na Mwandishi Wetu
MBUNGE machachari wa Viti Maalumu (CCM), Amina Chifupa, amelazwa katika hospitali moja inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Habari za uhakika kutoka ndani ya hospitali hiyo zinasema, Chifupa alipokewa hospitalini hapo juzi usiku kwa ajili ya matibabu ya maradhi yanayomsumbua.
Vyanzo vya habari kutoka hospitalini hapo viliieleza Tanzania Daima jana kwamba Chifupa alikuwa amelazwa katika wodi ya watu maarufu (VIP) alikofanyiwa vipimo kadhaa na muda mfupi baadaye akaanzishiwa matibabu.
Habari zaidi kutoka hospitalini hapo zinaeleza kuwa wodi aliyolazwa mbunge huyo iko katika uangalizi wa karibu, kuliko ilivyo kawaida na watu wasiohusika hawaruhusiwi kufika katika eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, hata baada ya gazeti hili kupata taarifa za ndani kuhusu maradhi yanayomsumbua mwanasiasa huyo, limeamua kutotaja ugonjwa unaomsumbua kwa sasa.
Habari zaidi zinadai kwamba licha ya mbunge huyo kulazwa katika hospitali hiyo, jina lake halijaandikwa kwenye kitabu cha orodha ya wagonjwa na badala yake limeandikwa jina la ofisa mmoja wa jeshi.
"Chifupa kafikishwa hapa jana, na anasumbuliwa na … ila anatibiwa kwa siri kubwa na chini ya uangalizi mkali ambao unazuia hata sisi wafanyakazi wa hapa hospitali kutoikaribia wodi hiyo, labda uwe na shughuli maalumu," kilisema chanzo chetu.
Hivi karibuni Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alilitangazia Bunge kwamba Chifupa ni mgonjwa, ndiyo maana ameshindwa kuhudhuria Kikao cha Bunge la Bajeti kilichoanza mapema wiki iliyopita.
Chifupa, mbunge kijana, amepotea katika macho ya jamii kinyume cha ilivyo hulka yake, tangu habari za kutalikiwa na aliyekuwa mumewe, Mohamed Mpakanjia, Mei mwaka huu ziandikwe katika vyombo vya habari.
Tanzania Daima ndilo lilikuwa gazeti la mwisho kufanya mahojiano na mbunge huyo wakati masuala yake hayo ya ndoa yaliporipotiwa.