Kati ya Januari - Februari 2025 simu 169 zimepigwa kuripoti matukio ya Ukatili kwa Watoto Nchini

Kati ya Januari - Februari 2025 simu 169 zimepigwa kuripoti matukio ya Ukatili kwa Watoto Nchini

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2022
Posts
2,780
Reaction score
6,607
0310_001_page-0001.jpg

0310_001_page-0002.jpg

0310_001_page-0003.jpg

0310_001_page-0004.jpg

TAMKO LA MTANDAO WA ELIMU TANZANIA (TEN/MET) NA LHRC JUU YA MATUKIO YA KUJERUHIWA NA KUUAWA KWA WANAFUNZI KUTOKΑΝΑ ΝΑ ADHABU KALI YA VIBOKO MASHULENI

Dar es Salaam, Machi 11, 2025.
Ndugu waandishi wa habari

Tarehe 26 Februari 2025 ziliripotiwa taarifa kupitia vyombo vya habari za kufariki kwa mwanafunzi aitwaye Mhoja Maduhu wa kidato cha pili aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Mwasamba iliyopo wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu. Mhoja anadaiwa kufariki dunia baada ya kuadhibiwa kwa kuchapwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake na mwalimu aitwaye kupita kiwango kwa kosa la kutofanya kazi ya kikundi darasani.

Ndugu waandishi wa habari
LHRC na Mtandao wa Elimu Tanzania tunasikitishwa sana na tukio hili, ambalo si tu linakiuka haki za mtoto, bali pia linakwenda kinyume na sheria na miongozo ya elimu nchini. Tunatoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wenzake, na jamii kwa ujumla kwa msiba huu mzito, huku tukisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha haki inatendeka na mazingira ya shule yanakuwa salama kwa kila mwanafunzi.
Ndugu waandishi wa habari

Takwimu zinaonesha kwa kipindi kifupi cha Januari hadi Februari 2025 huduma ya simu ya kitaifa kwa watoto (116) inayoratibiwa na C-SEMA ilipokea jumla ya kesi 169. Kesi 52 zilikuwa za ukatili na unyanyasaji wa kimwili dhidi ya watoto, kati ya kesi hizo 52 wasichana kesi 21, huku wavulana kesi 31, Aina za ukatili zilizoripotiwa ni kupigwa, kung'atwa, kuchomwa moto sehemu mbalimbali za mwili na adhabu kali ya viboko. Kila siku huduma ya simu ya kitaifa kwa watoto hupokea zaidi ya mawasiliano 10,000 kutoka kwa watoto na jamii.

Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba matukio ya watoto, wanafunzi kufanyiwa vitendo vya ukatili unyanyasaji na ukatili wa jinsia hususani kupewa adhabu kali ya viboko ni nyingi sana katika jamii yetu, ni ukweli usiopingika kwamba suala hili halina manufaa na linapaswa kukomeshwa.

Mahakama ya Afrika mwaka 2024 ilitoa maamuzi kukomesha adhabu ya viboko katika mifumo ya haki ikielezea kuwa adhabu hizo zinatweza utu wa mwanadamu na zinatakiwa kukomeshwa. Ni dhahiri kuwa adhabu za viboko si nzuri kwa binadamu yoyote kwani zinatweza utu na kusababisha maumivu makali yanayoweza kuwa ya kudumu au ya muda mfupi au pengine kupelekea kifo.

Mtandao una maoni kuwa bado kuna changamoto katika utekelezaji wa miongozo ya nidhamu mashuleni. Tukio hili linafanana na lile la mwaka 2018, ambapo mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta, Bukoba, alifariki dunia kutokana na adhabu ya viboko. Adhabu za viboko mashuleni zimeendelea kufanyika hata baada ya taarifa nyingi zanazoonyesha madhara yake.

Ndugu waandishi wa habari
Aidha, mnamo tarehe 4 Machi 2025 mtandao ulipokea taarifa kutoka kwa moja ya wananchi juu ya kuvunjwa mkono kwa mwanafunzi aitwae Khudhaifa Salim Hamisi anayesoma darasa la pili shule ya Msingi Msufini iliyopo kata ya Chamazi wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es Salaam. Mwanafunzi huyu alivunjika mkono baada ya kipigo kikali kutoka kwa mwalimu wake. Kwa mujibu wa taarifa, licha ya tukio hilo kuripotiwa katika kituo cha polisi Mbande kilichopo Mbagala wilaya ya Temeke hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka sasa.
Ndugu waandishi wa habari.

Kuongezeka kwa matukio haya pia kunachangiwa na baadhi ya wazazi kutokuwa na utayari kuyaripoti matukio ya aina hii katika vyombo vya dola ili hatua sitahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika. Wazazi wasio tayari kutoa taarifa wamekuwa wakifanya mazungumzo na familia za watuhumiwa nje na utaratibu uliopo kisheria na wakati mwingine wamekuwa wakipokea fedha zinazodaiwa za matibabu su fidia kinyume cha sheria.

