Mzalendo_Mkweli
JF-Expert Member
- Jan 30, 2012
- 2,025
- 1,270
SIJUI ni lini tutaacha kutumia siasa katika vitu vya msingi. Nawaza sana juu ya hili lakini sijapata majibu.Ni wiki moja sasa imepita tangu sakata la mchezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ limalizwe kisiasa na kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Fei Toto alivunja mkataba wake na Yanga. Aliandika barua ya kuwafahamisha Yanga kuwa ‘ndoa’ yao imevunjika. Akalipa na fedha za kuvunja huo mkataba.
Yanga wakaenda TFF kulalamika kuwa Fei Toto amevunja mkataba bila kuwashirikisha. Walikuwa na haki ya kushtaki kuhusu sakata hilo. Yawezekana ni kweli Fei Toto alivunja mkataba bila kuwashirikisha Yanga. lakini ukweli ni kwamba aliwafahamisha.
Kwanini Kamati ya TFF haijaamua kesi ya msingi na badala yake wamemlazimisha mchezaji arudi Yanga? Inachekesha sana.
Kwa kifupi ni kwamba mkataba wa Fei na Yanga ulishavunjika. Ndio maana Yanga ililalamika mkataba umevunjwa bila utaratibu. Hii ndio ilipaswa kuwa kesi ya msingi. Lakini badala yake imeamuliwa kesi nyingine kabisa.
Wewe uliona wapi duniani mchezaji analazimishwa arudi kwenye timu yake ya awali baada ya kuvunja mkataba?
Kama ulisoma vizuri mkataba wa Fei Toto na Yanga umeeleza wazi kuwa upande wa mchezaji unaweza kuvunja mkataba muda wowote kwa namna isivyo kawaida kama utafuata utaratibu wa Malipo.
Fei Toto alifanya hivyo. Aliwalipa Yanga fedha ya usajili na mishahara ya miezi mitatu. Hiki ndio kipengele cha wazi katika mkataba wake na Yanga.
Kamati imetumia kipengele gani kumrejesha. Hakuna. Ni siasa tu. Ama wanaogopa kuwa watu watasema kuwa wanaionea Yanga? Ni ajabu na kweli. Kwanini tusiamue vitu vya msingi kwa kufuata utaratibu?
Kama mkataba unasema namna ya kuvunja huwa tunatumia mkataba kufanya hivyo. Hakuna sehemu imeandikwa kuwa tunatumia sheria za FIFA kwa kesi ambayo mkataba wake unazungumza namna ya kufanya.
Mkataba wa Fei na Yanga umesema vyema namna ya kuvunja. Na mchezaji ametumia vipengele hivyo kuvunja mkataba wake na Yanga. Lipa wazi kabisa.
Kwanini TFF haikujadili kesi ya msingi ya mchezaji na Yanga ikaamua tu kumrudisha mchezaji kwenye klabu? Uliwahi kuona wapi jambo kama hili?
Yanga walilalamika kuwa Feisal amevunja mkataba bila kuwashirikisha. Ila ukweli ni kwamba Feisal aliwaandikia barua kuwafahamisha. Walitaka nini zaidi ya hicho wakati mkataba unaeleza wazi ukitaka kuvunja unafanya nini?
Walitaka Fei Toto afanye kitu gani kingine? Ni kichekesho. Kimsingi ni kwamba hadi Yanga na Fei Toto wanakwenda pale TFF mkataba ulishavunjika. Haikupaswa kujadiliwa tena kama Fei ni mchezaji wa Yanga ama la. Ila cha ajabu imejadiliwa hivyo.
Kilichopaswa kujadiliwa ni kama Feisal alikosea popote wakati anavunja mkataba wake huo. Utaratibu unafahamika kuwa ni faini ama adhabu ya kufungiwa. Huu Ndio muafaka wa kisheria. Kwanini hawakutaka kufanya hivyo? Wanajua wenyewe.
Unajua Madhara ya maamuzi haya? Subiri nitakueleza. Kwa namna hali ilivyo sasa Feisal hataki tena kucheza Yanga. Hataki kabisa. Ni kama tu mwanamke aliyeomba talaka kwenye ndoa. Kumlazimisha Feisal arudi Yanga ni kama kumlazimisha mbuzi ale mkate. Ni jambo gumu sana.
Matokeo yake ni kuwa Feisal anaweza kuendelea kucheza Ndondo kwao Zanzibar hadi mwisho wa msimu. Nini kitatokea? Tunapoteza mchezaji Muhimu katika Ligi yetu Pamoja na Taifa Stars.
Sote tunakubaliana kuwa Fei ni mchezaji mahiri zaidi katika nafasi anayocheza hapa nchini. Hana mfanano. Hakuna anayemkaribia hapo.
Hivyo kama Taifa tumeweka rehani kipaji cha mchezaji mkubwa kwa kutumia siasa. Inauma sana.
Source : Mwanaspoti