Je, MABEYO AMESEMA YOTE JUU YA NI NINI KILIMSIBU RAIS MAGUFULI KABLA HAJAFA?
'Kisha, baada ya miaka mitatu, nilipanda kwenda Yerusalemu, ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano' - Mtume Paulo (Wagalatia 1:18).
Katika kitabu chake kiitwacho 'Paul and Peter Meeting in Jerusalem', Askofu Prof. Kenneth Cragg wa Church of England alifafanua mstari huo katika kurasa 96. Katika kitabu hicho, Prof. Cragg alijaribu kujibu swali hili: Je, katika siku hizo 15, Kefa (Mtume Petro) na Mtume Paulo waliongea nini? Lakini hoja kwa nini maudhui ya maongezi hayapo katika kitabu cho chote cha Paulo haijajibiwa na Prof. Cragg. Hii ndio sehemu ya utafiti ambao Askofu Mwamakula amekuwa akifikiria kuufanya baadaye.
Wakati Askofu akiwaza hayo, Mkuu wa Majeshi mstaafu wa Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo aliibuka na kuongea na vyombo vya habari kuhusu kifo cha Rais Magufuli tarehe 17 Machi 2021. Jenerali Mabeyo alitumia muda mfupi (pengine saa 1) kuongea na wanahabari juu ya nini kilitokea kwa Rais Magufuli ndani ya kipindi cha masaa 24 kuanzia kati ya tarehe 16 na 17 Machi 2021.
Jenerali Mabeyo ameacha maswali mengi kwa watu ambayo pengine pia yatahitaji kujibiwa na waandishi wa habari za uchunguzi, watafiti na hata wana usalama katika miaka mingi ijayo. Baadhi ya maswali ni: Je, kwa nini katika saa za mwisho za maisha yake hapa duniani, Rais Magufuli hakuruhusiwa kuwa na familia yake - mke au watoto? Je, ni kitu gani kilichelewesha kuapishwa kwa Makamu wa Rais kuwa Rais hadi baada ya siku mbili badala ya masaa 24?
Je, kwa nini taarifa za msiba asipewe kwanza Makamu wa Rais, badala yake wakapata Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi? Je, kule Tanga alikokuwa Makamu wa Rais na kule Dodoma walikokuwa hao wengine wapi ndio karibu? Je, kulikuwa na 'mzozo' wa kutaka aapishwe mtu mwingine badala ya Makamu wa Rais? Je, huo 'mzozo' kama ulikuwepo na pengine kupelekea kuchelewesha kuapa, ulianzishwa na nani? Je, nani aliyekuwa anakusudiwa kuapa badala ya Makamu wa Rais?
Je, kuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya juu miongoni mwa aliowasema Mabeyo ambaye angeweza kusahau katiba inasema nini juu ya lililotokea wakati alikuwa ameapa kuilinda? Je, maelezo ya msemaji wa familia wakati ule wa msiba na maelezo ya Jenerali Mabeyo kuhusu sala ya mwisho kwa namna gani yanalingana na kwa namna gani yanatofautiana? Kama ipo tofauti, ni makusudi au nahati mbaya? Je, kama kuna tofauti, umma ufuate maelezo ya nani? Je, zile siku kadhaa kabla ya kifo chake (kipindi cha ikimya), Rais alikuwa wapi? Je, alitoa wosia au maelekezo gani? Kama aliweza kutoa amri kutaka arejeshwe nyumbani wakati amezidiwa, alishindwaje kutoa amri ya kutaka familia yake?
Ili kuyajibu maswali yote hayo itahitajika utafiti utakaotoa maelezo ya kutosha kuandika kitabu chenye kurasa 2000. Kuishi na watu wa aina ya Askofu Mwamakula inahitaji uvumilivu mwingi. Ukuikosa uvumilivu unaweza kumtumbukiza katika pipa la tindikali ili kumbukumbu ya mwili wake isiwepo, asipelekwe Itunge katika Isyeto (makaburi) la Chifu Mwamakula. Maswali yake hufanya watu waanze kufikiria kinachofanyika katika 'Sayari ya Mirithi'!
Kama Jenerali Mabeyo, angenyamaza kimya, Mwamakula angekuja na maswali yake haya ya 'kipumbavu'? Je, ni kwa nini watu husema chini chini wakijiuliza maswali kama hayo? Je, watu wanaogopa nini kuyajadili wakati Jenerali pia Mabeyo ameamua kufunua pipa jalalani? Hivi mtu akilifunua pipa jalalani, utawezaje kulaumu na kuwaadhibu kuku wanaochakura wadudu?
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Dar es Salaam, 18 Machi 2024; saa 12:25 jioni
View attachment 2938629