Nimeanza kuona kuwa sasa kweli Kibaki amerudi and he is there to stay. Watu wameanza kuizoea hali na kidogokidogo wanaikubali, hata hapa kwenye forum wanaonesha hivyo. Hasira zimepungua. Punde mambo mengine kama mahitaji ya kimaisha (chakula, huduma mbalimbali) yatachukua nafasi, na watu watarudi kuwatafutia watoto wao nafasi za shule, ni januari hii. Chuma kinaelekea kupoa, hakitapondeka tena. Raila na wenzie wamesahau msemo huu "strike the iron while it's still hot". Bw Odinga, chuma chapoa hicho, kallaghabaho!
Mambo haya yapo sana kwetu. Ukipata taarifa za msiba unajitupa chini na kujigalagaza huku ukiangua kilio, unachafuka kila mahali. Ajabu siku ya mazishi unaonekana na suti mpya nyeusi, tena nyote na nduguzo kama sare, hata tunashangaa mlipataje muda wa kufikiria sare kama mlikuwa na uchungu kiasi hicho. Baada ya maziko, siku hiyohiyo inafuata pilau, ndizi mbivu na vinywaji. Wale waliokuwa wanajigaragaza chini tunawaona wanacheza karata na kutaniana! Kila kitu kinasahaulika, maisha yanaendelea! Ndivyo tunavyosahau msiba, na ndiko Raila na wenzie wanakoelekea, hivi punde watasahau yote, kama mwendo ndio huu wa kusuasua. Yetu macho!