Mindyou
JF-Expert Member
- Sep 2, 2024
- 1,869
- 4,877
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema uamuzi wa Tanzania kuchukua umeme Ethiopia ni kitu chenye faida na si hasara kama watu wanavyodhani.
Mramba amesema ni faida kwa kuwa baadhi ya vyanzo vya umeme hapa nchini vinazalisha uniti moja kwa bei kubwa kuliko bei ambayo umeme huo utanunuliwa kutoka Ethiopia.
"Huo umeme wa Ethiopia tunanunua kwa senti za Marekani 0.077 lakini tuna vyanzo vingi ambavyo vinazalisha kwa gharama ya juu zaidi, hivyo hii ni nafuu kwetu," amesema na kuongeza umeme utaonunuliwa Ethiopia ni Megawati 100 tu.
Amesema umeme unaopelekwa mikoa ya Kaskazini unapotea kwa kiwango cha megawati 17 ambazo zinatosha kuhudumia Mkoa wa Songwe (unaotumia Mega 14) na zaidi.
"Hata huo wetu unaokuja kutoka Ethiopia utakuwa na hasara lakini hiyo hasara haituhusu, sisi tunanunulia mpakani Namanga, lakini tukipeleka sisi (umeme) tunatumia gharama kubwa," amesema Mramba.
Ameongeza kuwa "wachumi na wataalamu wote waliofanya tathmini juu ya jambo hilo waliona ni faida kubwa kuliko hasara"
Aidha, Mramba alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ununuzi wa umeme huo na kuongeza kuwa ufafanuzi uliotolewa na Msemaji wa Serikali baada kuibuka kwa mjadala huo uko sahihi.
"Maelezo ya msemaji wa Serikali yako sawa, hayana dosari," amesema Mramba na kuongeza kuwa suala la mauziano ya umeme ya nchi na nchi ni la kawaida na mpaka sasa Tanzania inauza na kununua umeme kutoka mataifa tofauti zaidi ya matatu.