Yanga: Tulimsajili Kondo wa Simba usiku
KAMATI ya Usajili ya Klabu ya Yanga, imekamilisha maumivu mengine kwa watani wao Simba, baada ya kumalizana na straika aliyekuwa njiani kutua kwa Wekundu hao, Shaban Kondo, lakini bosi mmoja wa Yanga anasema Simba walizembea.
Awali, Kondo alitua Simba siku chache tangu timu hiyo ilipoanza mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi lakini mabosi wa Msimbazi walichelewa kumpa mkataba na Yanga wakatumia mwanya huo.
Taarifa ambayo Championi Jumatano limethibitishiwa, imesema Kondo alitekwa na viongozi wa Yanga usiku akiwa matembezini na kupewa mkataba.
Kondo ambaye aliwahi kutua nchini Msumbiji alikokwenda kusaka timu, alikuwa tayari ameshakaribia kulamba mamilioni ya Simba, lakini Yanga wakashtuka haraka na kufanya utemi huo.
"Unajua kuna siku nilikuwa nazungumza na rafiki yangu mmoja akaniambia Mwalami (Mohamed) anasema kuna straika mmoja kinda amekuja hapa nchini akitokea nchini Msumbiji.
"Alimsifu kuwa ni hatari sana, tukawatuma watu wetu wakatuambia ni kweli yupo Simba anajaribiwa, tukaanza kumsaka taratibu," alisema bosi mmoja aliye katika Kamati ya Usajili ya Yanga huku akiongeza kwa kusema:
"Tulipata nafasi ya kuonana naye usiku tukabaini kwamba bado hajamalizana na Simba, hilo alituthibitishia yeye mwenyewe na tulipompa ofa yetu akaikubali tukamsainisha. Ni mchezaji mzuri, utamuona siku yoyote kuanzia kesho (jana)," alisema bosi huyo.