Uongozi wa Kampuni ya China Tanzania Security umetoa ufafanuzi kuhusu madai ya Mwanachana wa JamiiForums.com aliyeandika kuwa wafanyakazi wa ofisi hiyo ambao ni Walinzi wanaosimamia Vituo kadhaa vya Usafiri wa Mabasi ya Mwendokasi hawajalipwa mishahara kwa muda wa miezi mitatu na kuwa wakidai hawapati majibu ya kueleweka.
Mwanachama huyo alieleza kuwa mbali na hali hiyo kumekuwa na changamoto nyingine mbalimbali ikiwemo Wafanyakazi kutosikilizwa na kutojaliwa inapotokea wanapata changamoto wakiwa kazini.
Kusoma zaidi alichoandika Mdau huyo, bonyeza hapa ~ Walinzi tunaosimamia Vituo vya Mwendokasi hatujalipwa mshahara kwa miezi mitatu, tukifuatilia tunapigwa danadana
Ufafanuzi wa CHINA TANZANIA SECURITY
Administration Officer wa Kampuni hiyo, Pascal Temba amezungumza na JamiiForums na kufafanua hoja zilizowasilishwa na Mdau kwa kusema:
Kuhusu suala la Mshahara ambayo wanadai ni ya miezi miwili na siyo mitatu, hiyo inatokana na changamoto ambayo tunapitia ambayo inaweza kutokea katika ofisi yoyote ile.
Suala hilo kwanza halijawahi kutokea huko nyuma nadhani hata kwenu hii itakuwa taarifa ya kwanza kuhusu sisi inayozungumzia mishahara.
Suala la Mikataba siyo kweli kuwa hawana mikataba, yote iliyopo ni Mikataba ya maandishi.
Jambo lingine ni kuwa ofisi inashughulika na changamoto nyingine kadhaa za Wafanyakazi kuanzia mtu mmojammoja, na sio kweli kuwa malalamiko yao hayashughulikiwi sio kweli, naomba niweke vizuri kuhusu hilo.
Pamoja na suala hilo la mishahara lakini masuala ya nidhamu bado yanasimamiwa vizuri, unaweza kukuta kuna mfanyakazi anaanza kukiuka taratibu kwa kutofika kazini, mtu anapochukuliwa hatua za kinidhamu anaweza kwenda mbele na kuzungumza vitu vingine ambavyo havipo.