Pamekuwa na kambi mbili katika uteuzi huu na msaada wa wadau wa katiba na sheria unaweza kutupa mwanga.
Najua kuna jukwaa la mambo ya sheria lakini uteuzi huu una athari za kisiasa ambazo inawezekana kwa sasa hazipo wazi.
Tusaidieni tujue ukweli ni upi?
Mkuu, imekaa hivi:
1. Neno "Katibu Mkuu Kiongozi" halijaandikwa mahali popote kwenye Katiba ya JMT, 1977 (as amended);
2. Ibara ya 36 (1) na (2) ya Katiba ya JMT, 1977, inampatia mamlaka Rais kufanya uteuzi wa nafasi mbalimbali za watendaji wakuu wa serikali ikiwemo "Katibu Mkuu Kiongozi ";
3. Kwa muktadha wa Ibara ya 36 (2) ya Katiba ya JMT, 1977, Bunge limetunga Sheria ya Utumishi wa Umma (marejeo ya mwaka 2019) ambapo Kifungu cha 4(1) cha Sheria kinamtaka wazi kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya kumteua "Katibu Mkuu Kiongozi";
4. Labda kama kuna sheria au miongozo mingine ambayo sifahamu inayosimamia uteuzi wa "Katibu Mkuu Kiongozi", katika utafiti wangu mfupi nimegundua kuwa kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, 2019, au hata Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009 (Toleo la Tatu), hazijaweka wazi sifa za mtu anayetakiwa kuteuliwa kushika wadhifa wa "Katibu Mkuu Kiongozi". Kwa msingi huu, Rais anayo nafasi ya kumteua mtu yeyote ambaye anaamini atamsaidia vema ktk kutekeleza majukumu yake katika nafasi ya "Katibu Mkuu Kiongozi"; na
5. Pamoja na wajibu mwingine, Katibu Mkuu Kiongozi aliyeteuliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 4 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, 2019, ndiye anakuwa "Katibu wa Baraza la Mawaziri" kama ilivyotajwa katika Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, 2019, na Ibara ya 60 ya Katiba ya JMT, 1977.
Kwa imani yangu thabiti, uteuzi wa Dr. Bashiru kuwa "Katibu Mkuu Kiongozi" ni sahihi na halali na hakuna Katiba au sheria iliyovunjwa.
Maandishi yanayosambaza mitandaoni kuhusu sifa za mtu anayetakiwa kuteuliwa kushika nafasi ya "Katibu Mkuu Kiongozi" ni mojawapo ya Ibara katika Katiba iliyopendekezwa na Jaji Warioba.
Katiba ya Jaji Warioba haikupitishwa na haitumiki popote. Kwa hiyo, sio sahihi kufanya marejeo katika sheria ambayo haipo.
By the way, Katiba ya Jaji Warioba iliweka utaratibu mzuri sana wa namna ya kumpata "Katibu Mkuu Kiongozi" na nafasi zingine ktk utumishi wa umma.
Nawasilisha.