeye kupendwa chamani sisi wananchi wazalendo wa Tanzania tutampenda na kumuunga mkono na atafanikiwa kuliko watangulizi wake wote, ili tuondoke hapa kwenye tope na mkwamo uliojaa kashfa, umaskin na ufisadi mfano wa donda ndugu.
Niwe wazi tu. Suala la hayati Magufuli kuwa na wafuasi na mashabiki (fans and sympathizers) ni la kawaida, sio jambo geni. Historia inaonyesha hata Hitler, Mao, Mussolini, Stalin, Mobutu, Saddam, Idi Amini na wengine kama hao, nao pia walikuwa na wafuasi na wapambe, si kidogo. Walikuwa wema kwa walio wao (waliofadika nao tu), lakini waliharibu nchi na mataifa yao na ulimwengu kwa ujumla. Tuwapuuze. Tutazame mbele, kuijenga Tanzania bora kwenu na vizazi vijavyo.
Mungu Ibariki Tanznia, Mungu Mbariki Rais Mama Samia atende haki, mpe hekima na upendo na pia umlinde ili aongoze Taifa letu hili kipindi hiki kigumu cha mpito! Mungu Ibariki JF na watu wote waliosimama na kuhatarisha maisha yao kupambana na waovu, maonevu na dhuluma za Awamu ya Tano, ambao kwa namna moja au nyingine wameisaidia nchi yetu na kuvuka salama kuelekea kwenye ustawi na mafanikio, hao ni watumishi wako! Lakini usiwaache wanafiki na watesi wetu bila adhabu, ili wajifunze kutokudhihaki... lakini pia wajue kuwa Wewe ni Mtakatifu na unapenda haki, uwape kutambua na kutubu kisha wajifunze kupenda kweli na kujua kuwa hapa duniani sisi ni mawikili Wako tu na wapitaji, kama baba zetu. Tutende haki, tutende mema, tusiwe wanafiki. Amen.