Sidhani kama Kenyatta anastahili lawama katika hili la ukikuyu. Mzee Kenyatta alitawala miaka 15, tena akiwa babu. Alifanya kazi na Jaramogi Odinga kidogo, halafu miaka mingi na Moi. Hasa ile miaka ya 1970's basically ni Moi alikuwa anaendesha hiyo nchi, mzee Kenyatta alishajichokea! Na hata baada ya hapo, Moi alipata miaka mingine 24, muda wa kutosha kabisa kurekebisha kasoro hizo. Moi alisema anafuata "nyayo", binafsi sielewi ni nyayo zipi, lakini kama alifuata hizo za siasa za ukabila, wakenya ni mashahidi, na wanaosoma hii forum wanaweza kutoa maoni yao.
Miaka ile ya 1970's, wakenya wengi waliopinga serikali ya Kenya walikuwa wakikuyu pia, japo mzee Kenyatta mkikuyu mwenzao alikuwa madarakani. Ukisoma maandishi ya akina Ngugi wa Thiong'o, Ngugi wa Mirii, Micere Mugo, n.k., na mambo yaliyowapata baada ya kuandika maandishi hayo hutahitaji ushahidi zaidi. Vitabu vya Ngugi kama "Detained" na "Devil on the Cross" vinashambulia serikali moja kwa moja. Vingine "A Grain of Wheat", "Petals of Blood", vyote wanalia kuwa uhuru bado. Mzee Odinga naye kilio chake kilikuwa hichohicho alipoandika "Not Yet Uhuru", lakini kwa sababu ya mizizi ya ukabila iliyokuwapo tangu kabla, hakuweza kuungana na hawa wakikuyu ingawa wote walikuwa wakipinga serikali hiyohiyo katika muktadha uleule. Na waandishi wa kikikuyu wakaamua kujitoa wazi na kuanza kutukuza "ukikuyu" badala ya u-Kenya. Alishaanza Ngugi wa Thiong'o ku-blend upinzani wa kisiasa na utamaduni wa kikikuyu kwenye "The River Between" na "Weep Not, Child", akitukuza hasa mila ya ukeketaji na kubeza wasiotahiriwa. Akaleta nyingine ya kikikuyu kabisa "Ngaahika Ndeenda-I will marry when I want", na siku hizi naambiwa ameamua kuandika kikikuyu tu, wala hata si kiswahili ambayo huko Kenya ni lugha ya Taifa!
Kwa hiyo kwa kutazama fasihi, ambayo kwayo kimsingi jamii hujidhihirisha kwa jamii nyingine, tunaona kuwa jamii ya Kenya haikuanza ukabila na Kenyatta wala Kibaki. Mizizi hiyo ilikuwapo tangu kabla ya uhuru, na kuna watu wangependa ibaki hivyo, na wamekuwa wakiitetea waziwazi. Viongozi wangeweza kutumia uzalendo kurekebisha hali hiyo tangu mapema. Kenyatta alikuwepo kwa miaka 15, ambayo mingi ya hiyo Moi alifanya kazi za urais (akiwa makamu) chini ya kivuli cha "babu", hadi mzee wa watu alipojifia kwa amani usingizini mwaka 1978. Moi ambaye hujulikana pia kama "profesa" wa siasa za Kenya akachukua nafasi hiyo kwa miaka 24, na kwa hakika amekuwa rais wa Kenya hadi leo hii, (inadaiwa "Mwai Kibaki" humaanisha pia "Moi Kabaki").
Kwa hiyo nani hakutimiza wajibu wake katika kupambana na jinamizi la ukabila huko Kenya? Jibu mnalo!