Katika miaka ya karibuni, China na Afrika zimehimiza ushirikiano wao katika sekta mbalimbali kwa njia ya kiuvumbuzi, mfano ukiwa ni karakana ya Luban, ambayo imekuwa alama ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika mafunzo ya ufundi stadi.
Karakana ya Luban ni sehemu ya ushirikiano kati ya China na Afrika wa kujenga uwezo katika Hatua Nane zilizopendekezwa na China kwenye Mkutano wa mwaka 2018 wa FOCAC, ambapo lengo lake ni kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa Afrika.
Karakana hizo zinazingatia sekta zinazohitajika zaidi na nchi za Afrika zikiwemo reli, mashine, umeme, viwanda, magari, habari, madini, biashara ya mtandaoni, na akili ya bandia, na hadi sasa imewafundisha vijana zaidi ya 10,000 barani humo.
Dickson Esamai pamoja na wenzake wanafanya kazi kwa bidii katika uvumbuzi wa kilimo kwenye Karakana ya Luban iliyoko katika Chuo Kikuu cha Machakos, umbali wa kilomita 65 kutoka mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Dickson, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano anayesomea shahada ya kwanza katika ufundi wa kielektoniki na uhandisi, anatengeneza kifaa ambacho kitawasaidia wakulima kuongeza mavuno yao.
Katika mahojiano na Shirika la habari la China, Xinhua, Edson anasema wanajenga kifaa kitakachowaongoza wakulima kutambua zao sahihi la kulima kwenye ardhi yao kutokana na virutubisho vilivyopo kwenye ardhi hiyo. Kifaa hicho kinachoweza kubebwa mkononi kina uwezo wa kuhisi unyevu katika ardhi na hivyo kuwasaidia wakulima kupata kiasi sahihi cha maji kwa ajili ya mazao yao, na kwa njia hiyo, kuhifadhi rasilimali ya maji.
Ili kuongeza matumizi yake kati ya wakulima wadogowadogo ambao hawana simu janja, kifaa hicho pia kinaweza kutume ujumbe wa simu unaotoa taarifa muhimu kwa ajili ya shughuli za kilimo. Esamai anasema, kifaa hicho kilibuniwa na kutengenezwa toka mwanzo kutokana na vifaa vya kisasa vinavyopatikana katika Karakana ya Luban.
Tangu kuzinduliwa kwa karakana ya kwanza ya Luban nchini Djibouti mwezi Machi mwaka 2019, China imejenga karakana 17 za Luban katika nchi 11 barani Afrika, zikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Mali, Nigeria, Misri, Uganda, Côte d'Ivoire, Madagascar na Ethiopia, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kimataifa wa ufundi stadi ndani ya mfumo wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Desemba 5, mwaka jana, Chuo Kikuu cha Machakos na Chuo cha Ufundistadi cha Mji wa Tianjin vilisaini makubaliano ya miaka mitatu ya kuboresha nafasi ya Karakana ya Luban, na chini ya makubaliano hayo, pande hizo mbili zitaongeza usajili katika karakana hizo nchini Kenya ili kuongeza ujuzi wa kidijitali nchini humo.
Kwa sasa, Kenya ina karakana mbili za Luban, moja ipo Chuo Kikuu cha Machakos na nyingine iko katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru, ambacho kiko kilomita 280 kutoka jiji la Nairobi.