Bashe atimuliwa CCM
Adaiwa raia wa Somalia, afananishwa na Ulimwengu
na Martin Malera, Dodoma
HALMASHAURI KUU ya Chama cha Mapinduzi (NEC), imemvua nyadhifa zote na kumfukuza uanachama kada wake maarufu, Hussein Bashe, baada ya kubaini kuwa sio raia wa Tanzania.
Bashe ambaye alishinda kura za maoni kwenye jimbo la Nzega lililokuwa likishikiliwa na Lucas Selelii, (CCM), pia alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).
Akitangaza uamuzi huo juzi majira ya saa 11 alfajiri baada ya kumalizika kwa kikao cha NEC cha mchujo wa wagombea ubunge na Baraza la Wawakilishi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kapteni mstaafu, John Chiligati, alisema CCM imeamua kumtimua Bashe uanachama na kumuengua kuwania ubunge katika jimbo la Nzega, baada ya kubaini kuwa ni raia wa Somalia.
Alisema uchunguzi uliofanywa na chama hicho kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, umebaini kuwa Bashe licha ya kuzaliwa nchini, ni raia wa Somalia na hajaukana uraia wake.
Bashe sio raia wa Tanzania, alikuwa akiishi kwa mazoea tu. Tulipojaribu kutafuta uraia wake kwa kuwashirikisha watu wa Uhamiaji, walituthibitishia kuwa sio raia, licha ya kuzaliwa nchini na alikuwa akiishi kwa mazoea tu. Hii ni kama iliyowahi kumtokea Jenerali Ulimwengu na ndivyo ilivyo kwa Bashe, alisema Chiligati.
Akifafanua suala la uraia wa kada huyo wa CCM, Chiligati alisema Bashe alizaliwa nchini, lakini baba yake ambaye hata hivyo hakumtaja jina, alihamia nchini na kuukana uraia wake miaka 10 baada ya Bashe kuzaliwa.
Alisema licha ya kuwa baba yake alichukua uraia wa Tanzania, Bashe naye anapaswa kusaka uraia wa Tanzania, kwani kisheria haruhusiwi kurithi uraia wa baba yake.
Alipoulizwa kwa nini suala la uraia wa Bashe limeibuka kipindi hiki alichoshinda kura za maoni katika jimbo la Nzega wakati amewahi kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Chiligati alisema safari hii chama hicho kimepokea malalamiko rasmi kutoka kwa mmoja wa washindani wa Bashe (hakumtaja jina), alidai kuwa kada huyo sio raia.
Kama nilivyosema, alikuwa akiishi kwa mazoea, lakini safari hii tumeletewa malalamiko, tukayapeleka Uhamiaji, wakabaini kuwa kweli sio raia, tukaamua kumkata na kumvua nyadhifa zake pamoja na uanachama hadi hapo atakapoweka mambo yake sawa, alisema Chiligati.
Msemaji huyo wa CCM alisema mbali ya Bashe, NEC pia ililetewa malalamiko dhidi ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, Mbunge wa Kilosa kwamba naye ni raia wa Malawi.
Kama ilivyokuwa kwa Bashe, tulipeleka suala hilo uhamiaji nao walipofanya uchunguzi, walibaini kuwa ni madai ya uongo. Kama ingekuwa kweli, tungechukua hatua kama tulivyochukua kwa Bashe, alisema Chiligati.
Kutokana na hali hiyo, Chiligati alisema CCM imempa muda Bashe kuweka mambo yake sawa ili aweze kuwa raia wa Tanzania, arudishiwe uanachama wake na kupata fursa ya kushiriki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi nchini.
Alipoulizwa kwa nini NEC haikumpitisha Selelii aliyeshika nafasi ya pili Nzega, Chiligati alisema Mbunge huyo wa zamani wa Nzega hakubaliki, kwani alipishana kwa kura chache sana na mshindi wa tatu, Hamis Andrea.
Kuhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Nchini (TFF), Chiligati alisema NEC imezingatia zaidi suala la maadili kwani ni sawa na mchezaji aliyepigiwa kipenga katika dakika ya kwanza ya mchezo wa soka.
Mwakalebela ambaye alishinda kura za maoni katika jimbo la Iringa Mjini, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, akidaiwa kutoa rushwa wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Alipoulizwa kwa nini Mbunge wa Bariadi Mashariki Andrew Chenge na Bazil Mramba wa Rombo, wamepitishwa kutetea nafasi zao wakati wanakabiliwa na kesi za matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyo kwa Mwakalebela aliyedaiwa kutoa rushwa, Chiligati alisema wamezingatia maoni ya wanasheria kuwa kesi zao haziwezi kuathiri uteuzi wao.
Chenge bado anatuhuma na hajafunguliwa kesi, Mramba ana kesi ya matumizi mabaya ya madaraka, nayo haiwezi kuathiri uteuzi wake. Mwakalebela ndio kwanza anaanza na rafu na kapigiwa filimbi ndani ya dakika ya kwanza, hapo tumeangalia maadili zaidi, alisema Chiligati. Katika hatua nyingine, Bashe aliliambia Tanzania Daima jana kuwa anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, akiwa na vielelezo vinavyoonyesha kwamba ni raia wa Tanzania.
Source: Tanzania Daima.