Na. Robert Lengeju
Morogoro Vijijini.
Mwenyekiti wa muda wa Bunge maalumula katika, Pande Ameir Kificho ameunda tume maalumu ili kuchunguza, kujadili na baadaye kutoa maoni na ushauri kwa Serikali, kama posho ya shilingi milioni Tisa kwa mwezi inatosha au haitoshi. Kamati hii bila shaka itapewa bajeti yake, si ajabu nikasikia hata wamesafiri kwenda Namibia kuona kule wabunge wa Bunge maalumu la katiba walilipwa kiasi kiasi gani. Huu mzaha na matusi ya nguoni kwa mtanzania anayeishi chini ya dola moja!
Taasisi kadhaa ikiwepo Jukwaa la katika, tahariri za magazeti, taasisi za kiraia na wananchi kwa ujumla wametoa kauli zinazoonyesha wamekasirishwa na tama ya watanzania wenzao, ambao juzi walikuwa wanaishi wote chini ya dola, na leo kwa "cheo cha ubunge" ghafla laki tatu haziwatoshi!Naungana na watanzania wote wenye mapenzi mema kulaani kwa kiwango cha juu mno mwenendo huu ulioanza kuonyeshwa mapema mno na hawa tunaoatarajia watuletee katiba mpya.
Nimeshtushwa sana kusikia majina ya walioteuliwa kuingia kwenye hiyo tume haramu. Naiita tume haramu kwa sababu kisheria, mjadala wowote ambao mada yake ni uhalifu, ni mjadala haramu. Wajumbe wa kamati hii haramu ni Freeman Mbowe, William Lukuvi, Jenester Mhagama, Paul Kimiti,Asha Baka Makame na Mohamed Aboud. Sikusahau kuwataja kwa kuanza na Mheshimiwa, nimeondoa makusudi sifa hiyo kwani kwa kukubali kwao kuwa wajumbe wa kamati haramu mimi nimewaondolea sifa hiyo na wakieendelea na mjadala wanaendelea kuporoposha hadhi yao mbele ya jamii. Hapa ndipo ninapowakumbuka wanasiasa wa Kaliba ya Dr.Wilbroad Peter Slaa, Mh.James Mbatia, Mh. ZittoKabwe na Mh. Deo Filikunjombe. Nina uhakika, yeyote kati ya hawa angeteuliwa katika kamati ya namna hii wangekataa uteuzi huo.
Hoja yangu ni hapa ni hii, kwamba suala hilo halihitaji mjadala wala tume. Wale wanaaaona hiyo pesa haitoshi waache hiyo kazi, wapewe watu wengine. Wako huku mtaani watu wenye weledi na uchungu na nchi hii, ambao wanaweza kufanya hiyo kazi kwa kuhakikishiwa usfiri, chakula na malazi pekee, na wengine kwa kujitolea kabisa. Hii nchi imeshateswa na kujeruhiwa mno na sanaa hizo zinazoitwa ‘tume'. Hivi kuna haja ya kuunda tume kwa mfano, ya kujadili kama wabunge waruhusiwe kuvuta bangi bungeni? Kuna haja ya kuunda tume ya kujadili kama wabunge waingie bungeni bila nguo? Ikiundwa kamati ya namna hiyo nawe ukakubali uteuzi wake tukuweke kundi gani? Ni kwali tunahitaji mjadala kujua bangi inafaa au haifai?
Tumewapeleka bungeni kujadili rasimu na kutuletea pendekezo la katiba bora, na juzi ilikuwa siku ya kutunga kanuni za hilo bunge, ninyi mnaacha kutunga kanun, kazi tuliyowatuma, mnaunga kamati za kuongezana posho? Mungu awalaani. Juzi tu tulikuwa wote katika harakati za kudai vitanda viongezwe kule Amana kwakuwa wajawazito 12 wanachangia kitanda kimoja na wengine wakilala chini, leo nyie laki tatu ni vijisent?
Hivi hamjui hapo Dodoma kuna walimu wanalipwa 170,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na 5,500 kwa siku? Hamjui kuwa nchi hii ina machinga wanaozunguka mkoa mzima na kuambulia kuuza chupi ya 700 kwa siku? Hamjui kuwa kuna wenye akili timamu lakini wameamua kuokota makopo yanayowapatia ujira wa 1,000 kwa siku? Hivi mmetembelea soko la Dodoma muone wamama wanaouza bamia, hoho na sukumawiki ambao pato lao kwa siku ni shilingi 2000 huku wakiendesha familia? Hebua acheni unyang'anyi huo……..
MBOWE NA WENZAKO VUNJENI HIYO KAMATI KABLA NGUVU YA UMMA HAIJAWARUDIA WENYEWE! HAMNA MAMLAKA YA KUJADILI NAMNA YA KUWANYONYA WANANCHI!