Licha ya juhudi mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya mbinu mbadala za malezi na nidhamu, vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi bado vinaendelea kushuhudiwa ndani ya shule nchini, jambo linaloashiria udhaifu katika utekelezaji wa miongozo na sheria zinazosimamia haki za mtoto ndani ya mfumo wa elimu.

Ndugu waandishi wa habari
TEN/MET na LHRC kupitia afua mbalimbali za kupinga ukatili wa kijinsia mashuleni, tumekuwa tukihamasisha jamii na walimu kuhusu matumizi ya mbinu mbadala za kudhibiti nidhamu ya wanafunzi bila kutumia viboko na adhabu kali. Tumekuwa tukitumia majukwaa ya uchechemuzi na vikao vya kisekta kujadili na kuomba mabadiliko ya sheria na miongozo ili kuboresha ulinzi na usalama wa wanafunzi wakiwa shuleni na nje ya shule.

Ndugu waandishi wa habari
Tunaendelea kushirikiana na wadau wa elimu, serikali, na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa.
mazingira ya kujifunzia yanakuwa salama, jumuishi, na yanayozingatia haki za watoto kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Mtoto ya 2009, na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za watoto, kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (UNCRC), the UN Convention on the Rights of the Child (CRC)) ambao Tanzania imeridhia miaka 19 iliyopita na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto [The African Charter on The Rights and Welfare of The Child].

Mwisho, LHRC na TEN/MET tunashauri kama ifuatavyo:

1. Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na mapitio yake, na kuweka vifungu vya sheria vinavyopiga marufuku matumizi ya viboko shuleni na adhabu nyinginezo zinazoathiri haki ya kuishi ustawi, na utu wa mtoto. Marekebisho haya yataimarisha mfumo wa ulinzi na usalama wa wanafunzi na kuondoa mianya ya matumizi mabaya ya mamlaka na nguvu dhidi ya wanafunzi, hatua ambayo itasaidia kuzuia vitendo vya ukatili ndani na nje ya shule.

2. Tunaiomba Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia itoe waraka rasmi (circular) unaoelekeza walimu wote kuacha matumizi ya adhabu za viboko na kuelekeza mbinu mbadala za nidhamu zinazolinda utu na haki za watoto, wakati mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Elimu ukiendelea.

3. Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa kuanzishwa Madawati ya Ulinzi na usalama kwenye shule zote ifikapo mwaka 2029. Madawati haya yanatoa mfumo rasmi wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya watoto wanaokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali shuleni.

4. Hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na tukio hili la kikatili na matukio mengine yanayofanana na hili ambayo yamevunja haki ya msingi ya mtoto ya kuishi, kinyume na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Serikali iendelee kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa waathiriwa wa ukatili mashuleni na kwamba wahusika wanawajibishwa ipasavyo ili kutoa ujumbe wa wazi kuwa ukatili dhidi ya watoto na wanafunzi wote hautavumilika na haukubaliki.
5. Serikali iwekeze katika adhabu mbadala zisizotweza utu wala kutishia maslahi ya watoto na wanafunzi kwa ujumla,

6. Serikali ifuatilie pia adhabu zingine ambazo sio za viboko lakini ni mbaya na zinatweza utu wa watoto na kuwasababishia maumivu ya muda mrefu ya kimwili na kiakili.

7. Adhabu za viboko zimekuwa ni moja ya sababu za kuongezeka kwa utoro mashuleni, hivyo serikali ikomeshe adhabu hizi ili kuhakikisha wanafunzi wanabaki shuleni, wanandelea na masomo na kukamilisha mzunguko wao wa Elimu katika ngazi husika bila vitisho vyovyote.

8. Wazazi watoe taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapopata taarifa za kuumizwa au kuuawa kwa watoto wao na kuacha tabia ya kufanya mazungumzo na familia za watuhumiwa kwa lengo la kutaka kulimaliza jambo husika nje ya mfumo wa kisheria.

9. Wizara ya Elimu kupitia ofisi ya kamishina wa elimu iviimarishe vitengo vya udhibiti ubora wa elimu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosha, upatikanaji wa vitendea kazi na utolewaji wa mafunzo ya mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kikamilifu.

10. Wanajamii watoe taarifa za matukio ya aina hii kwa haraka au punde tu wanapopata taarifa za kutokea kwayo.

Imetolewa na:
Fulgence Massawe (Wakili)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji-LHRC


Martha Makala
Mratibu Kitaifa-TEN/MET

Pia soma ~ Simiyu: Mwanafunzi adaiwa kufariki kwa kuchapwa viboko na kukanyagwa kichwani na mwalimu shuleni
 
Back
Top Bottom