Mlalahoi.. hiyo ndiyo sauti inayotakiwa kusikika. Hata kama hawezi kuzungumza hadharani, basi aonekane hadharani kuwa ni mzima wa afya. Kama ni mgonjwa apelekwe hospitali na siyo kushikiliwa "ili atulie". Mnyezi Mungu ananjia nyingi za kuwaumbua watu!! Jambo likimtokea binti huyu kuna watu itapasa waseme. Kama amefanya kosa la kimaadili, hilo ni jambo moja la kumuangalia binadamu mwenzako kama "pensheni" na hivyo kufanya lolote lile ili "pensheni" isikatike ni kosa kubwa zaidi kwani wanamuangalia binadamu mwenzao kama kitu kinachoweza kutumiwa!
Katiba yetu iko wazi kuhusu hili (msisitizo wote wangu):
Ibara 16:1
Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi
kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na
unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na
mawasiliano yake ya binafsi.
Hivyo, kama Amina anatakiwa kuwasiliana na mtu yeyote basi waliomchukulia simu yake WANAVUNJA KATIBA
Ibara 17:1
Kila raia (hata kama ni Mbunge! M.M.) wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya
kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika
sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya
kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri
ya Muungano.
Wale ambao wanamlazimisha Amina kuwa mahali fulani wakati yeye anataka kuwa mahali kwingine WANAVUNJA KATIBA!
Ibara 18:1
Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru
kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta,
kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo
chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa
mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
Amina alitaka kutoa mawazo na maoni yake kama mtu huru. Kuna watu wametangaza hadharani ati wamemzuia! Kama Amina angekuwa mtoto wa miaka 18 wazazi wake kweli wangeweza kumsemea. Lakini akiwa mtu mzima tena Mbunge wa Bunge takatifu la Enzi la Jamhuri yetu Tukufu ya Muungano! anayo haki ya kutoa maoni yake bila "Mawasiliano yake kutoingiliwa kati". Waliokiri kufanya hivyo WANAVUNJA KATIBA!
Hivyo basi:
- Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Amina Chifupa Mpaka nje, apewe uhuru wake wa kusema, kuwaza, kwenda, kufanya atakalo bila kuingiliwa na mtu yeyote, kulazimishwa na mtu yeyote au kukwaza na mtu yeyote hata kama mtu huyu ni ndugu wa damu.
- Familia wanaweza kumshauri mtoto wao na ndugu yao kufanya lolote au kutofanya lolote, lakini kama amewaambia anataka kufanya jambo fulani na wao wanamng'ang'aniza asifanye wakati yeye akiwa na akili timamu na mtu huru anataka kufanya vinginevyo watu hao watishiwe kuchukuliwa hatua za kisheria wasipobadili vitendo vyao mara moja.
- Bi. Amina aachiliwe huru mara moja bila ya masharti yoyote na kama hataki kuzungumzia mambo ya ndoa yake hadharani huo ni uhuru wake na asilazimishwe na mtu yeyote kufanya hivyo. Na kama anataka kuzungumza hadharani basi asinyamazishwe na mtu yeyote hata kama mtu huyo ana malengo mazuri na nia nzuri!
Wenye kuchapisha tisheti chapesheni na picha yake muiweke hadharani hadi huyo binti aonekane hadharani mzima wa afya akiwa mtu huru!!! Uhuru katika nchi yetu siyo hisani ya wazazi wetu kwani Katiba inasema hivi:
Ibara 12:1
Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa.
Miongoni mwa binadamu hao ni Mhe. Amina wa Mpakanjia!!!!
hivyo basi,
FREE AMINA NOW!! FREE AMINA NOW! FREE AMINA NOW
chapisheni tsheti n.k!! ili liwe somo kwa watanzania kuwa nchi yetu bado huru na itaendelea kuwa huru!!!!